UONGOZE MOYO WANGU

Ilipoishia

Mtu huyo aligeuka taratibu na kumtazama Albat, macho ya Albat yaligongana na macho ya Leo Pordina, ana kwa ana.

Hiyo haikuwa ndoto tena bali lilikuwa ni tukio la kweli.

SASA ENDELEA…

Ukimya ulichukua nafasi ghafla, Albat alibaki amesimama kama picha ya ukutani huku akiwa ametoa macho mithili ya mjusi aliyekanyagwa.

Alianza kurudi nyuma taratibu, alilitetemeka kwa uwoga mkubwa, kwani macho yake hayakumdanganya, ni kweli Leo Pordina alikuwa amesimama mbele yake,akimtazama sana Albat.

“Hapana haiwezekani ni wewe Leo Pordina,” alitamka Albat kama mtu aliyechanganyikiwa.

Akiwa anarudi nyuma alijikuta anaanguka chini, wakati huo Leo Pordina hakusema lolote alibaki anamtazama Albat aliyekuwa akihangaika kama mtu anayetaka kufa.

Muonekano wa Leo Pordina hakuwa wa kawaida, nywele zake alizokuwa akipenda kuzifunga kwa nyuma hazikuwa zimefungwa tena, zilikuwa zimeachiwa kwa urefu hadi katikati ya mgongo. Gauni lake jeupe alilokuwa amelivaa pindi alipokuwa akiondoka uwanja wa ndege, gauni la ufupi  wa magotini, lilikuwa jeupe zaidi.

Leo Pordina hakuonyesha kutabasamu  zaidi alionyesha sura ya huzuni, akimtazama Albat aliyezidi kujawa na uwoga huku akihangaika.

“Leo Pordina si wewe haiwezekani, nasema haiwezekani,” alizidi kuongea huku akiogopa kukaribiana na Leo Pordina.

Ingawa alikuwa akitamani amuone Leo Pordina amepona kwenye ajali ya ndege, akitamani siku moja kumkumbatia lakini hapo aliogopa hata kumsogelea maana alikuwa amekuja katika hali isiyoeleweka, hii ilitokana na Albat kuhisi moyo wake uko katika hali ambayo hakuwahi kuihisi. Hali ya mle ndani pia ilikuwa imebadilika kwani kulikuwa na upepo mdogo uliokuwa ukisukuma baadhi ya vitu vidogo na kupeperusha mapazia.

Leo Pordina alinyoosha mkono akimtaka Albat amshike, Albat hakuwa tayari kufanya hivyo, maana akili yake ilikuwa ikiwaza kukimbia. Alishangaa kuona Leo Pordina anamuita na kuongea maneno aliyosema kwenye ndoto.

“Albat! mpenzi njoo nichukue.”

Albat hakuitika wala kujibu lolote kwani alikuwa katika hali ya kushangaa akimtazama Leo Pordina aliyekuwa umbali wa hatua tano tokea alipo yeye.

Lakini ghafla Leo Pordina alipotea, Albat alishtuka, mbele yake hakumuona tena, aliyafikicha macho yake huku akitazama huku na kule, moyo wake uliendelea kumdunda mithili ya ngoma inayopigwa huku akihema kama mbwa.

Hakujua ametoweka vipi wakati muda wote alikuwa amemkazia macho, upesi aliinuka na kwenda chumbani, ambako nako hakumuona, alirudi tena sebuleni pia hakumuona. Alikaa kwenye kochi asielewe lolote lile.

Hakika alionekana kuchanganyikiwa, jambo hilo aliliona kama ni ndoto lakini haikuwa ndoto bali ni kweli, alijiona yeye katika hali halisi. Yeye mwenyewe aliyelishuhudia tukio hilo, hakuliamini kama limetokea.

Alianza kuogopa kuliko siku zote, kwani akili yake ilianza kuamini kuwa Leo Pordina alikuwa kiumbe wa kutoka katika ulimwengu mwingine, yaani jini.

