UPENDO KUTOKA SAYARI NYINGINE (23)

ILIPOISHIA JANA… Alifoka mzee Martin kwa kutokuamini maneno hayo. Sikuambii kwa maneno matupu baba yangu nataka uzungumze na binti yako mwenyewe hapo ndio mahali penye jibu la swali lako.” Alijibu Seba na kumkabidhi Judith simu lakini Judith alikuwa akilia machozi mengi…SASA ENDELEA..

Ilibidi mzee Martin ajaribu kumtuliza ili wasalimiane. “Baba shikamoo.” Hatimaye Judith aliweza kutoa sauti na kumsalimia baba yake. Woow! Judith binti yangu umepona kabisa?” Alisema mzee Martin kwa sauti iliyokuwa na kitetemeshi kinachoashiria kilio. “Ndiyo baba yangu. Nashukuru sana kwa ninyi kunishughulikia hadi kufikia hapa.

Niko mzima kabisa na nitafurahi sana kukuona mzazi wangu.” Alisema Judith huku akifuta machozi machoni mwake.  “Asante mwanangu lakini mtu aliyesumbuka na wewe kwa kiwango kikubwa ni huyo mchumba wako Seba.

“Alitelekeza kila kitu cha maisha yake kwa ajili ya kukuhudumia. Ametumia mali zake kwa ajili ya kulipia kila gharama ya matibabu yako. huu ni upendo mkubwa sana ambao sijawahi kuona popote japo nimeishi miaka mingi na kusikia historia nyingi. Kamwe sijawahi kusikia mtu aliyefanya hivyo alivyofanya huyo kijana Sebastian,” alisema Mzee Martin.

“Nashukuru baba nimesikia kila kitu juu ya hilo na mimi sina la kufanya zaidi ya kushukuru na kumpa Mungu utukufu kwa ajili ya kuyashikilia maisha yetu na kuharakisha kupona kwangu. Seba ni chaguo langu sahihi na Mungu alimleta kwangu ili awe mwenzangu katika maisha yote.

“Najua kuwa alilofanya ni wajibu wake kwa ajili ya mke wake mtarajiwa japo si wengi wanaoweza kufanya alivyofanya,” alisema Judith maneno ambayo yalimhakikishia kuwa amepona asilimia mia moja.

Hekima zake na busara zilikuwa za hali ya juu. “Nashukuru kusikia hivyo binti yangu. Nitakuja huko si siku nyingi kuanzia leo.” Mzee Martn alihitimisha mazungumzo na binti yake kwa furaha ya aina yake.

Judith alirudisha simu kwa Seba.  “Mzee panda ndege ya kesho mchana nitapiga simu ofisini kwangu nao watakuchukulia tiketi ya ndege na kukuletea hapo nyumbani. Ningependa usafiri na shangazi Adela pamoja na baba mdogo Alen. Usiku wa kesho tutakuwa na muda mzuri wa kuwa pamoja kwa mazungumzo yetu. Nao nitatuma tiketi zao ili msafiri wote hiyo kesho,” alisema hivyo Sebastian na hatimaye akakata simu.

***

Jioni hii ilikuwa ni shangwe kubwa mioyoni mwa Seba na mchumba wake pale walipoyatembelea maduka mbalimbali ya nguo ghali sana katika Jiji la Nairobi. Waliweza kununua nguo za gharama kubwa wakiwa wote.

Seba alihakikisha anamnunulia mchumba wake nguo za gharama kubwa kwa matumizi ya chuoni na zile zilizohusu sherehe ya harusi ya mdogo wake na Njoroge usiku wa siku hiyo. Baada ya kufanya manunuzi hayo waliingia katika gari na kurudi chuoni kwa maandalizi ya sherehe ya usiku huo. Judith alijisikia malkia hasa katika kipindi chote akichokuwa karibu na Seba.

Hata baada ya harusi kwisha, walirudi chuoni wenye furaha nyingi na kujifunza mengi. “Nimejifunza mengi sana  Seba. Naisubiri siku ya harusi yetu itakuwa ni ya kihistoria hasa.” Alijibu Judith wakati gari likisimama kwenye uwanja wa chuo na wao wakaanza kuteremka na kuelekea ndani. Baada ya Seba kumfikisha Judith chumbani kwake alimuaga na yeye akaenda chumbani kwake.

***

Utata ndani ya ofisi ya Chief

Ilikuwa ni mshangao wa aina yake kwa katibu muhtasi wa ofisi ya mkurugenzi wa habari ambaye hakupenda kutajwa jina lake moja  kwa moja. Haikujulikana sababu hasa ila jina la Chief ndilo lililozoeleka na watu waliridhika kumwita hivyo. Sambamba na ughali wa kulijua jina lake, hata hivyo mtu huyo amekuwa adimu sana kuonekana machoni kwa watu. Huyu alikuwa ndiye Chief wa shirika la uandishi wa habari. Shirika lenye kusimamia haki za waandishi wa Riwaya na miswada mbalimbali, lijulikanalo kama UWARIDI.

Majukumu yake yalikuwa ni makubwa sana kwa ajili ya shirika na pia alikuwa ni Mpelelezi wa kujitegemea akisaidia kukabiliana na ujambazi pamoja na hujuma zinazofanyika nchini.  Kazi zake nyingi alikuwa akishirikiana na Serikali lakini  alikuwa akizifanya kwa siri sana na mara kwa mara alikuwa akisafiri kwenda katika nchi mbalimbali kwa mujibu wa majukumu yake.

