WENGER AKUBALI YAISHE

LONDON, England

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, ni kama amekata tamaa baada ya kukiri kwamba itakuwa vigumu kwa timu yake kumaliza ligi msimu huu ikiwa kwenye orodha ya nne bora, kufuatia kipigo cha juzi walichokipata dhidi ya Tottenham.

Mabao ya haraka kutoka kwa Dele Alli na Harry Kane kipindi cha pili katika mechi hiyo maarufu kama North London derby yalitosha kuihakikishia Spurs kumaliza juu ya Arsenal msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 1995, kadhalika kuweka hai matumaini yao ya kufukuzia ubingwa.

Arsenal, kwa namna nyingine, wapo nyuma kwa pointi sita kuifikia timu ya nne bora wakiwa na mechi mkononi, lakini Wenger amesisitiza kuwa kikosi chake hakitakata tamaa katika jitihada zao kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

“Itakuwa kazi ngumu sana sasa, lakini hatuna budi kupambana,” aliwaambia waandishi.

“Tuna mechi ya fainali Kombe la FA, bado tunayo nafasi kutinga nne bora na tutajitahidi kusahau yaliyotokea leo (juzi) kujiandaa na mechi zinazofuata,” aliongeza Wenger.

Arsenal hawajawahi kushindwa kutinga nne bora tangu Wenger alipowasili kwenye klabu hiyo na hivyo endapo itatokea itakuwa ni mara ya kwanza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*