Wambura anapoamua kutafuta haki yake mahakamani

NA ONESMO KAPINGA

HIVI karibuni, Michael Wambura, alikimbilia mahakamani baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumfungia maisha kujihusisha na masuala ya soka.

Wakati huo, Wambura alikuwa Makamu Rais wa TFF, lakini alipoteza nafasi hiyo kutokana na makosa matatu likiwamo la kupokea fedha za TFF kinyume cha sheria, kughushi nyaraka na kushusha hadhi ya shirikisho hilo.

Kwa wale ambao huenda wamesahau, Kamati ya Maadili ya TFF iliundwa baada ya ushauri wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), uliotokana na Wambura kuwasilisha malalamiko kwa shirikisho hilo.

Wambura aliwasilisha malalamiko Fifa baada ya kuenguliwa katika uchaguzi mkuu wa TFF uliofanyika mwaka 2013, kwa madai ya tuhuma mbalimbali yakiwamo ya kwenda mahakama ya kawaida ya sheria kudai haki.

Fifa ilisikiliza malalamiko ya Wambura na kuamua kutuma ujumbe nchini, lengo likiwa kutatua mgogoro uliokuwepo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliomwingiza madarakani Rais Jamal Malinzi.

Fifa ilibaini Wambura na wenzake waliondolewa katika uchaguzi wa 2013 bila kutendewa haki lakini kikubwa ni mapungufu yaliyoonekana katika katiba ya TFF.

Walichoelekeza Fifa kwa kamati ya utendaji ya TFF ni kufanya marekebisho katika katiba ya TFF na kuunda vyombo viwili vya kutoa uamuzi wa kisheria.

Kwa kipindi hicho, Fifa ilishauri licha ya katiba ya TFF kuwa na vyombo vya kutenda haki, lakini vilikuwa havina mamlaka zaidi ya sheria na kuamua iundwe kamati ya maadili na ile ya rufaa ya maadili ambazo zitakuwa zikitoa haki ndani ya shirikisho hilo.

Kamati hizo ziliundwa baadaye kabla ya kwenda kwenye uchaguzi wa mwaka 2013, lengo la Fifa likiwa ni kwamba masuala ya soka yashughulikiwe kwa kufuata taratibu zao na si kwenda katika mahakama ya kawaida kudai haki.

Naamini Wambura analifahamu hili kuliko mtu yeyote, lakini nashangaa kitendo chake cha kurudi tena mahakamani wakati Fifa ilitengeneza njia ya kutafuta haki katika masuala ya soka.

Lakini kwanini awe ni Wambura tu anayepingana na uamuzi ya kamati huru ya maadili? Kwani hakuna wengine waliofungiwa na kamati hiyo?

Kwanini mara zote Wambura anapingana na taratibu za mpira wa miguu na pale anapoona amenyimwa haki na kukimbilia mahakamani?

Hii si mara ya kwanza Wambura kwenda mahakama ya kawaida kudai haki. Aliwahi kwenda kuzuia uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba baada ya kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.

Amekuwa ni mtu anayeshinda mahakamani, ikitokea kupewa adhabu na chombo cha soka kinachosimamia haki badala ya kufuata taratibu za soka za kutatua matatizo.

Inawezekana safari hii, Wambura alikwenda mahakama ya kawaida ya sheria kudai haki kutokana na kamati ya maadili ya TFF kushindwa kumtendea haki, lakini alikuwa na nafasi ya kukata rufaa chombo cha juu yake.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*