googleAds

YALIYOPITA STARS SI NDWELE, TUGANGE YAJAYO

WIKI iliyopita kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, aliwasamehe wachezaji aliowazuia kujiunga na kikosi chake kutokana na kuchelewa kuripoti kambini kwa wakati.

Kitendo hicho kilionekana kuwagawa wadau wa soka nchini, baadhi wakiunga mkono kama sehemu ya kukomesha utovu wa nidhamu kwa wachezaji wetu, huku wengine wakipendekeza nyota hao wajumuishwe kundini kwa kuwa ni kosa lao la kwanza.

Wachezaji hao ni Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Shomari Kapombe, John Bocco, Erasto Nyoni na Hassan Dilunga wa Simba pamoja na Feisal Salim ‘Fei Toto’ wa Yanga.

Baada ya kuwatema hao, nafasi zao zimechukuliwa na Ally Sonso na Paul Ngalema (Lipuli FC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), David Mwantika, Frank Domayo (Azam FC), Salum Kihimbwa na Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar).

Baada ya kikao baina ya kocha huyo sambamba na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na viongozi wa Simba, pande hizo mbili zilifikia mwafaka na wachezaji hao kusamehewa.

Hata hivyo, Amunike aligoma kuwajumuisha na wenzao wanaojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda, jijini Kampala, Septemba 8, mwaka huu.

Kocha huyo raia wa Nigeria, alisema pamoja na kuwasamehe wachezaji hao, bado watasubiri wakati mwingine kuitwa Stars, lakini tu iwapo wataendelea kuonyesha viwango vya juu wakiwa na timu za klabu zao.

BINGWA tukiwa kama wadau wa soka kama ilivyo kwa michezo mingine hapa nchini, tunadhani ni vema wapenzi wa mchezo huo unaopendwa zaidi duniani kufunga mjadala juu ya kuenguliwa Stars kwa wachezaji hao na badala yake kuganga yajayo.

Tunaamini kuwa uamuzi huo wa kuwasamehe wachezaji hao umeonyesha kwamba Amunike alikuwa na mpango mzuri wa kuwa na timu yenye wachezaji ambao wana nidhamu, jambo ambalo ni muhimu na hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana kama hakuna nidhamu.

BINGWA tunasema yaliyopita si ndwele sasa ni wakati wa Stars kuganga yajayo.

Ndio ni wakati wa kuganga yajayo kwa kuwa mechi hiyo ni muhimu sana na ni ngumu kwa aina ya timu ambayo Stars inakwenda kukutana nayo.

Uganda imekuwa ikiisumbua sana Stars kila tunapokutana nao, iwe mechi za kirafiki au za michuano mbalimbali, huku ukizingatia wako nafasi za juu kwenye viwango vya ubora.

Uganda wako nafasi ya 82 huku Stars ya 140 katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) vya mwezi Julai.

Basi ni wakati wa TFF, klabu mbalimbali na mashabiki kuwaunga mkono Amunike na vijana wake waweze kufanya vizuri kwenye mchezo huo utakochezwa mjini Kampala.

MWISHO


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*