WENGER NA JINAMIZI LA DAKIKA 90 UGENINI

NA AYOUB HINJO    |

KUNA mambo yamebadilika Arsenal, hasa kipindi hiki ambacho wamekuwa ‘busy’ kuwaza Kombe la Ligi ya Europa. Wakati mwingine si utamaduni wao, sababu Arsene Wenger, ni kocha mshindi mara zote lakini kipindi hiki amekuwa na sura nyingi zisizoeleweka.

Kwa namna moja au nyingine, amekuwa akibishana na maamuzi yake mwenyewe. Nafikiri kila mmoja anakumbuka wakati msimu unaanza alipotuaminisha timu yake inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Ghafla niliwaza jinsi ligi ilivyoanza kwa wao kushiriki Ligi ya Europa, bado naamini Europa ni michuano migumu zaidi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Muda na nguvu inayotumika ni kubwa sana, nililiona hilo wakati Manchester United, msimu uliopita walipoamua kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya michuano hiyo.

Kadiri muda ulivyokuwa unasogea, hata sura ya Jose Mourinho ilizidi kubadilika nakuamua kucheza kamari ya kukubali yaishe katika Ligi Kuu na nguvu zote zilihamia Europa na mwisho wa siku kamari yake alishinda.

Lakini haikuwanyima fursa ya kushindwa kushinda michezo yao ya Ligi Kuu hasa nje ya uwanja wao wa Old Trafford, Mourinho alijitahidi kuweka uwiano hasa katika uteuzi wa kikosi na kutoa nafasi kwa wachezaji wake kujitambua nini wanakifanya.

Tangu kuanza kwa msimu huu mambo hayaendi sawa katika kikosi cha Arsenal, kila wanachokifanya kinaonekana kuleta ugumu katika Ligi Kuu.

Inawezekana nguvu wanayoitumia Europa inawaumiza sasa, lakini cha kusikitisha ni jinsi ambavyo wamekuwa na matokeo mabaya wanapokuwa ugenini.

Tangu mwaka 2018 uingie, timu hiyo haijafanikiwa kushinda mchezo wowote katika uwanja wa ugenini. Michezo mitano wamefungwa yote.

Michezo hiyo ilikuwa dhidi ya Bournemouth waliofungwa 2-1, Swansea 3-1, Tottenham 1-0, Brighton 2-1 na Newcastle United 2-1.

Haijawahi kutokea katika kikosi hicho, hii ni mara ya kwanza kushindwa kupata pointi katika viwanja vya ugenini. Najaribu kuitazama sura ya Wenger, anaonekana hana presha kabisa.

Kadiri muda unavyosonga, wamekuwa wanasikitisha sana. Ghafla nilirudisha kumbukumbu wakati Wenger anaamini kikosi chake kitatwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Lakini pia hakuonekana kabisa kuitolea macho michuano ya Europa, hadi sasa muda umeamua kusema ukweli juu ya mwenendo wa kikosi hicho.

Kuna mambo kadhaa yanakifanya kikosi hicho kishindwe kupata matokeo ugenini na hatimaye limekuwa jinamizi kubwa kwa Wenger.

Moja, safu ya ulinzi haina mawasiliano mazuri tangu kuanza kwa msimu wameruhusu mabao mengi sana ya kizembe. Wamefungwa mabao 45.

Mara nyingi mabeki wao wamekuwa na makosa mengi ambayo mwisho wa siku huiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu sana wa kupata matokeo.

Kuanzia kwenye kiungo cha ulinzi, kumekuwa na matatizo makubwa sana. Hakuna anayefanya kazi yake ipasavyo na hatimaye timu hiyo hujikuta katika wakati mgumu pindi mashambulizi ya wapinzani yanapoelekezwa kwao. Hadi sasa wamefungwa michezo 11.

Mbili, wanapokuwa uwanja wa nyumbani wanatumia nguvu kubwa kupata matokeo wakiwa na kiwango bora katika kila idara. Lakini wanapokuwa ugenini, wanakosa mwendelezo wa ubora wao.

Wachezaji wanashindwa kutimiza majukumu yao, makosa yao yanaipelekea timu hiyo kuwa katika wakati mgumu hasa wanapokuwa katika shinikizo la kupokea mashambulizi ya wapinzani.

Tatu, Wenger amekosa mbinu mbadala ya kikosi chake kupata matokeo hasa wanapokuwa katika viwanja vya ugenini. Hushindwa nini cha kufanya ili timu yake ivunje ngome ya wapinzani.

Alexandre Lacazatte, alipotangulia kufunga bao dhidi ya Newcastle, ilionekana kuwa ni kitu ambacho kinaweza kuwapa ahueni, lakini baada ya bao hilo hakukuwa na kilichoendelea tena zaidi ya timu hiyo kufungwa mabao mawili.

Msimu huu Arsenal inashika nafasi ya mwisho kwa kushindwa kufunga bao la ‘counter attack’, wameshindwa kutengeneza mashambulizi ya haraka kuelekea kwa wapinzani.

Licha ya kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa, kasi na muunganiko mzuri bado wameshindwa kufunga mabao muhimu kwao. Katika orodha hiyo wanaungana na timu za Swansea, Bournemouth, Brighton na Burnley.

Mara nyingi mipira mirefu husaidia kuua mchezo pindi mpinzani wako anapokuwa anakushambulia, lakini mbinu za Wenger zinaonekana kuwa tofauti katika hilo.

Nne, inawezekana wachezaji wa Arsenal wanasumbuliwa na tatizo la saikolojia? Mara kadhaa hushindwa kucheza katika viwango vyao wanapokuwa ugenini, hasa mbele ya mashabiki wanaoshangilia kwa nguvu na fujo.

Mechi hizo zote wameshindwa kucheza na mwisho wa siku walipoteza michezo hiyo. Inawezekana tatizo la kisaikolojia likawa linawasumbua.

Hapo baadaye watakuwa na michezo kadhaa ugenini, ikiwemo mchezo muhimu dhidi ya Atletico Madrid katika Ligi ya Europa. Watafanikiwa kupata matokeo na kwenda fainali?

Naamini kwa sasa hakuna kingine wanachokiangalia zaidi ya michuano hiyo, ili waweze kurudi katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, nje ya hapo watakuwa kwenye wakati mgumu sana.

Manchester United waliweza baada ya kuona hawataweza kufanya chochote katika Ligi Kuu, je, Wenger na vijana wake wataweza kushinda kombe hilo? Wenger ajitazame tena.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*