googleAds

WANATISHA Liverpool yamkosha Klopp, ataja siri ya ubingwa Ulaya

LONDON, England

KOCHA wa timu ya Liverpool, Jurgen Klopp, amedai kwamba aina ya soka walilocheza dhidi ya Southampton si la kisasa, lakini ni mbinu ya upambanaji ambayo imewafanya kutambulika kama mabingwa wa Ulaya.

Liverpool iliichapa Southampton mabao 2-1 katika mchezo huo wa Ligi Kuu England uliochezwa wikiendi iliyopita, lakini safu yao ya ulinzi ilionyesha udhaifu mkubwa mbele ya mlinda mlango, Adrian, ambaye hajaweza kucheza kwa kiwango cha kuridhisha.

Adrian ameanza kuitumikia Liverpool ndani ya siku chache bila kuwa fiti kikamilifu, hali iliyomfanya kutokuwa na kiwango bora dhidi ya Southampton na wakati huo huo, James Milner, pia alicheza dakika nyingi akiwa na ‘bandeji’ kichwani.

Mechi hiyo ilitawaliwa na ‘undava’ wa hali ya juu kama ilivyowahi kuwa katika soka la kizamani, lakini Liverpool iliweza kusimama imara na kumaliza kwa kuendeleza rekodi ya kushinda mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Klopp alisema alifurahishwa mno na namna wachezaji wake walivyojituma na kufanikiwa kuondoka na ushindi huo ugenini.

Lakini kocha huyo alikiri kwamba kikosi chake hicho hakijaweza kufikia kasi ya msimu uliopita.

“Tunapenda kucheza hivi kusema ukweli, soka la kizamani,” alisema Mjerumani huyo.

“Ujue zamani soka halikuwa bora sana, lakini kuna baadhi ya vitu vilikuwa ni vizuri mno na ndio maana tunaviona hadi sasa.

“Vijana wameonyesha upambanaji ambao nimevutiwa nao, Adrian anaonyesha kuwa tayari kucheza muda wowote anapopata nafasi.

“Milner pia alinivutia. Anacheza soka la kizamani ninalolipenda, soka la kuwa na njaa ya kushinda mchezo. Hatushangazwi na matokeo haya, lakini kushinda kila mara ni kitu ambacho hatujakizoea.

“Namna tunavyocheza ni sawa na kusema ligi inaisha leo. Hiyo ndio mbinu iliyotufikisha katika fainali tulizocheza na tutaendelea kufanya hivyo,” alisema Klopp.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*