WANAMICHEZO WANAVUNA WALICHOKIPANDA JUMUIYA YA MADOLA

WANAMICHEZO wa Tanzania wameendelea kufanya vibaya katika michezo ya Jumuiya ya Madola inayoendelea nchini Australia.

Tayari mabondia wanne ambao ni Selemani Kidunda, Haruna Swanga, Hezra Paul  na Kassim Ngutwike wameiaga michezo hiyo.

Mabondia walipigwa mwanzoni na kushindwa kufuzu hatua iliyofuata.

Kutokana na kutolewa kwa mabondia hao, matumaini ya wanamichezo wetu kurejea na medali ni madogo.

Pamoja na  mabondia kufanya vibaya, muogeleaji Hilal Hilal naye alitolewa jana, baada ya kushindwa kuingia katika hatua ya nusu fainali.

Matumaini ya Watanzania kupata medali yanazidi kupotea baada ya mwogeleaji Hilal kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali aliyeshindana katika mtindo wa ‘freestyle’.

Baada ya wanamichezo hao kutolewa, matumaini ya Tanzania  kupata medali katika michezo ya Jumuiya ya Madola ni madogo.

Kwa sasa matarajio ya  wanamichezo wetu kurejea na medali yamebaki kwa wanariadha na meza, ingawa si makubwa.

BINGWA tunasema kwamba, Tanzania tunavuna tulichokipanda kwa kuwa dalili za kufanya vibaya zilionekana kabla ya wanamichezo wetu  kuondoka nchini.

Wanamichezo wetu kama wa riadha, walishindwa kufanya maandalizi bora kutokana na kukosa fedha za kuweka kambi ya muda mrefu kama ambavyo nchi za wenzetu wanavyofanya maandalizi yao.

Tunakumbuka kambi ya riadha ilichelewa kuanza kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya kambi, hivyo hatushangai  kinachoendelea Australia.

Dalili za wanamichezo wetu kurejea nchini mkono mitupu zimeanza kuonekana kwa michezo hiyo miwili.

Lakini wanariadha ambao tulikuwa na mategemeo ya kufanya vizuri katika michezo ya Madola, waliondolewa na kuonekana pengo kwa timu hiyo.

Kwa ujumla maandalizi ya timu zote hayakuwa mazuri, kwani mabondia waliokuwa wanaandaliwa kwenda kushiriki michezo ya Madola walikuwa na maandalizi duni.

Tulishuhudia mabondia hao wakifanya mazoezi katika mazingira magumu, huku wakikosa vifaa vya kisasa vya mazoezi.

Mara nyingi timu  zetu zinapofanya vibaya sababu zinakuwa ni zilezile za kwamba maandalizi ni duni.

BINGWA tunahoji; aibu hii ya Tanzania kuendelea kuwa wasindikizaji katika mashindano ya kimataifa itaisha lini?


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*