WAPI PANAMFAA LEMAR?

LONDON, England


Thomas Lemar

SABABU kubwa ya klabu ya AS Monaco kuilipa klabu ya SM Caen kiasi cha euro milioni nne ili wampate winga Thomas Lemar, mwaka 2015, ilikuwa ni mpango wao wa kumwendeleza halafu baadaye wamuuze kwa faida.

Monaco ni ngazi ya wachezaji kadhaa Ufaransa wanaong’ara hivi karibuni, kuanzia Anthony Martial, Geoffrey Kondogbia, Benjamin Mendy na wengine wengi.

Walifikiria mbali sana. Walijua ipo siku timu mbalimbali Ulaya zitakuwa na nguvu ya kifedha katika soko la usajili na kuchukua mchezaji yeyote watakayemtaka.

Leo hii, Monaco inasubiria kiasi cha pauni milioni 166 kama ada ya uhamisho wa straika wao, Kylian Mbappe aliyetua katika klabu ambayo iliwahi kupigania isishuke daraja ya PSG.

Dirisha la usajili barani Ulaya kwa sasa limekuwa ni kichaa. Kutoka kununua mchezaji kwa pauni milioni 25-30, leo hii Arsenal na Liverpool zinatakiwa kulipa si chini ya pauni milioni 102 kumpata Lemar.

Kwa kweli hauwezi kuwalaumu. Kama Coutinho ana thamani ya euro milioni 142, basi Lemar anastahili kuuzwa nusu ya bei ya Mbrazili huyo, angalau zaidi yake.
Hivi sasa  Ligue 1 ina mchezaji mmoja ambaye anauwasha moto katika klabu ya Bordeaux, anaitwa Malcolm, thamani yake ni euro milioni 40, hivyo basi kwa alichokifanya Lemar hadi sasa kinatakiwa kuangaliwa na kufikiriwa upya kwenye kupanga thamani yake.

Monaco huenda ikashindwa kuhimili presha kutoka kwenye timu zinazomtaka Lemar ikiwemo Liverpool na hata kocha wake, Leonardo Jardim analitambua hilo.

 

Lemar ataleta kitu gani kipya?

Msimu uliopita wachezaji wa Monaco waliomiminiwa sifa zote walikuwa ni Mbappé, Fabinho, Tiemoué Bakayoko na Radamel Falcao, lakini Lemar naye alifanya mengi makubwa kutokana na uhodari wake na kubarikiwa ufundi mwingi katika mguu wake wa kushoto.

Ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga katika maeneo magumu. Ni aina ya mchezaji ambaye ukimwachia uwazi mkubwa kwenye eneo la adui basi guu lake la dhahabu lazima lisababishe majanga.

Lemar anaweza kumimina krosi zenye macho, zile zinazotua kichwani kwa straika bila shuruti, au katika mfumo wako ukimpa uhuru wa kutosha basi atakufungia mabao makali ya kideo.

Msimu uliopita alikuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kwamba upande ambao alikuwa akicheza wa kushoto, kulikuwa na beki msumbufu, Mendy ambaye alipenda mno kupandisha mashambulizi na kuwavuruga mabeki wa timu pinzani.

Mvurugo huo sasa ndiyo ulikuwa faida kwa Lemar, ambaye alikuwa akitokea kushoto na kuingia ndani kucheza kama namba 10 na alitumia faida ya mabeki kuacha uwazi mkubwa wakijaribu kumkaba Mendy na kusahau kuwa kuna Fisi wanayemuachia bucha.

Winga huyo alimaliza msimu kwa mabao tisa na asisti 10 huku akiisaidia Monaco kutinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufunga mabao sita.

Lemar ni zaidi ya kuwa mshambuliaji hata kwenye kukaba naye yumo, atapambana kurudisha mpira kwenye himaya yake na kuusoma vyema mchezo ili aweze kuingilia pasi za wapinzani na kusaidia shambulizi la kushtukiza.

Kuna ambao pengine watajiuliza, kama ni winga kwanini anaingia sana katikati. Kiufupi Lemar hajabarikiwa sana kasi na si winga halisi kama walivyo Bernardo Silva, Malcom au hata Sadio Mane na Mohamed Salah.

