VAR yawachefua Sarri, Pochettino

LONDON, England

KOCHA wa Chelsea, Maurizio Sarri, amewashutumu waamuzi wa Uingereza kushindwa kufahamu jinsi ya kutumia teknolojia ya mwamuzi, VAR, baada ya timu yake kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la EFL  dhidi ya Tottenham na huku mwenzake wa Spurs, Mauricio Pochettino, akilalamika kutopenda matumizi yake.

 Katika mchezo huo wa marudiano ambao ulipigwa usiku wa kuamkia jana katika Uwanja wa Stamford Bridge, Harry Kane ndiye aliyeipa Tottenham bao hilo la ushindi kwa njia ya penalti ikiwa ni dakika ya 26.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya England, ndiye aliyesababisha penalti hiyo bada ya kuangushwa na mlinda mlango wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga, lakini wakati huo mwamuzi wa pembeni alishanyoosha kibendera juu akiashiria kuwa alikuwa ameotea.

Kufuatia hali hiyo, mwamuzi wa mechi hiyo alikwenda kushauriana na wa video, ambaye picha yake ilionesha, Kane alikuwa sambamba na Cesar Azpilicueta na hivyo kuamua kumpa kadi Kepa na kisha akaamuru upigwe mkwaju wa penalti.

Akizungumza na Sky Sports, Sarri alisema kuwa kwa mtazamo wa  Chelsea wanaona kwamba straika  huyo wa  Tottenham, alikuwa ameotea na kwamba kitendo cha mwamuzi wa pembeni kunyoosha kibendera ndicho kilichowafanya mabeki wa timu yake kushindwa kuendelea kumkaba.

“Dakika chache zilizopita niliiangalia picha ya video katika kamera zetu alikuwa ameotea,” alisema kocha huyo wa zamani wa Napoli.

 “Kamera zetu zilikuwa sambamba na  Kane na alikuwa ameotea, lakini sio jambo la muhimu kwani muhimu mwamuzi wa akiba aliufuata mpira na kunyoosha kibendera na kuashiria kuwapo kuotea lakini haikuwasaidia mabeki wetu,” aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*