googleAds

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

Ilipoishia jana

“Unazidi kuwa jeuri sio? Sasa leo ndio mwisho wa urafiki wetu na ndio mwanzo wa uadui wetu.”

Ramona alimsogelea Biyanah, akamtazama kwa huzuni kubwa huku akitokwa na machozi na kisha akamwambia.

SASA ENDELEA

“Biyanah rafiki yangu, kwanini tufikie huko. Kwanini tuingie katika vita kisa mwanamume? Hebu tuache ujinga. Kumbuka tulikotoka. Tumefanya mengi na watu wanatujua, tulipendana sana.

Leo unataka kuniua kisa Roika, tafadhali naomba usifikie huko rafiki yangu. Nakupenda sana. Mimi mwenyewe nimeshindwa kumuacha Roika nimejitahidi sana, lakini tayari Roika ameshakaa kwenye moyo wangu.

Mwanzo nilikubali kumuacha Roika, lakini Roika hakuwa tayari kuniacha mimi. Sasa kwanini nimtese Roika na kujitesa mwenyewe, kwa nini nimuache ihali kuwa wewe hakupendi. Siwezi kuzidhulumu nafsi mbili, nafsi ya Roika na yangu, Biyanah.”

“Sitaki kusikia ujinga wako Ramona. Kama unathamini urafiki wetu, muache Roika. Nilishaapa kuwa sitakuwa tayari kuona Roika anakwenda kwa mwanamke mwingine.

Sasa kazi ni kwako kunyoa au kusuka. Urafiki  wetu hautatenganishwa na kitu chochote, isipokuwa mapenzi ndio yatauvunja urafiki wetu na kuuleta uadui, mapenzi ya kumpenda Roika. Hujui ni jinsi gani nilivyopata tabu kumpata Roika.”

“Naona sasa umefika mbali. Unataka kuniua kisa Roika. Sasa nakwambiaje, hutoweza, mwanamke gani wewe usio muelewa. Mwanamume hakupendi bado unamng’ang’ania. Huo ni ujinga, ni ujinga kulazimisha mapenzi tena ni ukichaa, ukichaa sana. Usifikiri kuwa wewe ni tajiri, basi nitakuogopa, katu sikuogopi.

Huenda mimi nitakuwa wa kwanza kukuangamiza kabla hujainyanyua silaha yako,” aliongea Ramona kwa hasira baada ya kuona Biyanah amekuwa mbogo na hataki kuelewa.

Biyanah alimtazama Ramona kwa dakika mbili za ukimya, na kisha akasema.

“Sasa utanijua mimi ni nani.”

Aliposema hivyo, alifungua mlango na kutoka mle ndani akiwa na hasira za mbogo.

Ramona alikaa chini akiwa amechoka. Alilia sana, hakupenda kujenga uadui na rafiki yake, rafiki yake aliyetoka naye mbali. Lakini ilibidi naye ajivike roho ya ujasiri, kwa kuwa alikuwa na wakati mgumu mbele.

Sasa alikuwa akikabiliwa na kazi ya kumkwepa Biyanah na pia alikuwa na kazi ya kujiokoa yeye mwenyewe au kumuokoa Roika dhidi ya watu wake wa Biashara  ambao ni watu hatari.

Alitamani kesho isifike, kesho ambayo atakwenda kaamua hatima ya maisha yake na hatima ya mwanaume anayempenda. Alijuliza hivi kweli anaweza kumpiga risasi Roika. Nafsi yake ilikataa. Alijuliza tena hivi kweli anaweza kukubali kuwa anamfahamu Roika nafsi pia ilipingana naye.

Maana akikubali kuwa anamfahamu, watu hao watakuwa na maswali kuwa, kwanini Roika awapeleleze huenda watajua kuwa Ramona na Roika ni wapelelezi kutoka Marekani au ni wafanyakazi wa Umoja wa Matifa UN. Na huenda watachukua jukumu la kuwaua wote wawili.

Alianza kujuta kwanini alijiingiza kwenye mapenzi. Alimlaumu Roika kwanini aliyapeleleza masiha yake. Alimlaumu sana, ingawa Roika hakuwepo pale.

Alilala usiku huo bila kula, hakuhisi njaa ingawa alikuwa hajala tokea jana. Usiku huo, aliota ndoto za ajabu, ndoto ambazo hakuwahi kuziota tokea azaliwe.

SHAZAYI MTOTO WA RAIS

Shazayi alizidi kunyongwa na maumivu ya mapenzi kila baada ya sekunde. Hakika alijikuta ni mtumwa zaidi ya mtumwa mbele ya mwanamume kutoka Tanzania. Alijiuliza ni hisia gani alizonazo za kumpenda mwanamume siku mbili baada ya kukutana. Hakujielewa kabisa, mtoto huyu pekee wa Rais Gahil Halim.

Asubuhi aliondoka na msafara wake wa ulinzi na usalama, kwenda hospitali, kwenda kujaribu kuona kama atakutana na Roika. Alipofika hospitali, hakumuona tena Roika. Kichwa kilizidi kumuuma, alihisi moyo wake unakwenda kusimama muda si mrefu. Kitu pekee  Alichokuwa akihitaji mwanamke huyo ni busu kutoka kwa Roika ili aweze kuokoa maisha yake.

Akiwa amekaa katika wodi ya watoto, daktari aliyekuwa anamfahamu Roika alikuwa akipita. Aliamua kumuita na kumuuliza kuhusu Roika. Kwa heshima zote za mtoto wa Rais, daktari alimsogelea Shazayi.

“Ni siku ya pili leo simuoni Mr Roika unaweza ukaniambia ni kwa nini?” Shazayi aliuliza.

Nini kitafuatia? usikose kesho


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*