googleAds

Wameng’ara lakini ubingwa wa ligi wanausikia bombani

LONDON, England

RAHA ya soka ni pale unaposhinda mechi na kutwaa ubingwa, lakini jambo hilo mara nyingi huwa si kazi rahisi kutokana na kwamba, mwisho wa siku ni timu moja tu ambayo inaweza kutwaa ubingwa wa mashindano yoyote na ya ligi.

Kutokana na jambo hilo kuna baadhi ya wachezaji nyota katika historia ya soka ambao wameshawahi kutwaa mataji makubwa wakiwa na timu za taifa kama vile Kombe la Dunia na wa fainali za Mataifa Ulaya, lakini hawajawahi kulitia mkononi kombe la michuano ya ligi kipindi chote cha kibarua chao.

Katika makala haya wafuatao ni wachezaji 10 ambao hawajawahi kutwaa ubingwa wa ligi kipindi chote walichocheza soka.

 1. Steven Gerrard

Wakati linapokuja suala la wachezaji wakongwe Liverpool, hakuna ambaye anaweza kumweka kando staa wao wa zamani, Steven Gerrard.

Mkongwe huyo ambaye ni zao la shule ya vijana ya Liverpool na shabiki mkubwa wa Reds, alianza kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ya Anfield msimu wa 1999/2000 akiwa na umri wa miaka 19.

Mkongwe huyo alikuwa nahodha wa  Liverpool kwa zaidi ya muongo mmoja kuanzia mwanzoni mwa msimu wa  2003/04 hadi mwishoni mwa msimu wa  2014/15 na ilishuhudiwa akipata mafanikio makubwa kipindi chote alichoitumikia klabu hiyo.

Kutokana na umahiri wake katika safu ya kiungo na upachikaji mabao, ilishuhudiwa Gerrard akiiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la FA mara mbili wa Kombe la EFL mara tatu na wa Makombe ya UEFA na wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lilikuwa ni bao lake ambalo mwaka 2005 liliiwezesha Reds kutoka nyuma na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na mwaka 2006  akafanya hivyo tena katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la FA,  lililoiwezesha timu hiyo kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya West Ham na kisha Liver wakaibuka mabingwa kwa mikwaju ya penalti.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Gerrard hakuweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England katika kipindi chote alichoitumikia, Liverpool zaidi ya kuifanya imalize ikiwa mshindi wa pili misimu ya 2001/02, 2008/09 na  2013/14.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya England, mwaka 2004 na 2005 alihusishwa kuwa angekwenda kujiunga na Chelsea na angeweza kushinda ubingwa wa ligi akiwa na Blues, lakini badala yake akaamua kubaki Liverpool.

2. Fernando Torres

 Licha ya straika huyo raia wa Hispania, Fernando Torres, kuchezea klabu kubwa na zenye mafanikio kama Atletico Madrid, Liverpool, Chelsea na AC Milan, cha kushangaza ni kwamba hakuwahi kubeba ubingwa wa ligi kwa takribani kipindi cha miongo miwili aliyosakata kandanda.

Ubingwa pekee ambao aliwahi kuutwaa akiwa na Atletico msimu wa 2001/02, lakini ni wa Ligi Draja la Kwanza Hispania, Segunda Division na wala si wa Ligi Kuu ya La Liga.

Akiwa katika michuano ya La Liga, Torres hakuweza kukaribia hata kuunusa ubingwa wa ligi hiyo na badala yake aliiwezesha Atletico kumaliza michuano hiyo ikiwa kwenye nafasi ya saba mara mbili.

 Hata hivyo, baadaye staa huyo aliamua kutimkia England alipojiunga na  Liverpool na akaiwezesha kushika nafasi ya pili msimu wa 2008/09, akiwa ameifungia mabao 14 katika michezo  24. Akiwa Chelsea, Torres alitoa mchango mkubwa ulioisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012, lakini akajikuta wakimaliza nafasi ya tatu kwenye michuano ya Ligi Kuu.

Cha kusikitisha ni kwamba, Torres angeweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England akiwa na klabu hiyo ya  Stamford Bridge kama angeendelea kubaki msimu mmoja, lakini akawa ameshapelekwa kwa mkopo AC Milan na kisha akarejea Atletico kwa ajili ya msimu wa 2014/15 na hivyo kuiacha Chelsea ikinyakua taji lake la nne katika michuano.

3. Marco Reus

Pengine hali ya staa huyo inaweza kubadilika msimu huu, kutokana na kuwa timu yake ya Borussia Dortmund, mpaka mapema jana ilikuwa ikiongoza kwenye msimamo wa Ligi ya   Bundesliga ikiwa mbele kwa tofauti ya pointi mbili na huku zikiwa zimebaki mechi nne kabla michuano hiyo haijamalizika.

Hata hivyo, mpaka sasa straika Marco Reus, bado anaendelea kuwa miongoni mwa mastaa ambao hawajawahi kutwaa ubingwa wa ligi.

 Pia licha ya kusadikika kuwa asiye na bahati na mataji hayo, tatizo la majeraha lilimfanya ashindwe kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2014 akiwa na kikosi cha Ujerumani.

Jambo la kuvutia kwa Reus ambaye aliwahi kuchezea timu ya vijana ya  Borussia Dortmund kabla ya kujiunga nayo tena Januari 2012 akitokea  Borussia Monchengladbach, lakini aliumalizia msimu wa  2011/12 akiwa na  Monchengladbach, jambo ambalo lilimfanya aukose ubingwa mara mbili mfululizo ambao Dortmund iliupata katika michuano hiyo ya Bundesliga.

4. Harry Kane

 Kama ilivyo kwa Marco Reus, Harry Kane pia hajawahi kutwaa ubingwa wowote wa ligi akiwa na Tottenham katika kipindi chote cha kibarua chake.

 Staa huyo kwa sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote Tottenham katika ligi hiyo ya England na ameshafikisha mabao  100 katika ligi hiyo.

Mastaa wengine ambao wanausikia kwenye bomba ubingwa huo wa ligi ni Gary Lineker, Gordon Banks, Jamie Carraghe, Daniele De Rossi, Klaas-Jan Huntelaar na Juan Mata.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*