googleAds

Wachezaji Yanga kuoga noti

NA MOHAMED KASSARA

KATIKA kuhakikisha wanamaliza kazi mapema nyumbani, uongozi wa Yanga umeahidi kuwajaza mamilioni wachezaji wao iwapo wataifunga Zesco United ya Zambia katika mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza, utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana Septemba 25, mwaka huu, nchini Zambia.

Timu itakayopita raundi hiyo, itatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, wakati ile itakayotolewa itaangukia Kombe la Shirikisho Afrika, ikianza na mechi ya mtoano.

Kwa kufahamu umuhimu wa mchezo huo, uongozi wa Yanga umetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwapindisha morali wachezaji wao wapambane na kupata ushindi mnono nyumbani utakaowarahisishia kazi watakapokwenda ugenini.

Ili kufanikisha mkakati huo, Kamati ya Mashindano imekutana na kukubaliana kutenga dau nono kama zawadi kwa wachezaji wao ili kuwapa motisha kama walivyofanikiwa katika mchezo uliopita dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Akizungumza na BINGWA jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema fedha hizo zimetengwa kwa kazi moja tu yakuwapandisha munkari wachezaji wao waifyekelee mbali Zesco.

“Kuna mamilioni ya fedha yametengwa kama motisha kwa wachezaji wetu, hii si mara ya kwanza, ni utaratibu wetu kama uongozi ili kuwapandisha hasira wachezaji wetu.

“Tulifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Rollers na kufanikiwa kupata ushindi ugenini, safari hii tumeamua kuanzia nyumbani kutokana na umuhimu wa mchezo wenyewe. Lengo kuu la kutoa motisha hiyo ni kuhakikisha wachezaji wetu wanapambana kupata ushindi mkubwa hapa ili iwe rahisi tutakapokwenda kwao,” alisema.

Mwakalebela alisema tayari wachezaji hao wameshalipwa fedha walizoahidiwa baada ya kuitoa Rollers, huku akisisitiza kuwaogesha mamilioni mengine wakifanikiwa kuifunga na hatimaye kuitoa Zesco katika michuano hiyo.

Alisema wameshazungumza na wachezaji wao juu ya umuhimu wa ushindi leo, akisema wameahidi kupambana kufa au kupona kupata ushindi mnono dhidi ya Wazambia hao.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Hamasa imewataka mashabiki wa Yanga kuujaza Uwanja wa Taifa na kuwashangilia mastaa wao watakapokuwa dimbani kupepetena na Wazammbia hao wanaonolewa na kocha wao wa zamani, George Lwandamina.

Mjumbe wa kamati hiyo, Hassan Bumbuli, alisema mashabiki, wapenzi na wanachama wa timu hiyo wachangamkie mapema tiketi zilizoanza kuuzwa kuanzia juzi kwenye vituo mbalimbali ili kuutapisha uwanja huo na kukata ngebe za watani wao wa jadi, Simba, hasa Msemaji wao, Haji Marana.

Manara amekuwa akiwabeza Yanga kwa kushindwa kuujaza Uwanja wa Taifa hata pale timu yao inapokabiliwa na mchezo muhimu tofauti na ilivyo kwa mashabiki wao ambao ‘kulitapisha’ dimba hilo ni kawaida yao.

Bumbuli alisema kamati yao inaendelea kuwahamasisha mashabiki wao kujitokeza kwa wingi uwanjani leo ili kuzima majigambo ya Manara na mashabiki wengine wa Simba na hata viongozi wao.

“Kamati ya Hamasa imejipanga vilivyo kuhakikisha Wanayanga wanajitokeza kwa wingi uwanjani, tayari tiketi zimeanza kuuzwa kwenye vituo mbalimbali nchini, nawaomba mashabiki tujitokeze kwa wingi na kuutapisha uwanja ili kuwaonyesha wale wanaotubeza kuwa tuna nguvu kiasi gani.

“Ninavyowafahamu Yanga inaweza kujaza hata viwanja viwili, hilo sina shaka nalo kabisa kwa kuwa Yanga ina mashabiki wengi, kikubwa kila mmoja aje na jezi yake uwanjani kuipa sapoti timu yetu ifanye vizuri kwenye mchezo huo,” alisema Bumbuli.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*