WASANII WETU WAJIFUNZE KWA WENZAO WA UGANDA

JUMAMOSI wiki iliyopita msanii wa muziki kutoka katika kundi maarufu la Goodlyfe, Moses Ssekibogo ‘Mowzey Radio’, alizikwa kijijini kwao Kagga, Nakawuka kilomita 25 kutoka jijini Kampala.

Mowzey alifariki dunia Alhamisi iliyopita baada ya kukaa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa muda wa siku 11 toka alipofanyiwa shambulio na baunsa katika Klabu ya De Bar iliyopo Entebbe.

Katika msiba huo uliohudhuriwa na viongozi wa Serikali, wasanii, ndugu, jamaa na mashabiki, ulivuta hisia za wengi na kuonyesha kuwa Mowzey alikuwa mtu wa watu, asiye na makuu.

Jambo muhimu ambalo ni zuri tukajifunza kutoka kwao ni namna wasanii wa Uganda walivyoonyesha ushirikiano kiasi cha kuubeba ule msiba kama ni wao kabisa.

Ushirikiano ni jambo muhimu mno katika sekta ya sanaa kwa kuwa hakuna mtu mwingine nje ya tasnia anayeweza kutengeneza ushirikiano kama si wasanii na mashabiki wenyewe.

Kwa hapa Tanzania, mara kadhaa suala la ushirikiano limekuwa likipigiwa kelele lakini limeonekana kuwa gumu kufanyika au kutekelezeka hasa mmoja ya wasanii anapopata tatizo.

Ukiacha tukio lile la kutekwa kwa mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzake ambalo jamii yote ilishirikiana mpaka wakapatikana, rejea tukio la mwigizaji, Wastara, kuuguza mguu wake.

Mpaka juzi anasafiri kwenda nchini India, ni wasanii wasiozidi watatu ndio walijitokeza katika uwanja wa ndege, Dar es Salaam kumsindikiza msanii huyo alipokuwa akielekea India kupata matibabu.

Ni tukio dogo lakini linatoa ishara mbaya ya mgawanyiko wa wasanii wetu katika sekta ya burudani hasa upande wa filamu. Ni vyema tukarekebisha hili kama kweli tunahitaji kusonga mbele.

BINGWA limevutiwa na umoja ulioonyeshwa na wasanii wa Uganda katika msiba wa mwanamuziki mwenzao, Mowzey Radio. Ni ushirikiano wenye tija tena wenye nguvu unaoweza kupaza sauti na ikasikika.

 

Tunamaliza kwa kusema kwamba, wasanii wetu wajifunze kwa wenzao wa Uganda kutokana na ushirikiano wao walioonyesha kwa kipindi chote cha msiba wa msanii huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*