Vichai kuzikwa kesho, mwanawe aahidi kuendeleza mapambano

LONDON, England


 

MAZISHI ya mmiliki wa klabu ya Leicester City, Vichai Srivaddhanaprabha, aliyefariki kwenye ajali ya kuanguka na kuungua kwa helikopta yake mwenyewe, yanatarajiwa kuanza wikiendi hii jijini Bangkok kwenye nchi aliyozaliwa ya Thailand.

Srivaddhanaprabha, 60, alikuwa ni mmoja wa wahanga watano waliokuwepo kwenye helikopta iliyoanguka katika uwanja wa kupaki magari nje ya Uwanja wa Leicester, King Power, usiku wa Jumamosi iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Thailand, mwili wa mwenyekiti huyo wa klabu hiyo, Vichai, unatarajiwa kusafirishwa leo kutoka Leicester kuelekea katika taifa hilo lililopo Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.

Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa watakaosafiri na mwili wa Vichai ni pamoja na mjane, Aimon na mwanawe, Aiyawatt.

Baada ya kifo cha baba yake, Aiyawatt ambaye alikuwa ni makamu mwenyekiti wa Leicester, alisema kwamba kwa sasa atayachukua majukumu mazito ya kubeba ‘matarajio makubwa na ndoto’ alizoacha mzazi wake huyo.

Kwa upande wa wachezaji wa kikosi cha Leicester, wao waliendelea na mazoezi kama kawaida kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu England watakaocheza wikiendi hii dhidi ya Cardiff.

Leicester ilitarajiwa kucheza mechi ya Kombe la EFL dhidi ya Southampton mapema wiki hii, lakini mtanange huo uliahirishwa kufuatia kifo cha Vichai.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*