googleAds

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

Ilipoishia jana

AKIWA amekaa katika wodi ya watoto,  daktari aliyekuwa akimfahamu Roika alikuwa akipita. Aliamua kumuita na kumuuliza kuhusu Roika. Kwa heshima zote za mtoto wa Rais, daktari alimsogelea Shazayi.

“Ni siku ya pili leo simuoni Mr Roika unaweza ukaniambia ni kwanini?” Shazayi aliuliza.

SASA ENDELEA

“Hata mimi sijui malikia wangu. Na si kawaida yake. Ni mtu ambaye anawapenda sana watoto. Lakini nashangaa hadi leo sijamuona hapa hospitalini sijui kaenda wapi.”

“Au amekwisharudi nchini kwao?” Shazayi aliuliza.

“Labda inaweza kuwa, lakini kirahisi hivyo. Mimi najua lazima angekuja kuwaona kwanza kabla hajaondoka.”

“Sasa atakuwa yuko wapi?”

“Sijui Malikia wangu.”

“Hivi unajua ni sehemu gani aliyokuwa akiishi?” Shazayi aliuliza.

“Aliniambia kuwa amefikia hoteli ya Alashak.”

“Ile hoteli iliyoko Nuruwan.”

“Ndio Malikia wangu.”

“Sawa nashukuru kwa kunifahamisha  nitakwenda kumtembelea nijue kama bado yuko Pakistani.”

Moyo wa Shazayi ulianza kupoa dhidi ya maumivu ya mapenzi, baada ya kuambiwa na daktari kuwa, Roika alikuwa amefikia hoteli ya Alashak iliyoko katika mji tulivu wa Nuruwan.

Alirudi nyumbani kwake kwanza, ambapo alipanga namna ya kutoka, kwa kuwa hakupenda kwenda huko pamoja na msafara wake wa ulinzi, alikuwa akifikiria ni namna gani atatoroka ili kwenda mji wa Nuruwan.

Ilipofika asubuhi ya saa 12, Shazayi alijivika mavazi ya kawaida akatokea drishani na kuelekea sehemu ya maegesho ya magari. Alifanya hivyo kwa uangalifu mkubwa ili asije kutwa na polisi wa usalama, polisi waliokuwa  sehemu zote ndani ya nyumba yake.

Alifanikiwa kutoka salama, bila kushtukiwa. Aliogopa sana, akiwaza endapo atakamatwa itakuwaje, maana itakuwa kesi kubwa mbele ya baba yake, baba yake anayemlinda mwanaye kuliko anavyojilinda yeye mwenyewe.

Kwa mwendo usio wa kawaida, aliendesha gari kuelekea Nuruwan. Polisi waliokuwa katika kizuizi, hawakulisimamisha gari, baada ya kuona ni gari lenye namba za serikali. Zaidi walimpigia saluti dereva aliyokuwa ndani, wasijue ni mtoto wa Rais wao. Wangemjua wasingemruhusu kupita.

Alifika hoteli ya Alashak saa tatu asubuhi. Ambapo alilipeleka gari hadi eneo la maegesho, ambako alikaa na kuwaza mambo kadhaa. Baadae alijifunga vizuri nikabu, akatoka kwenye gari na kulekea mapokezi. Hakuna mtu aliyejua kuwa yule ni mtoto wa Rais kutokana na kuwa alikuwa amejiziba uso.

Alipofika mapokezi, alimuuliza muhudumu wa hoteli.

“Samahani nahitaji kujua chumba anachoishi Mr Roika,” Shazayi aliuliza.

“Unafahamiana naye?” muhudumu aliuliza.

“Ndio ni rafiki yangu.”

“Sawa ngoja nimpigie simu.”

Muhudumu alipiga simu chumbani kwa Roika. Simu iliita muda mrefu bila kupokelewa.

“Nafikiri atakuwa ametoka, maana simu ya chumbani kwake haipokelewi,” aliongea muhudumu huyo, huku akiiushusha simu kutoka sikioni.”

Shazayi alizidi kuumia kupita kiasi, maana hotelini pia hakumuona. Alianza kuhisi kuwa huenda kuna jambo baya limemkuta Roika. Moyo wake unaompenda, uliomba jambo hilo lisiwe kweli. Alibaki amesimama pale mapokezi kama mtu aliyenyeshewa na mvua.

Wakati huo Ramona alikuwa akishuka kwenye lifti, akielekea eneo la maegesho ya magari. Muda huo ndio ulikuwa muda wake wa kuelekea katika jengo la kikundi cha kigaidi cha Swaba, ambako kuna mkutano na wafanya biashara wenzake. Alikuwa akitoka kwa unyonge wa hali ya juu ingawa alijikaza vilivyo ili watu wasijue.

Wakati akilekea kwenye gari, mhudumu alikuwa akimuona. Kwa kuwa aliwafamu Ramona na Roika ni marafiki, aliamua kumwambia Shazayi.

“Yule mwanamke anaelekea kwenye eneo la maegesho ya magari, anaitwa Ramona ni mrembo wa dunia. Yeye na Roika ni marafiki, unaweza ukamfuata na kumuuliza atakuwa anajua kama Roika yuko ndani au ametoka.”

Kwa shauku kubwa Shazayi alitoka pale mapokezi na kumfuata Ramona aliyekuwa akikaribia eneo la maegesho ya magari. Alijitahidi kumkimbilia na kumfikia kabla walinzi wake hawajamfungulia mlango.

Ramona alishtuka kuona mwanamke anamfuata pale kwenye gari, alisimama baada ya kuitwa.

“Habari, naitwa Shazayi,” aliongea Shazayi kwa lugha ya Kiingereza huku akimpa mkono Ramona.

Ramona hakummpa Shazayi mkono, alibaki kumtazama kwa sekunde 15 na baadae akasema.

“Naitwa Ramona nikusaidie nini?”

“Nahitaji kuonana na Roika sijui unaweza ukaniambia yuko wapi?” aliuliza Shazayi.

Macho yalimtoka Ramona alishtuka kisha akajikaza kuirudia hali yake ya mwanzo. Hakujua anayeongea naye ni mtoto wa Rais, lakini alipatwa na hofu kuona mwanamke huyo akimuulizia Roika, Roika mpenzi wake, ambaye kwa muda huo yuko chini ya ulinzi katika himaya ya kikundi cha kigaidi cha Swaba, chenye ushirikiano na wafanyabiashara wenzake. Kikundi kilichompa mtihani mkubwa, mtihani ambao hajawahi kukutana nao tokea azaliwe.

Alimtazama Shazayi kwa muda mrefu akilitafuta jibu la kumpa.

Nini kitafuatia usikose jumatatu


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*