googleAds

UONGOZE MOYO WANGU (47)

Na Eman Fisima 

Ilipoishia

Maelezo ya msichana raia wa Syria, Shania yalithibitisha kuwa Leo Pordina hakuwa ameondoka na boti za wakimbizi endapo kama alikuwa amepona kwenye ajali ya ndege.

 Hali hiyo ilizidi kumuweka Albat katika wakati mgumu, moyo wake ulishaanza kusinyaa, akili yake ilishasimama kwanza. Hakujua kama Leo Pordina alikuwa amezikwa pale kwenye kaburi la abiria wote au alikuwa amepona na kuondoka mji huo kwa njia yoyote ile au alishakufa kwa risasi.

SASA ENDELEA…

Usiku mkubwa uliingia, msichana Shania alikuwa wa kwanza kupitiwa na usingizi, alilala akimuacha Albat akiwa macho.

Albat alitoa simu yake kwenye begi na kuanza kuangalia picha za Leo Pordina, msichana mzuri ambaye hakuwa ameona wa kulingana naye. Alitamani amuone kwa mara nyingine. Kwa sababu kwa muda wa mwaka mmoja waliokuwa wakisoma chuo kimoja, yeye aliuona kama amekuwa karibu naye kwa siku mbili tu.

Aliikumbuka ile siku aliyomtamkia kuwa anampenda, ilikuwa ni siku nzuri sana kwenye maisha yake ingawa hakupewa jibu la kukubaliwa. Leo Pordina mara baada ya kumaliza mwaka mmoja wa masomo ndani ya chuo cha Zululand, alitakiwa kurudi katika chuo chake cha Maxfuture cha nchini kwake Ujerumani.

Alikuwa amemuahidi Albat kuwa atampa jibu atakapofika Ujerumani. Albat hakujua kwanini Leo Pordina alikuwa amemwambia hivyo.

Lakini mara baada ya kuachana uwanja wa ndege, mawasiliano yao yalikatika baada ya ndege aliyokuwa akisafiria Leo Pordina, kupata ajali. Ndege hiyo ya shirika la Kijerumani ilidondokea pwani ya Midian nchini Syria.

Wanafamilia na ndugu wa kutoka Afrika Kusini na Ujerumani, waliokuwa na ndugu zao kwenye ndege hiyo, walishakuwa wamezika nguo za ndugu zao, wakiamini kuwa ndugu zao walikwisha kufa.

Lakini mtu mmoja pekee msichana Leo Pordina alimtokea Albat na kumwambia yeye bado anaishi.

Hayo yote aliyakumbuka Albat akiwa ndani ya kijumba kilichokuwa pwani ya Midian katika mji wa Hajan Saik nchini Syria. Simu yake ilikuwa na chaji ila mtandao haukuweza kusoma, kwani katika nchi hiyo hakukuwa na mawasiliano ya simu kutokana na vita.

Alimtazama msichana Shania aliyekuwa usingizini na kumuona kama mwongozo wake wa kumtafuta Leo Pordina ingawa alishakuwa ameanza kukata tamaa.

Moyoni alijisemea.

“Binti mzuri kama huyu, mtoto anayetakiwa kuwa shule sasa anahangaika hajui ni lini tena atarudi kusoma, eeh! Mungu mnusuru.”

Alimwonea sana huruma, akimwona kama mdogo wake wa tumbo moja. Baadaye kidogo naye usingizi ulianza kumvuta, alitamani sana usiku huo aote ndoto yoyote yenye kumwonesha Leo Pordina au Leo Pordina amtokee.

Lakini alikuja kushtuka asubuhi ya saa 12 jua likiwa linachomoza kutokea usawa wa bahari. Mara baada ya kufumbua macho, hakumwona Shania pale alipokuwa amelala, alishtuka na kutoka nje upesi huku akimuita.

Alimkuta nje akiwa amekaa kwenye msingi akitazama baharini, alisomgelea na kumkuta akitokwa na machozi.

“Nini tena Shania?” aliuliza Albat.

Shania aliendelea kulia bila kujibu lolote, Albat alimsogelea, akachuchumaa na kumuuliza tena.

