VIERI AWATOLEA UVIVU WACHEZAJI WA INSTAGRAM

MILAN, Italia


 

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Italia, Christian Vieri, amewaibukia mastraika wa kizazi hiki kwa maisha yao ya ‘kuuza sura’ kwenye mitandao ya kijamii kuliko kunoa viwango vyao vya kupachika mabao.

Vieri anakumbukwa kwa kuzitumikia timu za Inter Milan na Juventus, ambako alikuwa akicheka na nyavu kwa kiwango cha kuridhisha.

Lakini gwiji huyo alisema kuwa washambuliaji wa miaka ya sasa wanapoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko kutikisa nyavu.

“Siku hizi ili uonekane straika bora inabidi uwe na akaunti nzuri ya Instagram, hawajitumi kufunga mabao 30 kila msimu, hawaumii wanaposhindwa kufunga bao kila wikiendi.

“Enzi zetu tulikuwa tunaumia mno tulipokuwa tunakosa mabao. Tulikuwa tukijifungia vyumbani na siku iliyofuata tulijitahidi kufuatilia makosa tuliyofanya ili tujifunze. Siku hizi hawafanyi hivyo, enzi zetu tuliumwa ugonjwa wa kufunga mabao,” alisema Vieri.

Vieri alifunga mabao 236 katika mechi 476 alizocheza ngazi ya klabu, wakati akiwa na timu ya taifa ya Italia alitikisa nyavu mara 23 katika michezo 49.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*