VIGOGO WENGINE KUONGEZWA KESI YA MALINZI

NA KULWA MZEE

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake unatarajia kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na kuongeza washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo.

Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri.

Mbali na Malinzi, washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa na Mhasibu Nsiande Mwanga, ambao wanasota mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.

“Kesi ililetwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, napenda kuitaarifu mahakama kwamba nimepangiwa kuendesha kesi hii na nimewasiliana na wenzangu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza usikilizwaji,” alidai Kimaro.

Alidai wamepitia faili kabla ya kuanza usikilizwaji wa awali, wanataka kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na wanaona kutakuwa na ongezeko la washtakiwa wengine.

Kimaro alidai mshtakiwa mmoja yupo nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na utaratibu wa kumleta umekamilika, hivyo aliomba kesi iahirishwe.

Kwa upande wa mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, Domician Rwegeshora, Abraham Senguji na Kashindi Thabit, waliomba kesi hiyo kuahirishwa hadi Aprili 18, mwaka huu kwa kuwa mawakili watakuwa wamerudi katika mkutano mkoani Arusha.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 18, mwaka huu kwa usikilizwaji wa awali na washtakiwa walirudishwa mahabusu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwamo ya utakatishaji fedha wa Dola 375,418 za Marekani.

Malinzi na wenzake walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni mwaka jana na wapo mahabusu kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*