Ingawa pia yule mganga wa kule Unulu alikuwa amemwambia zaidi ya mara moja kuwa Leo Pordina hakuwa mzimu, lakini alimuona muongo na kusema alikuwa ni mzimu.

Alijiuliza Leo Pordina ametoka vipi nchini Syria amekujaje kujaje, je, alikuwa akiishi au alikuwa ni mzima, kama anaishi kwanini amtokea katika mazingira yale, mazingira yaliokuwa si ya kawaida, huku muonekano wake Leo Pordina ukiwa si wa kawaida tofauti na alivyomzoea pindi walipokuwa wote Afrika Kusini.

Taarifa ya duniani kote, iliyohusu ajali ya ndege ya abiria 144 kati ya abiria 150 kupoteza maisha, ndio iliyolifanya tukio hilo kuwa tukio la ajabu machoni mwa Albat, kwani hata abiria hao sita walipoteza maisha wakiwa hospitalini baada ya hospitali waliohifadhiwa kulipuliwa na bomu.

Hivyo hata Albat alikuwa akiamini Leo Pordina alikuwa amekwisha kufa, ingawa mwanzo hakutaka kabisa kuamini hivyo ila taarifa ya kushambuliwa hospitali kwa bomu la masafa mafupi, kulimfanya akate tamaa na kuamini msichana huyo anayempenda naye alikuwa amepoteza maisha.

Baadaye alipata wazo la kumtafuta mganga mwingine ili apate kumtatulia tatizo lake, mganga atakayemueleza kwa kina kuhusu tukio hilo la kimiujiza. Ingawa mganga aliyekuwa amemuuleza hapo mwanzo, alikuwa ni chifu anayeheshimika nusu nzima ya Afrika Kusini, lakini alitaka kusikia maneno ya machifu wengine.

Alisafiri hadi mji wa Litavuba uliokuwa nje ya Jiji la Pretoria  hiyo ilikuwa ni baada ya kumuuliza rafiki yake mwingine aitwaye Kashe ambaye hakuwa mwanafunzi wa chuo, aliyekuwa raia wa nchi hiyo, kuhusu mahali wanakopatika machifu wakubwa wa kiganga.

Alipofika Litavuba alikutana na chifu mwingine wa kabila la Kizulu, alimueleza matatizo yake, lakini mganga huyo naye alizidi kumpa mashaka zaidi Albat.

“Kijana suala lako ni hatari hivyo siwezi kukuuleza chochote,” aliongea chifu huyo.

“Kwa nini chifu mbona sioni kama kuna hatari yoyote hebu nisaidie chifu,” alijibu Albat kwa huzuni kuu.

“Nimesema siwezi kuingilia mambo yalio nje ya uwezo wangu, hivyo ni lazima unielewe kijana,” alijibu chifu huyo kwa ukali.

Albat aliamua kusimama akiwa amechukia, akiwa anataka kutoka mganga alimwambia.

“Hakuna atakayeweza kukueleza tatizo lako na wala kulitatua, chifu yoyote yule si waganga wa dunia nzima.”

Albat aliondoka kwa chifu huyo kwa huzuni akizidi kuwa katika hali mbaya ya kimawazo, akiwa anaendesha gari, alijiuliza uhatari wa jambo hili ulikuwa uko wapi, kwa nini machifu walikuwa wakiliogopa, lilikuwa na nini.

Baadaye aliona hana budi kumueleza rafiki yake mkubwa Mwita Mtanzania mwenzake, ingawa alijua ni vibaya kusema jambo hilo kwani  hapo mwanzo marafiki zake walimchukulia kuwa alikuwa amepatwa na tatizo la kiakili au ameathirika kisaikolojia.

Alipanga kukaa vizuri na Mwita na kumueleza kwa kina huenda angemuelewa ili apate namna ya kumsaidia. Alipofika Zululand, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Mwita, Mwita alimkaribisha vizuri ingawa alimuomba Albat msamaha kwa kutoenda kwake tokea majuzi.