Hawezi kumpita mpinzani kwa kukimbia kimbia tu, mara nyingi hutegemea chenga ya mwili au kusubiri mwenzake apite pembeni kumhadaa beki ndipo yeye aufinyie mpira kwa ndani.

Mfumo ambao unamfaa Lemar ni 4-2-3-1, hapo atapata nafasi ya kutosha ya kutokea na mpira pembeni na hata mfumo wa Arsene Wenger pale Arsenal wa 3-4-2-1 utamfaa akichezeshwa nafasi ya Alexis Sánchez.

Unyumbulifu wake kwenye mifumo mbalimbali pia utaongeza nguvu maradufu katika safu ya kiungo ya Liverpool, akichezeshwa kwenye eneo la Coutinho, kutokea kushoto na kutengeneza nafasi za kutosha sambamba na kupiga mashuti.

 

Timu gani itafanikiwa kumnasa?

Kwa muda mrefu sasa Klopp ametajwa kuvutiwa na Lemar, lakini baada ya Coutinho kuondoka na kukivuruga kichwa chake, Mjerumani huyo ameingia sokoni kuisaka saini yake.

Wenger, anajulikana kuwa ni mkali wa kusaka vipaji Ufaransa lakini hilo haliwezi kutujibia swali la ilikuwaje akawasajili Yaya Sanogo au Francis Coquelin.

Huenda Lemar akawa ni mchezaji aliyemuona miaka saba nyuma, lakini ikumbukwe wazi kuwa Mfaransa huyo alishataka kujiunga na Liverpool majira yaliyopita ya kiangazi lakini katika kipindi timu hizo ziko meza ya mazungumzo, Lemar alikuwa timu ya taifa akifanya yake hivyo dili likawa gumu kukamilika.

Monaco pia walikuwa na jeuri ya kumbakisha na hata sasa wanaweza kuwa nayo kutokana na kwamba watakuwa na fedha za uhamisho wa Mbappe ambazo zitasaidia kuboresha kikosi chao.

Lakini, nyota huyo anaonesha kutaka kuondoka hivi karibuni na mapema.

Monaco tayari ilishindwa kuvuka hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa msimu huu kwa kumaliza kama vibonde wa kundi lao huku kwenye Ligue 1 mambo yakiwa magumu kutokana na ubabe wa PSG, licha ya wao kuwa nafasi ya pili.

Ukweli ni kwamba, Lemar hana furaha msimu huu. Licha ya kutokuwa na uhakika wa kunasa kombe lolote msimu huu, majeraha ya nyama za poja nayo yamechangia kuipoteza furaha yake. Alikosekana kwa takribani mechi tano lakini aliporudi mwanzoni mwa Desemba mwaka jana, alionesha kuwa bado ana uwezo kwa kutoa asisti na kufunga bao ndani ya mwezi na nusu.

Bila shaka, Lemar atafanya kila jitihada za kuondoka Monaco mwezi huu ili kupata changamoto mpya.

 

Nini kitatokea baadaye?

Ni hatari kwa Lemar kwani huenda akajikuta kwenye timu ambayo haina uhakika wa kumaliza ndani ya ‘top four’.

Liverpool inaonekana kama ni timu itakayomaliza nafasi za juu na kitendo cha kumsajili Lemar ili angalau kuziba pengo la Coutinho nalo huenda likawasaidia kwenye harakati zao hizo.

Kwa upande wa Arsenal, inaonekana mzani haujakaa sawa ndani ya klabu hiyo kutokana na tetesi za Sanchez na Mesut Ozil, sambamba na Wenger mwenyewe.

Huu ni mwaka wa Kombe la Dunia na France atahitaji sana kujiunga na wenzake katika safari ya kuelekea Urusi, hivyo ni vyema angebaki kwanza Monaco halafu ndiyo aamue kuondoka baada ya mashindano hayo kumalizika.

Akichagua timu isiyo sahihi kwa sasa itagharimu nafasi yake timu ya taifa, kwani itamchukua muda hadi kutulia kiakili.

Lakini kama kocha wake, Jardim alivyokiri kuhusu kuvurugika kwa soko la usajili, iwapo fedha nzuri itakuja mezani kwake kutoka Liverpool basi lolote laweza kutokea.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*