googleAds

UONGOZE MOYO WANGU (GUIDE MY HEART) 42

Na Eman Fisima

Ilipoishia

Muda mfupi baadaye, wakiwa ndani ya ndege, ndege ya Shirika Kuu la Uturuki iliruka kuianza safari ya kuelekea nchini Uturuki.

SASA ENDELEA

ULIKUWA ni mwendo wa saa 40 kutoka Berlin, Ujerumani hadi Raizopor nchini Uturuki. Ndege ya shirika kuu la Uturuki, ilitua uwanja wa kimataifa wa Turkey Balon saa nne asubuhi.

Albat pamoja na watu watatu walishuka kwenye ndege hiyo na kutoka kabisa nje ya uwanja, walichukua usafiri wa tax uliowapeleka hadi Hoteli ya Nasaporo.

Hoteli hiyo ilikuwa Mashariki mwa Jiji la Raizopor. Albat na waandishi hao watatu walichukua vyumba tofauti vya kulala. Baadaye kidogo wote walikutana muda wa chakula katika eneo la mgahawa. Walikaa kula chakula na kuongea mambo kadhaa.

Walikuwa wakizungumzia safari yao mpya ya kuelekea mji wa Galanir mji uliokuwa Mashariki kabisa mwa Uturuki mpakani mwa Syria. Wote pale walikuwa wakijua kuwa Albat alikuwa mwandishi halali wa shirika hilo.

Wakati Bwana Lenardo akimtafutia Albat kitambulisho cha uandishi wa habari wa shirika lao, alikuwa amezungumza na watu wakubwa wa shirika la DW kule Berlin. Hivyo wao ndio waliokuwa wakijua kuwa Albat hakuwa mwandishi wa habari.

Waandishi hao watatu wakiwemo wasichana wawili na mwanamume mmoja, wote wakiwa ni raia wa Ujerumani, walijua Albat alikuwa ripota wa habari ambaye alitokea barani Afrika na kuja kujumuika nao kwenda katika kambi ya shirika la umoja wa mataifa, la msaada wa chakula lililokuwa Galanir.

Wakiwa wamekaa pale wakipata chakula, huku maongezi mengine yakiendelea, Albat aliwaambia.

“Mimi nataka kuelekea Hajan Saik nchini Syria.”

Aliposema hivyo walimshangaa, mwandishi aitwae Angelina aliuliza.

“Umepewa kazi ya kwenda huko?”

“Ndio mimi niliomba kuingia mji wa Hajan Saik kama ripota wa uchunguzi wa hali ya maisha ya raia wachache waliobaki katika maeneo yote, kuanzia hapo hadi mwanzoni mwa mji mkuu Damascus,” alijibu Albat.

“Mmh! Mbona binafsi sikusikia pale ofisini kama kuna kumpeleka mwandishi yeyote eneo hilo?” aliuliza mwandishi aitwe Kevin mtu aliyekuwa sehemu ya kamera pia.

“Kiongozi hakutaka kuiweka wazi safari yangu,” alijibu Albat.

“Unajua eneo la Hajan Saik ni eneo lisilo na  utulivu ingawa kuna raia bado wanaishi, ndege za Serikali huwa zinaangusha mabomu baadhi ya siku ili kuwasambaratisha waasi. Eneo hilo ni hatari hata kwa sisi waandishi kwa sababu hiyo. Sasa nashangaa wewe kupewa ruhusa ya kwenda huko,” aliongea Angelina.

“Halafu kuna haja gani ya kwenda huko wakati mwandishi wetu aliyepo mji mkuu wa Damascus anaripoti na taarifa za Hajan Saik pia?” aliuliza mwandishi aitwae Ruce.

Maswali hayo yalizidi kumtesa Albat kwani hakutaka wenzake wajue kuwa safari yake hiiyo ilikuwa si kwa ajili ya uandishi wa habari bali kwa ajili ya kumtafuta mtu muhimu.

Waandishi hao wakati wanapewa taarifa kuhusu Albat waliambiwa kuwa ni mwandishi kutoka Afrika ambaye atajumuika nao katika safari ya kuelekea kambi ya Umoja wa mataifa ya msaada wa chakula. Lakini walishangaa kuona anawaambia kuwa ataingia katika mji wa Hajan Saik.

“Kwa hiyo utakwenda na magari ya msaada?” aliuliza Angelina.

“Ndio nimeambiwa hivyo,” alijibu Albat.

“Lakini umoja wa mataifa wana waandishi wao wa habari ambao hutembea na magari ya chakula, wakirudi pale mpakani hutupatia sisi habari.”

“Ndio hivyo jamani lazima niende.”

“Sawa hatuna kipingamizi kama ofisini wamekupa kazi hiyo, sisi hatuna la kusema,” alijibu Angelina.

Baada ya maongezi hayo na kumaliza chakula kila mmoja alielekea chumbani kwake.

Ilikuwa inatimia siku ya pili na saa kadhaa, Albat hakuwa ametokewa na Leo Pordina, hakuwa ameota ndoto wala kuoneshwa ishara fulani ya kimuujiza, hali hiyo ilianza kumshtua.

Akiwa chumbani alikuwa akijiuliza jambo hilo, kwani ilikuwa si kawaida kuona ukimya huo. Kawaida ilikuwa kama Leo Pordina hatamtokea Albat mbele ya macho yake basi alikuwa akiota ndoto yoyote kuhusu Leo Pordina. Na kama hivyo pia havitakuwepo, basi kitabu cha Leo Pordina huonyesha ishara ya kuhama endapo kitahamishwa.

