Waziri Mkuu: Kuanzia leo hakuna kiingilio kwa Watanzania

Lulu Ringo, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kwamba kuanzia leo Watanzania wataingia kushuhudia mashindano ya AFCON U-17 bila kulipia gharama yeyote.

Kauli hiyo imetolewa jana, Aprili 14, 2019 wakati alipofungua michuano hiyo iliyoanza kuchezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ambapo katika mchezo wa ufunguzi, Tanzania (Serengeti Boys) walifungwa bao 5-4 dhidi ya Nigeria na mchezo wa pili Angola walishinda bao 1-0 dhidi ya Uganda.

Waziri Mkuu alipotangaza uamuzi huo wa Serikali alikuwa na ameambatana na Rais wa Shirikisho la Soka na barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad.

Mabao ya Nigeria yalipatikana dakika ya 20, 29, 36, 71 na 78 na mabao ya Tanzania yalipatikana dakika ya 21, 51, 56 na 60 ambapo magoli mawili kati ya hayo, yalipatikana kwa penati.

Bao la kwanza la Tanzania lililofungwa na Alphonce Mabula Msanga lilitinga kimiani dakika ya 21. Bao la pili, lilipatikana dakika ya sita ya kipindi cha pili na lilifungwa na Kelvin Pius John.

Dakika tano baadaye, Morice Michael Abraham aliipatia Tanzania bao la tatu lililofungwa kwa njia ya penati. Kabla vijana wa Nigeria hawajakaa sawa, dakika nne nyingine, Edmund Godfrey John alitinga kimiani bao la nne, ambalo pia lililifungwa kwa penati.

Timu ya Tanzania iko kundi A na imepangwa na timu za Nigeria, Uganda na Angola. Michuano hii inatarajiwa kumalizika Aprili 28.

Endapo timu ya Taifa ya vijana ya Serengeti Boys itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili iliyosalia, itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia kwa vijana wa umri wa miaka 17 yatakayofanyika mwakani huko Brazil.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*