googleAds

Winga ‘fundi’ bado kidogo Simba

NA ASHA KIGUNDULA

WAKATI mashabiki wa Simba wakiwa na hamu ya kuona makali ya Luis Maquisonne, baada ya kuonjeshwa kidogo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi,uongozi wa klabu hiyo umesema unashughulikia kibali chake cha kimataifa, suala ambalo litachukua muda mfupi kukamilika.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema bado wanasubiri kibali cha Kimataifa (ITC) cha mchezaji wao huyo kutoka klabu ya UD Songo ya Msumbiji, ambayo alikuwa kwa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

“Kibali cha Luis bado, siku si nyingi kitapatikana na kuanza rasmi kuitumikia klabu yetu ya Simba. Kila kitu kimefanyika, bado kibali tu, ambacho kitatua muda wowote kuanzia sasa,” alisema Manara akimzungumzia mchezaji huyo wa kimataifa wa Msumbiji.

Aidha, Manara alisema hali ya mchezaji wao, Deo Kanda, inaendelea vizuri, ambapo baada ya mechi tatu kutoka sasa atajiunga na wachezaji wenzake kuendelea na majukumu yake ndani ya kikosi hicho.

Alisema Kanda aliyeumia katika mechi yao dhidi ya Yanga anaendelea vizuri na ameanza mazoezi mepesi na wachezaji wenzake.

Aliongeza kuwa mbali ya Kanda, klabu hiyo ilikuwa na majeruhi mwingine, ambaye ni Hassan Dilunga, lakini sasa anaendelea vizuri baada ya kuumia katika mchezo wao dhidi ya Alliance ya Mwanza. “Dilunga anaendelea vizuri, hata mazoezi ya pamoja ameshaanza…” alisema Manara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*