googleAds

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU [38]

Ilipoishia Jana

Haraka Roika alishuka kutoka darini, akaelekea kufungua mlango na kutoka mle ndani. Ile anatoka tu, aligongana uso kwa uso na mijibaba yenye miraba minne ikiwa na bunduki.

SASA ENDELEA

Macho yalimtoka Roika Malino, alibaki kuwatazama wale watu asijue nini cha kufanya. Akiwa mithili ya mtu aliyegandishwa na barafu, huku mwili wake ukitetemeka, alibaki amekishika kitasa cha mlango, asijue akimbie au arudi ndani.

Mapigo ya moyo wake yalimuenda mbio kupita kawaida. Sasa alijua huenda maisha yake yamefika mwisho.

Wale watu nao walibaki na sintofahamu, wakimshangaa mtu aliyekuwa mbele yao. Mtu ambaye si mwenzao na si mfanyakazi wa jengo lile. Akiwa ametoka kwenye chumba chao.

Watu hao walikuwa ni Waarabu watano na wazungu wawili. Wakiwa wamevaa mavazi meusi ya kijeshi.

“Wewe ni nani?” kwa sauti kali na ya juu mmoja wao aliuliza.

Roika hakuwa na jibu la kuwapa, alibaki kuwatazama akisubiri msaada wa Mungu.

Haraka walimfuata huku wakinyanyua bunduki zao na kumuelekezea.

“Mikono juu! Kaa chini, kaa chini.”

Roika alitii amri akanyoosha mikono yake juu na kukaa chini. Mara tu walipomfikia, walimsogezea midomo ya bunduki zao karibu kabisa na uso wake. Waliangaliana wao kwa wao, wakijiuliza maswali kwa hisia za pamoja, juu ya mtu waliyekuwa wamemuweka chini ya ulinzi.

Ilikuwa imewashangaza sana, kumuona mtu wasiyemfahamu ndani ya himaya yao, himaya ambayo binadamu wa kawaida kuingia ilikuwa ni ngumu. Kwani wakazi wa mtaa huo waliijua vema hatari ya jengo hilo. Sura ya Roika kwao ilikuwa ngeni.

“Inuka juu, weka mikono kichwani,” aliongea mmoja wa watu hao, kwa lugha ya kiarabu.

Roika aliinuka, huku akiiweka mikono yake kichwani. Mapigo ya moyo wake yalizidi kumuenda mbio, jasho lilimtoka bila kukatika. Japo alikuwa akihofia maisha yake, lakini woga zaidi ulikuwa ni jinsi watu hao watakavyompeleka kule aliko mpenzi wake, Ramona na wafanyakazi wote. Alimuomba Mungu atende muujiza wake, wale watu wasimpeleke kule mkutano ulikokuwa ukiendelea.

Baada ya Roika kusimama, mmoja wao alimfuata na kumsukumia ukutani. Akaanza kumkagua kwa kumpapasa mwili mzima. Wakati huo Roika, alikuwa akimuomba Mungu watu hao wasifanikiwe kukiona kitambulisho chake cha UN, alichokuwa amekificha ndani ya waleti. Maana endapo watu hao watamjua kuwa ni mtu wa Umoja wa mataifa, itakuwa ni jambo la hatari kwake na kwa Umoja huo.

Wakiwa wanaendelea kumpekua, walifanikiwa kuiona waleti yake. Waleti iliyokuwa mfuko wa mbele. Waliichukua na kuanza kuipekua. Waliipekua sehemu zote. Kwa bahati nzuri waliziona pesa tu dola 200, ambazo ni sawa na shilingi 3,00000.

Lakini hawakukiona kitambulisho chochote, kinachomtambulisha Roika ni nani na anatoka wapi. Ina maana kuwa hata kitambulisho cha UN pia hawakufanikiwa kukiona mle ndani ya waleti

“Wewe ni nani na umefuata nini hapa?” aliuliza mmoja wale watu akiwa amekunja sura huku akimtazama Roika usoni.

Roika hakujibu chochote.

“Ahaa unajifanya bubu, sasa utaongea tu,” aliongea mmoja wao, huku akiiandaa  ngumi yake vizuri.

Roika alipigwa ngumi ya uso, ngumi iliyompa kizunguzungu, na kumfanya asisikie chochote kutokana na masikio yake yote kuziba kwa sekunde tano. Alitokwa na damu puani. Alihema huku akitetemeka.

“Unaitwa nani?” walimuuliza kwa mara nyingine.

Lakini bado Roika hakutaka kuwajibu. Mmoja wao akiwa anajianda kumpiga ngumi nyingine, sauti kutoka nyuma ilisikika.

“Kuna nini hapo?”

Mmoja wa wakubwa zao alikuwa anakuja lile eneo. Alipofika pale alishangaa kuona vijana wake, wakiwa wamemuweka mtu mmoja chini ya ulinzi.

“Kuna nini hapa, na huyu ni nani?” aliuliza mkubwa wao.

“Hatujui ni  nani. Wakati tumesimama hapa, tulimkuta akitoka chumba hiki. Inaonyesha ni mtu aliyekuja kutupeleleza.”

“Kutupeleleza? Mmemuuliza yeye ni nani?”

“Hakuna alichokiongea toka tulipomkamata.”

“Hebu ingia ndani kaangalie alikuwa anafanya nini.”

Mmoja wa watu wale aliingia ndani ya kile chumba, chumba alichokuwa ametoka Roika. Alipofika ndani, aliangalia kushoto na kulia na baadaye aliinua kichwa kutazama juu. Alishangaa kuona kijimlango cha kuingilia darini kikiwa wazi. Alirudi haraka nje na kumuita mkubwa wake akajionee.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*