WENGER ALILIA VAR LIGI KUU ENGLAND

  LONDON,   England     |  

KOCHA Arsene Wenger amesema kwamba anavyoamini Ligi Kuu ya England itakuwa imeachwa na nyingine duniani, baada ya uamuzi wa kutotumika teknolojia ya goli ya   VAR msimu ujao.

Kilio hicho cha kocha huyo wa Gunners, kimekuja baada ya juzi kubaki amefadhaika kwa kushindwa kupewa penalti katika mchezo ambao walifungwa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United.

Huku wageni wakiwa wanaongoza 1-0 katika mchezo huo ambao ulipigwa katika dimba la St. James’ Park, inaonekana shuti lilipopigwa na   Pierre-Emerick Aubameyang kabla ya kupaa juu ya lango lilimbabatiza mkononi beki, Jamaal Lascelles,     ambaye alikuwa akijaribu kuzuia mpira huo.

Hata hivyo, mwamuzi, Anthony Taylor, aliamua upigwe mpira wa kona badala ya penalti na kisha Newcastle wakafanikiwa kupata bao dakika 12 baadae kupitia kwa nyota wao, Ayoze Perez.

Huku klabu nyingi za Ligi Kuu zikiwa zimeshapiga kura ya kupinga kutumika utaratibu huo wa VAR katika mashindano hayo, Wenger anafikiri kuwa matukio kama haya yataendelea kuvuruga mechi.

“Mwamuzi ni mwamuzi,” Wenger aliuambia mkutano wa waandishi wa habari. “Kile ambacho kinatakiwa ni kumsaidia mwamuzi, lakini kwa bahati mbaya Ligi Kuu wameamua kutotumia VAR. Nadhani huu ni uamuzi mbaya mno,”   aliongeza kocha huyo.

“Nafikiri kwa uamuzi huu tutakuwa tumebaki nyuma ya ulimwengu,” alikwenda mbali zaidi kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*