“Usijali besti,” alijibu Albat.

“Sawa naona umekuja nipe habari,” aliongea Mwita.

“Mwita kwa sasa sina haja ya kusita kuongea chochote mbele yako naomba unisikie na unielewe lile nitakalo kwambia, naomba usije kunichukulia kuwa nimechanganyikiwa, wewe ni msomi hebu tafakari,” aliongea Albat.

“Sawa usijali wewe nambie tu

Albat alishusha pumzi na kumwambia.

“Leo Pordina amenitokea jana.”

Mwita alishtuka alimtazama Albat kisha akamuuliza.

“Kivipi?”

“Jana nimemuona Leo Pordina, tumekutana uso kwa uso kasimama kabisa mbele yangu.”

“Albat hebu kuwa siriazi.”

“Mwita unataka niwe siriazi kiasi gani au hadi niingie kwenye kichwa chako ndio utajua nakueleza ukweli?” aliuliza Albat kwa hasira kidogo.

“Amekutokea kivipi wakati hakuna taarifa yoyote ya kurudi kwake, kila mmoja anajua Leo Pordina amekwisha kufa na hata kama hakufa hawezi kutoka nchini Syria salama, sasa iweje useme umemuona nyumbani kwako?”

“Niamini mimi Mwita nachokwambia ni cha kweli. Siku ile mlivyoondoka tu kitabu kilirudi chumbani na aliyekirudisha ni Leo Pordina mwenyewe.”

“Ulimuona vipi wakati akikirudisha?”

“Nilitegesha kamera na nilipoitazama video nilimuona.”

“Mmmh! Albat wewe sio mzima hebu wewe mwenyewe jiulize inawezekana vipi, mtu akaja kurudisha kitabu kilichofichwa, kwanza katokea wapi milango si huwa unafunga. Mimi nahisi kabisa Albat wewe una matatizo, kama sio ya kisaikolojia basi ya kiakili. Mimi kama rafiki yako nakuomba twende kwa daktari sasa hivi,” aliongea Mwita maneno yaliomkasirisha Albat.

Aliamua kusimama kwenye kiti na kuanza kuondoka, alipofika mlangoni alisimama na kumgeukia Mwita huku machozi mengi yakiwa yanamtoka.

“Sawa haina shida niache na uwendawazimu wangu. Kama umeshindwa kunisikiliza na kunielewa, sina haja ya kukupigia gitaa, wakati ushakuwa mbuzi. Sitarudi tena kukueleza lolote linalohusu maisha yangu na ukiwapigia simu nyumbani kuwaeleza kuwa mimi nimechanganyikiwa basi usije ukaniita tena rafiki yako,” aliongea Albart akibubujikwa na machozi mengi.

Maneno hayo yalimuumiza Mwita, alipotaka kuongea kitu, Albat alifungua mlango na kutoka.

“Albat!” aliita Mwita.

Alimfauta hadi nje na kukuta tayari ashaingia kwenye gari, alipomkimbilia Albat alikanyaga mafuta na kuondoa gari kwa kasi.

Alirudi hadi nyumbani na kukaa chini ya mlango alilia kama mtoto, huzuni ilimtawala Mtanzania huyu kiasi cha kujiona amepatwa na laana. Alifungua friji na kutoa pombe kali na kuzinywa zote, alilala usiku kucha akiwa na pombe nyingi kichwani.

Hata aliposhtuka asubuhi alimuona mtu kama Leo Pordina akiwa amemsimamia mbele yake, kutokana na pombe kali macho yake hayakuweza kuona vema. Aliogopa na kwenda kujificha kwenye kiti kilichokuwa karibu na kona.

“Niache niache usije kunisogelea,” aliongea akiwa bado amelewa.

Nini kitafuatia? usikose kesho

Previous Article
Next Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*