googleAds

UONGOZE MOYO WANGU (50)

NA EMAN FISIMA, +255 654 076 265

Ilipoishia

Wakati Albat na Shania wakiongozwa na wapigaji kuelekea kwenye vyumba vyao, Albat alimuona mwanamke mmoja aliyekuwa ameketi karibu na kompyuta. Mwanamke huyo alikuwa amevaa nguo nyeusi hijabu na nikabu, yalionekana macho yake tu.

SASA ENDELEA

Mwanamke huyo alikuwa makini kwenye kompyuta akiandika vitu fulani. Albat alimtazama na kumpita akiwa amemshika Shania mkono.

Alishangaa kwa sababu ndani ya ngome hiyo hakumuona mwanamke mwingine zaidi ya huyo. Wapiganaji hao walimuongoza hadi kwenye chumba alichotakiwa kuhifadhiwa. Baadaye aliletewa chakula ambacho alikila yeye na Shania, walikula kwa haraka maana kila mtu alikuwa na njaa sana.

Baadaye Albat alianza kuandaa vifaa vyake vya uandishi wa habari, wakati akifanya hivyo alimkumbuka baba yake na Leo Pordina, bwana Lenardo aliyekuwa amemfundisha namna ya kuandika habari na kuzirusha kwenye ofisi za DW Ujerumani kwa kifaa maalumu cha intaneti.

Anakumbuka alimwambia kuwa licha ya kujifanya mwandishi wa habari, alitakiwa kujifunza kabisa kazi hiyo ili iweze kumlinda akiwa Syria.  Japo chuoni hakusomea masuala ya uandishi wa habari, lakini alitakiwa aonekane anaiweza kazi hiyo ili kikundi kama Alkujar endapo kitakuwa kimemtia mikononi mwao aweze kukifanyia kazi.

Baada ya kuandaa aliunganisha kamera ndogo na kompyuta, akakiweka kifaa maalumu cha intaneti chenye uwezo mkubwa wa kusoma mtandao. Aliingia kwenye tovuti ya DW ya wafanyakazi. Alianza kujirekodi yeye akizungumza.

“Nipo kwenye ngome ya waasi wa Alkujar naomba ushirikiano wenu, baadaye nitakuwa na kiongozi wao bwana Hussein katika mahojiano maalumu.”

Video hiyo aliyokuwa amejirekodi, aliituma moja kwa moja. Makao makuu ya DW Ujerumani, walipoipata video hiyo, hawakuamini, hakika walishangaa kwa sababu hakukuwa na mwandishi wao yoyote aliyekwenda katika mji wa Hajan Saik zaidi ya waandishi wao watatu waliokuwa mpakani mwa Uturuki na Syria. Walijiuliza ni mwandishi wao yupi aliyekwenda huko.

Mwaka mmoja uliopita waandishi wawili waliuawa na kundi hilo wakihisiwa kuwa ni wapelelezi wa serikali ya Marekani, hivyo vyombo vya habari havikutaka kupeleka mwandishi yeyote huko.

Waliipokea video ya Albat na kumtumia  ujumbe wa kufurahishwa na kazi yake walimshukuru na kumuahidi kumpa ushirikiano.

Albat alijua kuwa endapo atawafanyia kazi nzuri ya kuandika habari zao kikundi hicho cha waasi basi wapiganaji hao watamuacha huru ili akaendelee na kazi yake iliyomleta Syria ya kumtafuta msichana wa moyo wake, Leo Pordina.

Baadaye Albat alitoka nje ya kile chumba na kukutana na mmoja ya wapiganaji. Alimuomba mpiganaji huyo kumpa taarifa ya maandishi kuhusu mikakati yao na maelezo mengine ambayo walihitaji dunia ijue pamoja serikali ya Syria.

Mpiganaji huyo aliwasiliana na kiongozi Hussein ambaye alimwambia aende kwa mwanamke aliyekuwa ameketi kwenye kompyuta ili akapate maelezo ya kuanza nayo ya maandishi.

Albat alikwenda hadi kwa yule mwanamke aliyekuwa amemuona mwanzo aliyekuwa akionekana ni mtu muhimu kwenye kundi hilo, huku akisindikizwa na mpiganaji aliyekuwa na bunduki. Alipofika pale alisimama kando yake na kumsalimia mwanamke huyo kwa lugha ya Kiingereza.

“Habari yako.”

Mwanamke huyo alinyanyua sura yake na kumtazama Albat, ghafla alishtuka hadi kikombe cha kahawa kilichokuwa juu ya meza yake kilidondoka chini na kupasuka.

Albat na yule mpiganaji walimshangaa,

“Samahani kwa kukushtua bila shaka ulikuwa mbali kimawazo?” aliuliza Albat.

Lakini yule mwanamke aliendelea kumtazama Albat, macho yakiwa yamemtoka vilivyo, ilionyesha kuwa alikuwa ameshtushwa sana na kumuona Albat, haikujulikana ni kwa sababu gani.

Baada ya kuona mpiganaji aliyekuwa pembeni  yao naye akianza kuonyesha mashaka, mwanamke huyo alijipoteza na kurudi haraka kwenye hali yake ya kawaida.

“Ohoo! Ni kweli umenishtua, maana ghafla tu nimekuta umesimama mbele yangu, nilikuwa kwenye dimbwi la mawazo na kazi yangu,” aliongea mwanamke huyo akijichekesha na kujipoteza kabisa na mwonekano wa mwanzo.

“Samahani sikudhani kama ningekushtua kiasi hicho,” alijibu Albat.

“Usijali ehee nambie unashida gani?”

“Nahitaji maelezo ambayo Hussein anahitaji yatolewe kwenye habari,” aliongea Albat.

Yule mwanamke alichapisha maandishi yaliyokuwa kwenye faili la  kompyuta yake na kumpa Albat karatasi mbili za maelezo.

“Asante nakutakia mchana mwema,” aliongea Albat.

Mwanamke huyo alijibu kwa kutikisa kichwa, Albat aliondoka pale huku akisindikizwa na mpiganaji. Mpiganaji aliishia nje Albat aliingia ndani na kuanza kusoma maandishi hayo mbele ya kamera.

Ilipotimu saa mbili usiku, mlango wake uligongwa, alikwenda kufungua, alikuwa ni yule mwanamke. Sura yake ikiwa ndani ya nikabu, macho pekee ndiyo yaliyoonekana.

“Samahani wakati nakula nimeagizwa nikuletee na wewe chakula,” aliongea mwanamke huyo kwa sauti ya kujilazimisha.

“Asante sana! Karibu ingia ndani,” alijibu Albat.

Nini kitafuatia? Usikose kesho. 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*