UZINDUZI MISS TANZANIA TUMAINI JIPYA KWA WAREMBO

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MWISHONI mwa wiki iliyopita Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alizindua mashindano makubwa ya urembo nchini, Miss Tanzania, ikiwa ni siku kadhaa zimepita toka Kampuni ya The Look ichukue majukumu ya kuyasimamia.

Uzinduzi huo ulifanyika juzi katika Ukumbi wa Makumbusho, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau wa urembo, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), wabunifu wa mavazi na warembo waliowahi kupita kwenye jukwaa hilo na kufanikiwa.

Miongoni mwa warembo hao ni Miss Tanzania 1994, Basila Mwanukuzi, mrembo ambaye hivi sasa ndiye mratibu wa shindano hilo baada ya kuipokea Kampuni ya Lino International Agency iliyoratibu mashindano hayo toka mwaka 1994.

Katika shughuli hiyo ya uzinduzi, mikakati na dira mpya ya mashindano hayo yalitangazwa lengo likiwa ni kurudisha hadhi ya Miss Tanzania ambayo miaka ya hivi karibuni ilikuwa imepotea kwa matukio kadhaa.

Miongoni mwa mikakati ya Miss Tanzania mpya ni kufuta mashindano ya vitongoji (Miss Kitongoji) na badala yake warembo wote watajumuishwa kwenye ngazi ya mkoa kwa sababu katika ngazi hiyo ya chini ndiko kulijaa ubabaishaji mkubwa na kufanya shindano zima kupoteza hadhi.

Basila alibainisha hayo akiwa kama mrembo mzoefu na mwathirika wa kutopata zawadi zake kwa wakati aliposhinda taji hilo miaka ya 90. Bila shaka anafahamu jinsi gani warembo chipukizi wanavyokutana na changamoto katika ngazi za vitongoji hasa mashindano hayo madogo yanapoandaliwa na kampuni zisizotekeleza ahadi zake.

Naye Waziri Mwakyembe ambaye siku hiyo alikata utepe kuashiria uzinduzi wa Miss Tanzania mwaka 2018, aliendelea kusisitiza dhamira yake ya kutaka mashindano ya Miss Tanzania yawe na heshima kubwa kama ilivyokuwa miaka ile ya 2000.

Alikumbusha kuwa kipindi hicho msimu wa Miss Tanzania ukifika mashabiki walikuwa wanagombea tiketi za kuingia kwenye onyesho kwa sababu lilikuwa na nguvu ya ushawishi kwa mashabiki, wadau na hata kampuni mbalimbali kuwekeza.

Mwakyembe alionya waandaaji wa Miss Tanzania kuwazungusha washindi pale wanapotakiwa kupewa zawadi zao alkikumbusha jinsi mrembo Diana Edward, Miss Tanzania 2016/18, alivyohangaika kupata zawadi yake ya gari, alilokuja kupewa mwaka mmoja baadaye baada ya shindano.

Imani yangu uzinduzi huu wa Miss Tanzania ni tumaini jipya kwa warembo wanaotaka kutumia jukwaa kutimiza malengo yao katika sekta ya urembo. Heshima ya shindano itakaporudi na kampuni za uwekezaji zitamiminika kudhamini.

Kama nitakua sahihi, sababu kubwa ya zawadi kuchelewa ni kukosekana kwa wadhamini wa uhakika na nijuavyo mimi hakuna kampuni itakayowekeza fedha yake katika kitu ambacho hakina hadhi au heshima itakayowapa faida.

Hivyo ubabaishaji uliokuwa unafanyika ndani ya Miss Tanzania ndio ulichangia kwa kiasi kikubwa kuwakimbiza wadhamini na hatimaye shindano kupoteza hadhi yake kwenye nyanja ya urembo.

Matumaini yangu kwa Miss Tanzania 2018, natarajia kuona heshima na hadhi ikirudi ndani ya mashindano hayo na yatakuwa katika mfumo wa uwazi na ukweli hivyo kupata warembo wenye mchango chanya kwenye jamii.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*