googleAds

WAAMUZI WASIPINDISHE SHERIA 17 ZA SOKA

MWAMUZI Hussein Athumani kutoka mkoani Katavi, ameondolewa katika orodha ya waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa maelekezo kwamba alishindwa kasi ya mchezo kati ya Majimaji na Yanga.

Mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0 uliochezwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea na Athumani kuonekana kushindwa kabisa kwenda na kasi ya mchezo.

Mwamuzi huyo anadaiwa kuchezesha mchezo huo chini ya kiwango, ambapo Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tazania (TFF), imefikia kumwondoa baada ya kubaini mapungufu yake.

Lakini kubwa tunaloliona hapa ni mwamuzi huyo kushindwa kutafsiri vema sheria 17 zinazotawala katika  mchezo wa soka, kwani waamuzi wengi wamekuwa wakionyesha upungufu mkubwa hasa katika mechi zinazohusisha timu zenye upinzani mkubwa.

Tunaamini kwamba baadhi ya waamuzi wana uwezo mkubwa wa kuchezesha michezo, lakini tunachokiona ni ukiritimba wa viongozi wa shirikisho hilo wa kuwapitisha waamuzi ambao hawakufaulu vizuri mtihani wa kukimbia ‘Coopertest’.

Pengine kama shirikisho hilo lingekuwa makini katika kuwapitisha waamuzi kuchezesha ligi hiyo, tunadhani kwamba upungufu unaoendelea kwa baadhi yao tusingeuona wakati huu.

Tunasema kitendo cha shirikisho kujuana na waamuzi ni moja ya changamoto ambayo tunaona kwa sasa ligi kuu, kwani malalamiko kwa waamuzi ni mengi kuliko matarajio.

Tukitarajia kupungua kwa malalamiko ya waamuzi baada ya kuwafungia wengine kutokana na kuonyesha udhaifu mkubwa katika uamuzi, lakini ilikuwa tofauti kwani matukio kama haya ya waamuzi ya kutokwenda na kasi ya mchezo yanazidi kuongezeka.

Sisi BINGWA tunaona kwamba bado kuna tatizo kwa waamuzi wetu na ili kuondokana nalo, kuna kila sababu za makusudi za kuangalia kwanza uwezo wa waamuzi wanaopewa nafasi ya kuchezesha ligi hiyo.

Kwa upande wetu tunaamini kwamba ligi kuu haiwezi kuwa bora kama tutakuwa na waamuzi ambao hawawezi kutafsiri kwa ufasaha sheria 17 za soka.

Tunamaliza kwa kusisitiza kwamba kutofahamu vema sheria hizo kusiwe sababu ya kuzipindisha kwa lengo la kuibeba timu moja inayohitaji kutwaa ubingwa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*