USIWE NA PUPA, KUWA MAKINI, USIHUKUMU KWA KUTUMIA FIKRA

NA RAMADHANI MASENGA  |

WASIWASI mwingi wa watu katika maisha unajengwa katika fikra. Vitu vingi havitishi wala havina madhara kama wengi wanavyodhani, bali fikra potofu hutufanya kuamini hivyo.

Ni vijana wachache unaweza kuwaambia waende katika ofisi ya Bunge kuomba nafasi za kazi wakakubali kwa haraka. Wengi ukisema hivyo, si ajabu wakaanza kuguna kwanza ama kuamua kupotezea habari yenyewe. Kisa?

Hawaamini kama wanaweza kuingia na kukubaliwa maombi yao. Usidhani walienda kujaribu wakakataliwa. Hapana. Ila wametengeneza fikra kuwa hawastahili ama wakienda watakataliwa. Hii ipo katika mambo mengi.

Watu tumekuwa  na kawaida ya kutengeneza fikra juu ya kitu ama jambo f’lani kuliko kuangalia ukweli wenyewe. Asilimia zaidi ya hamsini ya watu wanaolaumu  wanasalitiwa huwa ni fikra tu, wala si ukweli halisi.

Watu wamekuwa wepesi wa kuhukumu kwa kutumia fikra bila kukaa nao na kuangalia mahali penye tatizo ili limalizwe.

Kuna dada mmoja aliniambia  anatafuta njia ya kuchana na mchumba wake kwa sababu tangu amepata kazi ya kuendesha magari ya kwenda nje ya nchi amebadilika.

Hampigii simu kama zamani, akiamua kumpigia yeye, jamaaa haongei sana zaidi ya kusema nitakupigia baadaye, ilmradi tu. Kwa sababu hizo dada yule anasema anataka kuachana na mchumba wake.

Kafikia uamuzi huo baada ya kuhisi mpenzi wake atakuwa amepata msichana mwingie anayemthamini zaidi yake. Nani kamwambia hayo? Fikra zake.

Huenda akawa sahihi, ila hata yeye hana uhakika, anashibishwa mawazo na fikra zake na kuamua kuamini. Kwanini usitafute muda ukae na mwenzako ukazungumza naye juu ya matatizo unayoyaona?

Ukizungumza naye ndipo utakapopata usahihi ama upotofu wa fikra zako. Huenda ikawa kazi ndiyo inamfanya asiwe kama alivyokuwa zamani.

Huenda kuna matatizo yamejitokeza ghaf’la ndiyo yamesababisha hali kama hiyo. Haya yote huwezi kuyajua kama utaamua kutumia fikra zako  kutoa maamuzi bila kumshirikisha.

Angalau watu wengi wenye hali f’lani ya kujiamini huwa wanafikiria zaidi wanapoona kuna mabadiliko kwa wenzao. Huwa hawakimbilii kudhani wanasalitiwa ila huruhusu ubongo wao kufikiri zaidi.

Wapo wanaoweza kudhani wenzo wametingwa na majukumu, wengine wanajiuliza kama kuna matataizo yamewapata wenzao ila si kuamini tu wanasalitiwa.

Kuepuka kuteseka kwa fikra unapoona mwenzako amebadilika tofauti na zamani kaa naye kisha amua kutoa dukuduku lako. Mapenzi hayapelekwi hivyo.

Ili kuweka mapenzi yako katika hali ya amani unapoona mwenzako anaenda tofauti kaa naye kisha mueleze kinachokusibu. Ukiendekeza dhana kila siku unaweza kukuta unaingia katika ugomvi na mpenzi wako bila sababu za maana.

Fikra za namna hiyo ukiziendekeza si ajabu hata ukimkuta mwenzako anaongea na mtu wa jinsia tofauti ukaanza kuhisi ndiye aliyesababisha amani katika mahusiano yako kupaa. Zote fikra hizo.

Maisha yana mambo mengi. Ukimya wa mwenzako huenda si lazima ukasababishwa na kuwa na mtu mwingine. Sababu ziko nyingi, ukihukumu bila kumsikiliza mwenzako unajiumiza bure.

Acha kuteseka kwa mawazo yako mwenyewe. Huyo unayefikiria anakusaliti eti kwa sababu tangu jana ajakutafuta kwenye simu, huenda yuko matatizoni.

Wakati unalia na kumlani kumbe mwenzako labda simu yake ina matatizo. Sasa kwanini unajitesa bure kwa mtu ambaye huna uhakika na anachokifanya muda huu.

Kwani ni mara ngapi umeshawahi kumfuma na sms  kutoka kwa hawara? Acha kupelekeshwa na fikra hasi. Kabla hujahukumu wala kuanza kuumizwa kutokana na mabadiliko fulani ya mwenzako hakikisha unapata ukweli halisi.

ramadhanimasenga@yahoo.com 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*