USIPOWAJUA MASHABIKI WA SOKA, WATAKUUMIZA KICHWA

NA EZEKIEL TENDWA

0718769944

JUMATANO wiki hii nilijumuika na wadau wa soka kuushuhudia mchezo     wa  Kombe la Mapinduzi kati ya Yanga dhidi ya wageni waalikwa URA wa nchini Uganda, uliomalizika kwa Yanga kupoteza kwa penalti 5-4.

Timu hizo zililazimika kupigiana penalti baada ya kutoka sare ya kutofungana katika muda wa kawaida wa kumaliza dakika 90 na Yanga kuanza safari kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika kushuhudia mchezo huo, niliondoka na mambo mawili makubwa. Mosi ni jinsi kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alivyolaumiwa baada ya Obrey Chirwa kukosa penalti na jingine namna kocha mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, alivyoamua kujiweka pembeni kwenye mchezo huo na kumuachia kila kitu msaidizi wake.

Nianze na hili la Nsajigwa kumtwisha zigo Chirwa. Niliushuhudia mchezo huo kwenye kibandaumiza kimoja pale Kibamba, ambapo wakati Chirwa anapasha misuli ili kuingia mashabiki wa Yanga walilipuka kwa furaha lakini alipokosa penalti ikawa nongwa.

Chirwa hakuwa na wenzake kwa muda mrefu na badala yake alikuwa kwao Zambia ikidaiwa kuwa alikuwa na madai yake kwa uongozi, ambapo baada ya kukaa meza moja na mabosi zake, wakakubaliana kurudi kundini.

Baada ya kurudi kundini, moja kwa moja alikwenda visiwani Zanzibar kuungana  na wenzake katika mchezo wa hatua ya nusu fainali dhidi ya URA na kwa bahati mbaya sana kama inavyoweza kutokea kwa wachezaji wengine duniani, akapoteza penalti yake iliyowatupa nje ya michuano hiyo.

Kukosa penalti kuliwafanya baadhi ya mashabiki wa Yanga kuanza kutoa maneno ya kejeli kwa Nsajigwa pamoja na mchezaji mwenyewe.

Mashabiki wale wale waliokuwa wakimshangilia wakati anapasha misuli kabla ya kuingia uwanjani, ni wale wale waliomlaumu kocha kumuingiza na hii ni baada ya kukosa penalti.

Binafsi ningewaelewa mashabiki kama muda ule Chirwa anapasha misuli ili aingie uwanjani, pale pale wangeanza kulaumu kwanini anaingizwa wakati hakuwapo nchini kwa muda mrefu.

Walichokifanya walishangilia sana, lakini alipokosea wakanuna, wakamuona hafai, wakaliona benchi la ufundi dhaifu.

Nina uhakika kwamba kama Chirwa angefunga ile penalti yake, mashabiki wangemuona shujaa, wangemuona pia Shadrack Nsajigwa shujaa kwa kumpanga mtu ambaye hakuwapo lakini alafanya vizuri.

Kwa sababu mambo yalikwenda tofauti hapo wakasahau kwamba walimshangilia alipoingia na alipokosea wakamkana.

Baada ya mchezo ule Nsajigwa alitupiwa kila aina ya neno na baadhi ya mashabiki waliokerwa na penalti aliyoikosa Chirwa bila kujua kuwa hata akina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, nao mara kadhaa wanakosa kama ilivyotokea kwa Chirwa.

Hawamuangalii na kumpa pongezi zake Nsajigwa aliyekwenda na kikosi cha wachezaji wengi vijana wakapambana mpaka wakafika hatua ya nusu fainali, hapana, wao wanachojua ni kulaumu tu namna Chirwa alivyokosa ile penalti.

Nina uhakika kama kocha wao Lwandamina ambaye naye hakuwapo muda mrefu kutokana na matatizo ya kifamilia yaliyokuwa yakimkabili kwao Zambia, angeamua kwenda kukaa kwenye benchi na timu ikapoteza lawama zote angeangushiwa yeye na wangeshinda bado angesifiwa kwamba ni bonge la kocha.

Ukweli ni kwamba mashabiki ni watu ambao hawana urafiki wa kudumu na mtu. Ukifanya vizuri watakushangilia sana lakini ukikosea wewe unaweza ukawa adui yao mkubwa. Wao hawajui kama kuna kukosea, hawajui hilo kabisa.

Taarifa zilizopo ni kwamba baada ya timu hizo kwenda kwenye mikwaju ya penalti, baadhi ya wachezaji wa Yanga akiwamo Ibrahim Ajib, walikataa kwenda kupiga penalti kwa kuhofia wakikosa wataingia kwenye lawama ndipo Chirwa akajitosa kuokoa jahazi.

Hapo mashabiki waanze kujitathmini kwamba mpaka inafikia baadhi ya wachezaji wanagoma kwenda kupiga penalti kuogopa lawama, hiyo inamaanisha kuwa kuna haja ya kila mmoja kuthamini kazi ya mwenzake. Binafsi sidhani kama kuna mchezaji anayeweza kukosa penalti kwa makusudi.

Kama leo hii Chirwa kukosa penalti baadhi ya mashabiki wameanza kuvimba wakitaka kupasuka, hiyo inamaanisha kuwa hata litakapotokea tena tukio kama hilo la timu kupigiana penalti, wachezaji wengi wa Yanga wataingiwa na woga kwa kuogopa kutolewa kafara.

Madhara ya kuogopa kupiga penalti ni kwamba mchezaji akienda huku roho inadunda, kuna asilimia kubwa akapoteza na hicho ndicho kinachoweza kuwakuta wachezaji wa Yanga na timu nyingine kama wasiporekebisha mwenendo wao. Kama akina Ronaldo na Messi wanakosa, hawa wanaocheza soka la Tanzania ni nani wasikose?


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*