googleAds

Wapinzani wa Malindi, Al- Masry kutua Zenji leo

NA IBRAHIM MAKAME, ZANZIBAR

WAPINZANI wa timu ya Malindi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Al- Masry ya Misri, leo  wanatarajiwa kuwasili visiwani hapa, tayari kwa mchezo wa  raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Amaan.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Kimataifa wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF),  Ali Bakar Cheupe, kikosi cha Al-Masry kitakuwa na msafara wa watu 28, akiwamo wachezaji, benchi la ufundi la viongozi wa klabu hiyo.

Akizugumza na BINGWA jana visiwani hapa, Cheupe alisema timu hiyo itapokelewa na wenyeji wao, Malindi na pamoja na viongozi wa ZFF. 

Cheupe alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kwa asilimia kubwa  huku akiomba Wazinzibari kujitokeza kwa wingi uwanjani Jumapili kuiunga mkono Malindi ili iweze kupata ushindi katika mchezo huo.

Alisema mchezo huo ni muhimu kwa Malindi kupata ushindi ili kujiweka katika mazingira bora ya kusonga mbele timu hizo zitakaporudiana nchini Misri wiki moja badae.

Malindi ilifanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kuitupa nje ya mashindano hayo timu ya Mogadishu City ya Somalia kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa marudiano uliochezwa Agosti 25,  mwaka huu,  kwenye Uwanja wa Amaan.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja huo, timu hizo zilitoka suluhu ndani ya dakika 90. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*