googleAds

YANGA, AZAM ZIELEKEZE NGUVU MICHUANO YA AFRIKA

YANGA imepata uzoefu  kwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea viwasini Zanzibar, licha ya kutolewa na Simba  kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare tasa ndani ya dakika 90  katika  mchezo wa  hatua ya Nusu Fainali uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan.

Kombe hilo la Mapinduzi lililoshirikisha timu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara; Azam, Simba na Yanga, URA ya Uganda na timu nne wenyeji za Zanzibar, fainali inatarajia kuchezwa kesho kwenye uwanja huo, ambapo Simba na Azam ndizo zimefanikiwa kupenya hatua hiyo.

Hapakuwa na namna yoyote kwani timu moja lazima ingetinga fainali na nyingine kubaki kwa kuwa matokeo ya mpira yana matokeo matatu.

Tunaamini kwamba michuano ya Kombe la Mapinduzi  imewapa kipimo tosha Yanga katika harakati zao za kujiandaa na mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, lakini Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam watakaoshiriki Kombe la Shirikisho litakaloanza mwezi ujao.

Kupitia Kombe la Mapinduzi, tunaamini kwamba benchi la ufundi la Yanga litakuwa limeona ubora na upungufu wa wachezaji na italifanyia kazi mapungufu hayo kabla ya kuanza kwa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunaamini kwamba, Yanga kutofika fainali kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, hakumaanishi kuwa timu ilikuwa mbovu, bali ni matokeo unayoyatarajia kuyapata katika mchezo wa soka.

Kama  tulivyosema mpira una matokeo matatu kushinda, kufungwa na kutoka sare, hayo ndiyo yaliyotokea kwa upande wa Yanga, lakini wanatakiwa kusahau na Azam na Yanga  zielekeze nguvu zaidi katika michuano mikubwa  ya Afrika.

Kwa upande wetu, BINGWA bado tunaona Yanga ni timu nzuri na ikijipanga kikamilifu inaweza kuwa ni mwakilishi bora kwenye  Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.

Kwa kutambua umuhimu wa ligi hiyo na  benchi la ufundi la Yanga litakuwa limeweka mikakati ya kuhakikisha wanaandaa kikosi cha ushindi, lakini  likianzia kufanyia kazi upungufu uliojitokeza kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Tunaamini kwamba, kwa kufanya hivyo kutawapa fursa wachezaji wa timu hiyo kujua udhaifu wao, lakini kupata mbinu mpya zitakazowafanya wasahihishe makosa yao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*