Lakini suala la kitabu hakujua kuwa kama kinahama kwa wakati huo au hakihami kwa kuwa alikuwa akilala nacho kitandani.

Baadaye aliamua kuliacha suala hilo na kusema kuwa huenda hali hiyo itajitokeza usiku wa kumkia kesho au wakati wowote ule.

Kesho ilipofika wote waliianza safari ya kuelekea mji wa Galanir. Toyota hilux, gari ya shirika la DW ndiyo iliyokuja kuwachukua. Wakati huo ilikuwa ni saa tano asubuhi, jua likiwa na nguvu hafifu sana ya kuangaza kutokana na hali ya baridi.

Mawazo ya kutotokewa na Leo Pordina yalikuwa kichwani mwa Albat si tu alikuwa akihofu ukimya huo, pia alikuwa amemkumbuka sana kwani alikuwa akipenda kumuona ingawa alikuwa mwoga.

Saa zilivyozidi kusogea ndivyo walivyokuwa wakiutafuta mji wa Galanir, mji uliokuwa mpakani wa Uturuki na Syria. Baada ya saa tisa waliingia katika mji huo, ikiwa ni saa tatu usiku.

Walipelekwa moja kwa moja hotelini. Usiku huo, Albat akiwa chumbani kwake, alifanya zoezi moja la  majaribio. Kutokana na kutotokewa na Leo Pordina katika hali ya kawaida, wala ndotoni, aliamua kukichukua kitabu na kwenda kukiweka karibu na meza ya runinga. Lengo likiwa ni kutaka kujua kama kitarudi kitandani yaani Leo Pordina atakirudisha karibu yake ama la.

Baada ya kukiweka hapo alipanda kitandani na kulala. Asubuhi ilipofika, alishtuka kutoka usingizini, alipotazama kitandani hakukiona kitabu, upesi alishuka kitandani na kuelekea kwenye meza ya runinga ambapo alikiona pale pale.

Hofu ilimjia, alijiuliza nini maana ya jambo lile, kwa kuwa haijawahi kutokea kitabu kile kisirudi endepo kitahamishwa kutoka kitandani.

Ina mana kuwa Leo Pordina hakuwa tena karibu yake? Hivyo ndivyo alivyojiuliza.

Alianza kuogopa sana kwani aliyakumbuka maneno ya mchungaji Thomas Shurreh, kuwa endapo ataona Leo Pordina hamtokei tena ajue kuwa huenda amekwisha kufa.

Kwani alisema kuwa, Leo Pordina kumtokea ilikuwa ni ishara ya kuwa  msichana huyo alikuwa bado akiishi katika dunia hii. Kumbukumbu hizo ndizo zilizomtesa Albat, alianza kuhisi huenda kweli Leo Pordina alikuwa amekwishakufa kweli.

Maana ilikuwa si kawaida kuona ukimya huo usio na ishara yoyote. Alianza kuhisi kuwa safari yake ilikuwa haina maana kwani lengo la safari hiyo, lilikuwa ni kwenda kuhakikisha kama Leo Pordina anaishi katika dunia hii ama alikufa katika ajali ya ndege au vita inayoendelea Syria.

Asubuhi hiyo alitokwa na machozi, akimwomba Leo Pordina msamaha endapo atakuwa amechangia kifo chake kwa kuchelewa kufika. Akiwa katika majonzi hayo, wenzake walimjulisha kwa ujumbe wa simu kuwa wanamsubiri yeye kwa ajili ya kuendelea na safari.

Alijiandaa na kushuka hadi chini ambapo aliwakuta mgahawani wakipata chakula, naye alipata kifungua kinywa kwa kujilazimisha. Wenzake walianza kumwona hayuko katika hali ya kawaida.

Baada ya chakula waliingia kwenye gari kwa ajili ya kuelekea kambi ya umoja wa mataifa iliyokuwa karibu kabisa na mpaka wa Syria. Njiani Albat hakuwa sawa kabisa alijitahidi kujikaza asigundulike kuwa alikuwa na mawazo lakini alishindwa, hofu, majonzi na wasiwasi wake, vilishindwa kujificha.

“Uko sawa kweli?” aliuliza Angelina.

“Niko sawa tu,” alijibu Albat kwa tabasamu la uongo.

Baada ya saa mbili walikuwa wakifika katika kambi hiyo ya umoja wa mataifa, kambi iliyokuwa ikisambaza chakula katika miji mbalimbali nchini Syria.

Walipokewa vizuri na viongozi wa eneo hilo wa umoja wa mataifa. Siku ya pili Angelina na wenzake walianza kuripoti habari kutokea katika kambi hiyo, iliyokuwa ikiwasaidia sana raia wa Syria waliobaki katika maeneo mbalimbali nchini mwao.

Wakati huo moyo wa kukata tamaa wa Albat ulianza kumtafuna. Alianza kuogopa kuingia katika mji wa Hajan Saik maana tayari alishakuwa ameanza kuona dalili za kutofanikiwa. Hii ilitokana na kutotokewa na Leo Pordina kwa siku tatu kwenda nne.

Alianza kujishauri aingie katika mji huo au asingie maana alihisi kabisa kuwa Leo Pordina tayari alishakuwa amekufa.

Nini kitafutia, usikose kesho.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*