Mambo mengi alikuwa anayafanya kwa umakini sana huku akijigawanya katika kutimiza kila eneo la majukumu yote aliyonayo. Ilikuwa ni aghalabu sana kukaa nyumbani kwake, familia yake ilimkosa sana na hata mkewe ambaye alikuwa ni mbunge wa viti maalumu alikuwa hakai na mumewe hata kwa masaa mawili mfululizo kwa ajili ya mazungumzo ya kifamilia. Kila wakati majukumu ya kiserikali na ya shirika lake la uandishi wa habari yalimlemea.

Mara zote alikuwa akiacha maagizo kwa ajili ya kazi na msaidizi wake alikuwa akiyawakilisha kwa watu muhimu. Huu ndio uliokuwa utaratibu hasa wa bosi wa shirika hili, utaratibu ambao umezoeleka kwa watenda kazi walioko chini yake. Mkuu huyu wa shirika alikuwa akifika mara kwa mara hasa kunapokuwa na mambo muhimu ya kuyashughulikia  yanayohusu habari nyeti, au vikao muhimu. Mara nyingine hupotea na kusahaulika kwani habari zake si wote wanazipata zaidi ya msaidizi wake ambaye huchukua nafasi yake mara nyingi. Mwingine ambaye hubeba siri za bosi wake ni katibu muhtasi. Huyu ni mama wa makamu ambaye umri wake hauzidi miaka arobaini na mbili jina lake aliitwa Selina.

Asubuhi hii alikuwa na mshangao mkubwa baada ya kukuta kwenye  meza yake kuna kipande cha karatasi  chenye mwandiko wa Bosi wake. Hakujua kama alikuja ofisini saa ngapi na alitoka muda gani. Moyo wake ulienda mbio kidogo kwani bosi wake huyo alimjulisha kuwa yuko safarini nchini Uholanzi. Hakujua kuwa karatasi hiyo yenye mwandiko wa bosi wake ilifikaje ofisini kwake wakati mtu mwenyewe hayupo kabisa nchini. Kabla ya kufungua karatasi ile ili aisome alitoka nje ili aonane na mlinzi. “James hivi mkurugenzi amefika hapa ofisini saa ngapi?” Aliuliza Selina huku akiwa na wasiwasi.

“Alifika saa mbili usiku Mamy na aliondoka saa nane na robo usiku. Inaelekea alikuwa na shughuli nzito sana ofisini.” Alijibu James mlinzi wa jengo hilo la shirika la uandishi. “Ina maana James umeingia zamu ya usiku? Kwani Ricky hajaja kukupokea si jana ulishinda hapa kazini?” Aliuliza Selina Katibu muhtasi wa ofisi ya Chief. “Madamu, Ricky ni mgonjwa jana alinipigia simu kuwa hataweza kufika ndio maana nikachukua na zamu yake. Alisema Jemes.

“Sawa lakini sijapenda huu mtindo. Pamoja na matatizo ya Ricky lakini usisahau kuwa wewe ni mwanadamu ambaye pia unachoka. Ungetoa taarifa ofisi ingefanya mpango kwa ajili ya kuleta watu wanaoweza kushika zamu ya Ricky kwa usalama wa mali za ofisi na kwa usalama wa afya yako pia.”

Alisema Selina Katibu Muhtasi wa Chief kisha akazama ofisini kwa ajili ya kuendelea na kazi zake. Alipofika ofisini kwake alikuta simu ya mezani ikiwa inamalizia mlio wa mwisho ikimaanisha kuwa ililia muda mrefu wakati alipokuwa akiongea na mlinzi. Kwa  kuwa hakujua ninani aliyepiga ilimbidi avute subira akijua kuwa mtu huyo anaweza kupiga tena.

Kilichomvuta zaidi kwa wakati huo ilikuwa ni ile karatasi yenye mwandiko wa bosi wake. Aliinyanyua na kuifungua kwa pupa  na kuanza kuisoma nayo ilikuwa imeandikwa hivi:

“Habari Selina. Labda utastaajabu sana kuona kipande hiki cha karatasi nilichokiandika kwa mkono wangu. Hizi si salamu kutoka Uholanzi bali niko hapa nchini nimeingia kwa kunyata kutokana na jambo nyeti nililoazimia kulifanya. Kilichonirudisha ni kuchunguza tatizo la upotevu wa mabilioni ya Escrow Tegeta. Hivi nimepotea tena lakini nitakapoibuka nitakuwa na mambo mapya ya kuyalisha magazeti yetu kwa faida ya wananchi wa Tanzania.

Ila habari kutoka mahali fulani zinaeleza kuwa Andrew yule mwandishi machachari yuko nchi ya jirani akiwa na habari za kutosha kuhusu Sebastiani Changawe na mpenzi wake. Ila nakutahadharisha kuwa usitoe habari hizi na wala waandishi wetu wasiandike chochote kwa sasa mpaka tutakapopata kitu hasa cha kuandika kuhusu watu hao. Nitakuona kwa wakati mtulivu ambao utakuwa na mengi ya kujaza kwenye mafaili yako ya kazi. Na kutakia kazi njema.

Itaendelea kesho


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*