googleAds

Waingereza bado hawamwamini Harry Kane?

NA AYOUB HINJO

KAMA mchezo wa soka ungekuwa unachezwa midomoni basi England wangekuwa mabingwa katika kila mashindano au michuano iwe ya Ulaya au Dunia, wale watu wanaongea haswa.

Ndugu yangu, Ally Kamwe aliwahi kuniambia kuwa tofauti ya Waingereza na Watanzania ni ‘ndui’ tu, kila kitu walichonacho nasi tunacho, wala sipingani naye.

Ni mafundi wa vinywa sisi, maneno ya nusu kurasa tunaweza kuyaelezea kwa zaidi ya saa 12 na usichoke kutusikiliza.

Tunapenda sifa, tunapenda hadhi, tunapenda mno kuwa juu na bora kuliko wengine.

Mbali ya hivyo, sote tuna tabia moja inayofanana, unafki.

Ndio, Watanzania ni wanafiki wazuri kama ilivyo kwa Waingereza. Sekunde tutamzoea Mbwana Samatta, sekunde tena tutamsifia na kumfananisha hata na Ronaldo de Lima, nani anajali? 

Jeuri ya Waingereza inaanza kujengwa kuanzia kwenye vyombo vyao vya habari, kila kitu kinaanzia hapo na kusambaa duniani kote.

Maneno ya Waingereza mara nyingi yanapingana na uhalisia ambao utakuja kutokea, kwa namna moja au nyingine si watu wa kuwaamini sana pindi ukiwa karibu nao.

Ushajiuliza kwanini mpaka kufikia sasa straika wao hatari, Harry Kane hajatafutiwa jina kama nyota wengine kuwahi kutokea katika nchi hiyo?

Inafikirisha kidogo, ina maana Kane bado hajaaminika ndani ya ardhi ya Malkia Elizabeth? Hayo ni sehemu ya maswali mepesi ambayo yanahitaji majibu magumu yaliyoshiba kweli kweli.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, utahitaji kitu gani ili kujua ubora wa Kane ukitoa mataji ambayo kwa timu anayocheza inaweza kuwa ndoto kuyapata? 

Utahitaji nini ili kukubali kuwa Kane ni moja ya mastraika hatari wa kizazi hiki? Inanishangaza hata Waingereza wenyewe wamekaa kimya juu ya kijana huyo.

Ni wazi nyota ya Jack Wilshere ilipoanza kung’aa ilimfanya kuzungumzwa kila kona ya England na ulimwenguni kutokana na sifa alizopewa wakati ana miaka 16 tu.

Wilshere alikuwa kwenye kilele cha ubora wa kuzungumzwa hasa baada ya mchezo wake dhidi ya Barcelona mwaka 2011, kila alichokifanya kiligeuka kuwa dhahabu.

Waingereza walipagawa na Wilshere, hawakusikia kitu chochote cha kuambiwa zaidi ya kumpamba kwa maneno matamu, lakini leo hii hakuna anayethubutu kumtaja kiungo huyo.

Kuhusu Wilshere sio habari tena sababu alishindwa kuishi kwenye ndoto za Waingereza, maisha yamebadilika kila kinachomuhusu Wilshere hivi sasa ni cha Wilshere mwenyewe.

Nani hakumbuki jinsi Wayne Rooney alivyoitwa ‘The White Pele’? Yaani Pele Mweupe. Wala Waingereza hawakujali na kuitazama dunia itawaangaliaje.

Ndio, Rooney aliishi maisha yake uwanjani, hakika ni moja ya wachezaji bora wa England kuwahi kutokea ikiwa mpaka hivi sasa ameamua kujiunga na Derby County lakini aliweka rekodi mbalimbali.

Rooney ni mfungaji wa muda wote wa Manchester United na England, lakini bado hakuonekana anafaa mbele ya Waingereza walioimba jina lake wakati wa udogo wake sababu si mtu anayevutia kama David Beckham.

Rooney hatazamiki mara mbili, anaishi kwenye dunia yake. Waingereza ni wanafki sana, rekodi za Rooney hazizungumzwi kama habari za Beckham kuonekana kwenye harusi ya mtoto wa Malkia au starehe zake katika ufukwe wa Ibiza.

Kwa miaka ya hivi karibuni ilikuwa kwa Dele Alli ambaye aliitwa ‘The English Iniesta’, maana yake ni Iniesta wa Uingereza. Inachekesha.

Dele hafiki hata robo ya Andres Iniesta yule aliyekuwa na umri wa miaka 34 wakati anamaliza muda wake Barcelona, aliyetimkia Japan kucheza soka lake la mwisho, inasikitisha sana juu ya hilo.

Kwa taarifa tu, angalia jinsi wanavyolikuza jina la Jadon Sancho yule kinda wa miaka 18 anayekipiga Borrusia Dortmund.

Sancho anatajwa kila siku na kusifiwa juu ya uwezo wake, nyimbo zao kutoka kwa akina Wilshere zinaelekea kwa chipukizi huyo anayeing’arisha Dortmund, tusubiri tuone. 

Pamoja na kumwaga sifa zote kwa wachezaji wao bado sijaona mahali wakijaribu kumtazama Kane kwa mbali zaidi ya hapa.

Unajua kwanini? Iko hivi, maisha ya Kane ya soka yalianza kwa misukosuko mingi ikiwa alishawahi kukataliwa akademi ya Arsenal sababu ya mwili wake kuwa kibonge.

Hakuna aliyekiona kipaji cha Kane wakati ule, wala hakujulikana kwa urahisi zaidi ya kuachwa na kudharauliwa kwenye udogo wake.

Hata alipoanza kufunga hawakumtazama kwa jicho la tatu zaidi ya kukosoa kile alichokifanya kwa kutoa adhabu kali kwa makipa, nani alijali? Hakuna.

Kane wala haitwi Ronaldo de Lima licha ya umahiri wake wa kupachika mabao, kuna kitu bado Waingereza hawajakikubali au kumuamini? Labda mimi sijui.

Lakini ni Waingereza pekee watayoisema kwa wingi sababu hiyo hapo baadae na watasema hivyo kwa sababu, upo ukweli unaowatafuna kwenye vifua vyao na hawako tayari kuuamini.

Tena kwa tazama jinsi hata habari za Kane kupewa unahodha wa timu ya Taifa ya England zilivyoonekana za kawaida wakati wanaenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka jana nchini Urusi.

Hakuna aliyemjali, kila mtu alimchukulia kawaida sana, kama si juhudi zake binafsi, huenda leo hii Kane asingekuwa mwanadamu huyu tunayemfahamu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*