VICTOR MOSES: YATIMA ALIYEDHARAULIWA NA MOURINHO, SASA ANANG’ARA

LONDON, England

VICTOR Moses ni jina maarufu kwenye Ligi Kuu ya England na timu ya Taifa ya Nigeria, ni  yatima aliyeamua kutafuta maisha yake kabla ya kutimiza ndoto alizokuwa nazo za kuwa mwanasoka wa kulipwa.

Ameibuka na kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa  Chelsea na Ligi Kuu England msimu huu, baada ya kuandika historia kwa  kubadili nafasi yake uwanjani.

Kabla ya kuhamia nafasi ya beki wa pembeni, nyota huyo aliye na umri wa miaka 25, alikuwa mshambuliaji hatari akitokea pembeni.

Mafanikio hayo hayawezi kubezwa ikilinganishwa na historia ya maisha yake. Wengi hawaifahamu historia ya kusikitisha iliyoko nyuma ya mafanikio ya Moses.

Mauaji ya wazazi wake

Staa huyo alikuwa mitaani akicheza soka na watoto wenzake wakati baba yake, Austin aliyekuwa kasisi katika kanisa lake na mama yake, Josephine, walipovamiwa na kuuawa.

Mauaji hayo yalihusishwa na chuki za kidini baina ya waislamu walio wengi na wakristo wachache nchini Nigeria na baba yake alikuwa mlengwa.

Moses alitafutiwa makazi na mjomba wake kwenda kuishi nchini England kama mkimbizi.

Aliwasili Kusini mwa London na hakumjua mtu yeyote zaidi ya kupokelewa na walezi na alijiunga na klabu ya Cosmos 90 baada ya juhudi zake binafsi kuomba kuichezea.

Timu hiyo ilikuwa kibonde na siku ya kwanza anaichezea, Moses alicheza beki wa kati na siku hiyo alifunga mabao manane.

Mafanikio yake Chelsea yanahusishwa na mchango wa aliyewahi kuwa nahodha wa zamani wa  Chelsea, Colin Pates.

Pates ni nani?

Pates ni kocha  aliyekijenga  na kukikuza kipaji cha Moses wakati akiwa anasoma shule ya Whitgift iliyopo Croydon na sasa anajivunia kumwona mwanafunzi wake huyo akiwa mchezaji nyota wa Chelsea.

“Sikuwahi kutarajia Moses angemudu kuwa beki wa pembeni, sikuwahi kufikiria kama angeweza kuchagua kucheza nafasi hiyo na kuifurahia, ameonyesha kiwango kizuri na amewathibitishia wengi kuwa anaweza,” alisema Pates.

Pates ambaye ni kocha wa zamani na mchezaji wa Chelsea, anasema Moses alipenda  soka na alikuwa na furaha  na hakuwa na msongo wa mawazo kutokana na kuwa peke yake.

Kocha  huyo aliyefundisha soka katika klabu ya  Whitgift kwa miaka  20,  anasema maisha ya Moses yalikuwa siri na hakuwahi kuyazungumzia ila alikuwa na furaha wakati akiwa shule na alipewa uhuru kutokana na kufanya vizuri katika masomo yake na walimu walitumia muda mwingi kumsaidia.

“Shule ilifahamu historia ya maisha  yake na kile kilichowakuta wazazi wake na klabu ya  Crystal Palace iliyomsajili ilitambua suala hilo.

Pates anakumbuka jinsi alivyokuwa akimshauri na kusema: “Victor hakuwa  mvivu na kuna wakati nilimpa moyo na alikuwa anajituma kwa bidii.

Ushangiliaji

“Alikuwa anabinuka kwa furaha alipofunga bao na tuliwahi kumkataza kwa sababu angeweza kuumia  kutokana na kutotua vizuri na kwamba  kuna mambo alikatazwa na kukemewa,”

alisema kocha huyo wa zamani wa Pates.

“Alikuwa shujaa shuleni, alishinda vikombe vingi kuanzia ngazi ya wilaya na taifa, alishinda Kombe la vijana la FA mwaka 2005 na kuna wakati alifunga mabao  5-0 peke yake.

Mafanikio

Moses alisajiliwa na Crystal Palace  na  kupata  nafasi katika kikosi cha kwanza akiwa na umri wa miaka 16 na kuitwa katika vikosi vya timu ya taifa ya  England  ya vijana.

Aliamua kuichezea timu ya taifa ya  Nigeria, baada ya kuitwa katika kikosi hicho na alitoa mchango wake na timu hiyo ikafanikiwa kuwa mabingwa wa kombe la Mataifa ya  2013.

Akionekana kuwa na ndoto za kufanikiwa baada ya kusajiliwa Chelsea, ghafla alianza kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza na alikopeshwa katika  klabu za Liverpool, Stoke na West Ham.

Mambo hayakunyooka katika klabu, hivyo kwa kukosa nafasi ya kudumu katika vikosi vya kwanza na mara chache alicheza akitokea benchi.

Arejea Chelsea

Hatimaye Moses alirejea Chelsea msimu uliopita na kocha wake zamani, Pates hakushangazwa na kiwango chake anachoendelea kukionyesha msimu huu.

Moses anazungumza lafudhi ya wenyeji wa Kusini mwa Jiji la London kutokana na kukulia  jijini humo.

“Nimekopeshwa katika klabu tatu tofauti, ila kwa sasa nina kocha mzuri ambaye anatoa nafasi kwa vijana kufanya vizuri na ndicho ninachokifanya hivi sasa, nataka kuendelea kufanya vizuri kila mchezo,” alisema Moses.

Kuanzia Oktoba mosi, nyota huyo alijumuishwa kikosini na kocha Conte na Chelsea, haijapoteza mchezo hata mmoja.

Katika mechi ya Ligi Kuu  England dhidi ya Middlesbrough iliyochezwa  mwishoni mwa wiki, Moses alitunikiwa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo, akiisadia Chelsea kuibuka na ushindi wa  1-0.

Conte azungumza

Antonio Conte anakiri kushangazwa kuwa Victor Moses alikosa nafasi katika kikosi cha Jose Mourinho alipokuwa Chelsea na anasisitiza aliona uwezo wake mazoezini, siku ya kwanza alipowasili Stamford Bridge.

Moses  ni mchezaji muhimu katika mfumo wa 3-4-3 unaotumiwa na Conte ulioipa mafanikio ‘Blues’ kuanzia Septemba.

“Nilitambua uwezo wake siku ya kwanza wakati wa maandalizi ya msimu,” Conte alilieleza Gazzetta dello Sport. “Moses ana kipaji, nguvu na uwezo wa kukimbia mita 70 uwanjani. Nashindwa kuficha hisia zangu kutaka kujua sababu za mchezaji kama huyu kutothaminiwa.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*