WACHEZAJI HAWA WALIPOTEZA MATUMAINI LAKINI MSIMU HUU WAPO VIZURI EPL

LONDON, England


 

KWA mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kwa timu tatu mpaka kufikia mzunguko wa 10 hazijapoteza mchezo wowote mpaka sasa.

Manchester City na Liverpool wanatenganishwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa katika msimamo huku Chelsea wakisalia nafasi ya tatu licha ya kutopoteza mchezo mpaka sasa.

Kama ilivyo kila msimu, timu kubwa huwa na wachezaji ambao viwango vyao huwa vya kusuasua lakini kuna kipindi hao nyota hurudi kwenye viwango vya juu na kushangaza wengine.

Kama ilivyotarajiwa, wachezaji kama Eden Hazard, Mohamed Salah, Sergio Aguero na Pierre-Emerick Aubameyang, wapo kwenye ubora mkubwa, ingawa kuna nyota wengine ambao hawakutegemewa kufanya vizuri tangu kuanza kwa msimu wameonekana kuwa moto wa kuotea mbali.

Makala haya yanakuletea wachezaji watatu ambao tangu kuanza kwa msimu huu wamekuwa kwenye viwango vya juu na kuwashangaza wafuatiliaji wa Ligi Kuu England ‘EPL’.

LUKE SHAW (MANCHESTER UNITED)

Luke Shaw alisajiliwa na Manchester United miaka kadhaa iliyopita na alitarajiwa kuziba nafasi ya mkongwe, Patrice Evra, aliyeondoka kikosini hapo.

Hata hivyo, hawakuwa na maendeleo mazuri sababu ya kupata majeraha ya mara kwa mara yaliyochangia kiwango chake kushuka kwa kasi tofauti na ilivyotarajiwa.

Kabla ya msimu huu kuanza iliaminika Shaw angeendelea kuwa mchezaji wa akiba akisubiri nafasi kwa Ashley Young au Matteo Darmian ambaye alitajwa kuondoka katika dirisha la usajili lililopita.

Misimu miwili iliyopita, Shaw alikuwa katika wakati mgumu baada ya kocha wa timu hiyo, Jose Mourinho, kumponda kwenye vyombo vya habari.

Lakini tangu kuanza kwa msimu huu, Shaw amefanikiwa kuiteka akili ya Mourinho kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha mpaka hivi sasa.

Akiwa moja ya wachezaji tegemeo huku akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa klabu hiyo mara mbili mfululizo, yaani Agosti na Septemba.

ROSS BARKLEY (CHELSEA)

Ross Barkley ni moja ya wachezaji waliotabiriwa kuwa na uwezo mkubwa wakati anachipukia kutoka kwenye akademi ya Everton.

Alianza kwa kasi kubwa katika kikosi cha kwanza cha Everton na kuwa mchezaji tegemeo wa timu hiyo kutoka Merseyside, lakini majeraha ya mara kwa mara yalimfanya kupoteza nafasi ndani ya klabu hiyo.

Licha ya kuwa majeruhi, Chelsea chini ya Antonio Conte, walimsajili hivyo katika dirisha dogo la Januari mwaka jana, wakiamini atarudi kwenye kiwango chake.

Lakini msimu huu chini ya Maurizio Sarri, kiungo huyo anaonekana kuwa mhimili wa kikosi hicho katika kutengeneza nafasi za mabao na kuchezesha.

Tetesi ambazo zilitoka awali zilidai kuwa kiungo huyo raia wa England asingefanikiwa kurejea uwanjani hivi karibuni, Chelsea ilikuwa tayari kuvunja mkataba wake.

JOE GOMEZ (LIVERPOOL)

Kuwasili kwa Virgil Van Dijk kutoka Southampton katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka jana, kuliifanya beki ya Liverpool ionekane imara tofauti na ilivyokuwa awali.

Van Dijk alitengeneza kombinesheni na Dejan Lovren ambaye mara kwa mara anatajwa kufanya makosa katika mechi kubwa na kuifanya timu hiyo kupoteza mchezo.

Lakini tangu kuanza kwa msimu huu, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amemrudisha kikosini beki wake, Joe Gomez, ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu kwa majeraha.

Gomez ametengeneza kombinesheni bora na Van Dijk na kuifanya ngome ya Liverpool kutopitika kwa urahisi kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Kiwango chake anachokionyesha beki huyo raia wa England hivi sasa kimekuwa gumzo katika Ligi Kuu huku akitabiriwa kufanya makubwa zaidi kama majeraha yatampita mbali.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*