WAKITOKA WAKATAMBIKE

*Simba kuhamishia mauaji Taifa leo, Mbeya City waingiwa na mchecheto

NA AYOUB HINJO

TIMU ya Simba inashuka dimbani leo kumenyana na Mbeya City katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukiwa mchezo wa 22 kwa wenyeji na 24 kwa wageni hao kutoka jijini Mbeya.

Simba imetoka kushinda michezo miwili ya mwisho waliyocheza ugenini dhidi ya Njombe Mji na Mtibwa Sugar, mchezo wa leo dhidi ya Mbeya City unakuwa wa kwanza Uwanja wa Taifa, tangu wacheze mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Al Masry kutoka Misri.

Kwa upande wao, Mbeya City walitoka sare michezo yao miwili iliyopita dhidi ya Azam, uliomalizika kwa suluhu na mwingine ulifanyika katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, timu hizo zikifungana mabao 2-2.

Wekundu wa Msimbazi wapo kileleni kwa pointi 52 wakifuatiwa kwa ukaribu na Yanga wenye pointi 47, huku Mbeya City wakiwa nafasi ya nane wakijikusanyia pointi 26.

Msimu huu timu ya Simba inajivunia rekodi nzuri ya ufungaji mabao, wakifunga mabao 52 na kufungwa 11. Kwa upande wa Mbeya City, hadi sasa wamefunga mabao 20 na kufungwa 25.

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amesema kikosi chao kipo vizuri baada ya kurudi Morogoro kwenye  mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar.

Aliongeza kuwa wanahitaji ushindi kuweka hai mbio zao za kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

“Tumerudi salama, kila mchezaji yupo vizuri. Mbeya City ni timu nzuri lakini tutapambana kupata pointi tatu ili kujikita zaidi kileleni na mwisho wa msimu tuwe mabingwa,” alisema Djuma.

Pamoja na vinara hao kuwa na matokeo mazuri msimu huu, wamekuwa na rekodi ya kushangaza dhidi ya Mbeya City ambao walipanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14.

Timu hizo zimekutana mara nne katika Uwanja wa Taifa, Simba wakishinda mara moja, sare mbili na Mbeya City wakifanikiwa kupata ushindi mara moja tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*