googleAds

Usajili Yanga wavuja

NA ZAINAB IDDY

IWAPO mabosi wa Yanga pamoja na wafadhili wa klabu hiyo, watazingatia mapendekezo yaliyopo katika ripoti ya kocha wao, Luc Eymael, msimu ujao mashabiki wao watakuwa wakiombea timu yao icheze kila siku kwani watakuwa na uhakika wa kupata burudani.

Pamoja na Eymael kukataa kata kata kutaja yaliyomo kwenye ripoti yake aliyokiri kuukabidhi uongozi wa Yanga wiki iliyopita, BINGWA limefanikiwa kunasa kilichopo katika faili lake.

Ikumbukwe kuwa gazeti hili lilikuwa la kwanza kufanya mahojiano maalum na Eymael mara baada ya kutua nchini ambapo alifunguka mengi, ikiwamo aliyopanga kuifanyia Yanga.

Toka wakati huo, gazeti hili limekuwa karibu mno na Mbelgiji huyo pamoja na msaidizi wake wa viungo, Riedoh Berdien, raia wa Afrika Kusini. 

Ni kutokana na ukaribu huo, imekuwa rahisi kwa BINGWA kupenyezewa lolote lile linalomuhusu kocha huyo na kikosi cha Yanga kwa ujumla.

Sasa wakati Eymael akiwa ametimkia nchini kwao Ubelgiji kwa kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara imesimamishwa kutokana na hofu ya maambukizi ya virus vya Corona, BINGWA limefahamishwa kuwa kocha huyo amewataka Yanga ifanye iwezalo isikose kumsajilia wachezaji watano wa kiwango cha juu.

Wachezaji hao ni mabeki watatu; wa kulia, kushoto na wa kati, lakini pia kiungo mmoja mtundu na mbunifu kama Clatous Chama wa Simba pamoja na washambuliaji wawili wenye njaa ya mabao.

“Katika ripoti yake (Eymael), ameainisha mambo mengi ya kufanyiwa kazi kipindi hiki ligi ikiwa imesimama hadi msimu utakapomalizika. Kuna wachezaji ametaka uongozi ujiandae kuwauza au kuwatoa kwa mkopo au hata kuachwa kabisa.

“Pia, wapo aliopendekeza ufanyike utaratibu wa kuwaongezea mikataba au kuiboresha. Baadhi yao ni makipa wote wawili (Farouk Shikalo na Metacha Mnata), Japhary (Mohammed), Lamine (Moro), Fei Toto (Feisal Salum), Tshishimbi (Papy), Morrison (Bernard), Makapu (Said Juma), Nchimbi (Ditram) na wengineo.

“Kwa upande wa wachezaji wapya, wapo wazawa kama watatu hivi au wanne kama watapatikana, ila wakikosekana kuna wachezaji atawaleta wa kiwango cha juu. Tatizo ni fedha za usajili, hasa kwa wachezaji wa kigeni anaowataka,” alisema mtoa habari wetu aliye karibu na Eymael.

Alisema kocha huyo anataka kuwa na kikosi cha wachezaji wenye kiwango cha Morrison au zaidi yake na tayari ana majina ya wakali kama sita hivi anaotaka kuungana nao kuifanya Yanga kuwa tishio msimu ujao.

Habari zaidi kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa wafadhili wa klabu hiyo, Kampuni ya GSM Group na wengineo wanaofanya mambo yao chini kwa chini, wapo tayari kutenga zaidi ya bilioni 1.5 kwa ajili ya usajili pekee ili kukisuka upya kikosi chao.

Imeelezwa kuwa kitendo cha Yanga kuifunga Simba bao 1-0 hivi karibuni na kiwango kilichoonyeshwa na Morrison, kimewavutia matajiri wengi wa klabu hiyo ambao wanaamini iwapo watamtimizia Eymael mahitaji yake, msimu ujao utakuwa ni kicheko kwa Wanajangwani.

Katika moja ya mahojiano yake na BINGWA, Eymael aliwahi kusema kuwa ana orodha ya wachezaji wengi wa kiwango cha juu zaidi ya Morrison aliowafundika kwenye timu mbalimbali.

Na kabla ya kuondoka nchini wikiendi iliyopita, Eymael aliyeanza jukumu la kuinoa Yanga Januari 9, mwaka huu, akichukua mikoba ya Mwinyi Zahera, alisema kuwa kutokana na mabadiliko anayoyaona katika kikosi chake kwa sasa, ana matumaini ya kuwa na timu bora msimu ujao.

“Wachezaji waliopo hivi sasa wengi nimewakuta na sijaanza nao msimu, hivyo hatua tuliyofikia sio mbaya kulingana na vijana nilionao…akili na macho yangu ni kuwa na kikosi bora msimu ujao.

“Nimeshakabidhi ripoti ya aina ya wachezaji ninaohitaji wapya na kwa wale wa zamani ambao nitaendelea nao, bila shaka kama watapatikana msimu ujoa tutakuwa na kikosi bora zaidi ya vyote vilivyokuwepo msimu huu,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*