googleAds

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

Ilipoishia jana

BAADAYE mkutano uliahirishwa, ambapo ulipangwa kuendelea kesho. Wajumbe wote na viongozi wa vikundi vya kigaidi, walikwenda kupumzika makwao, wakiliacha jengo la Swaba kwenye ulinzi mkali. Huku Ramona naye, akirudi hotelini.

Alipofika hotelini, aliingia chumbani kwake na kilio kikubwa.

SASA ENDELEA

Alilia sana na kumlaumu Roika kwanini alimfuatilia katika mambo yake. Alianza kujuta kwanini alikutana na Roika na kwanini alimkubalia. Kujilaumu huko, kulikuwa ni jinsi atavyokwenda kumpoteza mtu anayempenda. Tayari Roika alikuwa amekwishamuingia vilivyo kwenye moyo wake, hivyo kujipeleka kwenye mikono ya kazi yake, ilikuwa imemuuma sana.

Ramona hakupenda kuipoteza kazi yake, kazi iliyokuwa ikimuingizia mamilioni ya pesa. Aliogopa pia kupoteza maisha yake. Aliwathamini sana wafanyabiashara wenzake na watu wa vikundi mbalimbali vya kigaidi, maana wao ndio waliomfanya atajirike siku hadi siku.

Sasa ilimbidi achague mambo mawili, kubaki na ule msimamo wake wa kwamba hamfahamu Roika au kukubali kuwa anamfahamu.

Endapo atasema hamfahamu, itamlazimu kushika bunduki na kumuua. Na kama atasema anamfahamu, basi anaweza kuleta madhara makubwa zaidi ikiwemo kumpoteza Roika na yeye mwenyewe kuingia katika ogomvi na wafanya biashara wenzake, ambao wanaweza kumuua. Maaana hawatakuwa tayari kuingia matatani kwa ajili ya mtu mmoja.

Kichwa kilianza kumuuma mrembo Ramona, alihisi uzito wa kichwa chake, umeuzidi uzito wa mwili. Hakujua atafanya nini. Juu ya kuokoa maisha ya mpenzi wake na pia kujiokoa yeye mwenyewe. Aliipenda kazi yake na pia alimpenda Roika. Aliogopa kuuawa na wafanya biashara wenzake, watu waliokuwa na roho ya ukatili.

Alizunguka mle chumbani kama chizi, hasira zilizoambatana na huzuni zilizidi kumtawala. Hapo mapenzi yalianza kushindana na kazi yake. Alijua akimuua Roika, kazi yake itakuwa salama na yeye pia atakuwa salama. Hataingia katika mgogoro dhidi ya watu wake, ambao ni watu hatari. Lakini endapo atakubali kuwa anamjua Roika, huenda atakufa yeye pamoja na Roika mwenyewe.

Akiwa katika mawazo hayo, mlango wake uligongwa, aliamua kutoa sauti tu ili kmujibu anayegonga mlango ya kwamba haitaji mtu yoyote kuingia kwake kwa muda huo. Lakini aliyekuwa mlangoni, hakutaka kuelewa, aliendalea kugonga.

Kwa hasira Biyanah, alielekea mlangoni ili kumkaripia aliyekuwa akibisha hodi, maana alikuwa hasikii. Alipofika mlangoni, hakufungua kwanza, alisema tena.

“Nimesema sihitaji mtu yoyote kwa wakati huu, wala sihitaji chakula, umenielewa?”

Lakini mlango ulizidi kugongwa. Kwa hasira aliufungua ili kumuona mshenzi aliyekuwa na kiburi, asiyetaka kuelewa.

Macho yake yaligongana na rafiki yake Biyanah.  Kwa huzuni na hasira hafifu, alijishusha, akamtazama rafiki yake na kumkaribisha kwa shingo upande.

“Karibu.”

Biyanah akionyesha kuwa hakuja kwa furaha, aliingia ndani bila kuongea chochote. Alipofika ndani, hakutaka kukaa. Alisimama huku  akitazama pembeni, asitake kumtazama Ramona.

“Karibu ukae,” aliongea Ramona kwa wasiwasi mkubwa.

Biyanah alimgeukia Ramona, akamtazama kwa dakika mbili za ukimya na kumuuliza swali.

“Hivi ni urafiki gani tulionao sisi? urafiki wa kutendeana dhuruma. Kwanini tuwe marafiki, wakati urafiki wetu unatenganishwa roho mbaya uliyonayo?”

“Sikuelewi Biyanah.”

“Acha ujinga, hunielewi kitu gani? Wewe ni mnafiki tena ni shetani. Hustahili kuwa rafiki yangu,” aliongea Biyanah kwa hasira kuu.

Alipomaliza kusema hivyo, Ramona alimfuata na kumpiga kibao. Biyanah aligeuka pembeni na kisha akamgeukia tena Ramona.

“Umenisaliti na bado unanipiga kibao. Unadhihilisha kuwa ulipanga kunichukulia Roika wangu.”

“Biyanah inatosha, sitaki kusikia maneno yako machafu. Kama Roika ni wako, kwanini sasa yuko kwangu. Wewe ni mwanamke msomi na mwenye akili, umeshindwa kujiuliza swali kama hilo na kujijibu wewe mwenyewe? Siku zote moyo wa binadamu, hususan mwanaume, ukimpenda mtu ni vigumu kuukatalia usipende. Roika ananipenda mimi na hakuhitaji wewe. Hata mimi nampenda, nampenda tena sana. kwanini ulazimishe mambo yasiyowezekana. Tafuta mtu mwingine Roika ni wa watu,” aliongea Ramona kwa hasira.

Maneno hayo yalimpa hasira zaidi Biyanah, naye alinyanyua mkono wake na kumpiga Ramona kibao.

“Hata ukinipiga, siwezi kumuacha Roika. Kwa sababu yeye ananipenda na mimi nampenda. Niko tayari urafiki wetu uvunjike. Maana sitakuwa tayari kuwa na rafiki anayelazimisha mambo,” aliongea Ramona huku akitokwa na machozi.

“Naona Ramona unacheza na mimi. Hunijui sio. Nadhani ni hakika hunijui. Nataka kuanzia sasa umuachea Roika la sivyo utamuacha wakati unaingia kaburini.”

“Kama ukitaka nimuache Roika wewe kwanza fanya kazi ya kumshawishi Roika aniache mimi na akupende wewe ndipo na mimi nitamuacha.”

“Unazidi kuwa jeuri sio? Sasa leo ndio mwisho wa urafiki wetu na ndio mwanzo wa uadui wetu.”

Ramona alimsogelea Biyanah, akamtazama kwa huzuni kubwa huku akitokwa na machozi na kisha akamwambia

Nini kitafuatia usikose kesho


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*