“Nini tatizo mdogo wangu, mbona unalia?”

“Lazima nilie nisipolia sitakuwa nimeridhika, siamini kama leo hii mimi nabaki duniani mwenyewe, mama yangu amekufa, baba yangu amekufa, kaka yangu amekufa. Mdogo wangu ndio hivyo sielewi kama amefika salama Ujerumani. Hii yote inatokea kwa sababu ya watu wachache wenye kujali masilahi yao binafsi,” alijibu Shania akilia sana.

Albat alimkumbatia pasipo kumwambia lolote maana ni kweli jambo hilo liliumiza. Baadaye alimwambia.

“Usijali kuhusu mdogo wako naamini ipo siku utamwona.”

Baadaye alimsihi akaoge baharini ili waondoke mahali pale. Shania alikwenda kuoga baharini, Albat naye alioga mara baada ya Shania kutoka. Walijiandaa na kuondoka katika kijumba kile.

Walishika njia inayoingia katikati ya mji, Shania alikuwa akiogopa lakini Albat alimwambia kuwa asiogope, maana iliwalazimu kufika huko.

Wakiwa wanakaribia katika majengo fulani, ghafla magari saba aina ya Toyota Hilux yenye uwazi nyuma yalitokea mbele yao. Magari hayo yalikuwa yamewapakia watu waliovaa mavazi meusi wakiwa na bendera nyeusi zilizokuwa na maandishi ya Kiarabu.

Walikuwa ni wapiganaji wa Alkujar. Albat alishtuka, alitamani kukimbia lakini hakuona pa kukimbilia. Alisimama kando ya barabara, akiwa amemshika mkono Shania. Shania alijawa na woga mkubwa alijishika kwa Albat vizuri.

Mpiganaji wa mbele alinyanyua mkono akitoa ishara ya kusimamisha magari ya nyuma. Magari yalisimama katikati ya barabara, kando ya Albat. Wananchi wachache waliokuwa mitaani walikimbilia ndani mwao.

Wapiganaji hao waliokuwa juu ya magari, baadhi yao wakiwa wamejifunika nyuso zao, wote walimtazama Albat. Mmoja alimnyooshea kidole Albat na kumuita.

“Wewe kuja hapa!” aliongea kwa lugha ya Kiarabu.

Shania alijificha nyuma ya Albat akitetemeka sana. Albat alijivika ujasiri wa uongo na kusogea hadi pale.

“Wewe nani?” aliuliza mpiganaji huyo.

Albat hakuelewa ameulizwa nini ilibidi aulize kwa lugha ya Kiingereza.

“Tunaweza kuongea Kiingereza?”

Mpiganaji yule alimuita mpiganaji mwenzake, alishuka kwenye gari na kumsogelea Albat, alimtazama na Shania aliyekuwa nyuma ya Albat na kuuliza kwa Kiingereza.

“Wewe ni nani?”

“Naitwa Albat ni mwandishi wa habari?”

“Unatokea wapi?”

“Ujerumani?”

“Nyinyi ndio mnasababisha raia wetu wakakimbilia huko?”

“Hapana mimi ni mwandishi tu.”

“Hapana bila shaka wewe ni Mmarekani.”

“Ni Mwafrika natokea DW Ujerumani, lengo la kufika hapa ni kwa ajili ya kuandika habari yoyote kuhusu ajali ya ndege. Pia kutangaza habari zenu namna mlivyo na nguvu ya kijeshi.”

Albat aliposema hivyo, mpiganaji huyo alimsogelea mwenzake na kumwambia mambo yote aliyokuwa akizungumza na Albat. Baada ya kuongea na mwenzake, alimrudia Albat na kumwambia.

“Kesho tukutane tena hapa maana uko kwenye himaya yetu. Ila kama umetudanganya tutakupa adhabu ya mwili kutengana na kichwa chako. Na huyu binti ni nani?”

“Nilimkuta tu mahali akiwa mpweke nikampa chakula,” alijibu Albat.

Baada ya kujibiwa hivyo, mpiganaji huyo aliingia kwenye gari. Ishara ya kuondoka ikaoneshwa, magari yote yalipita kando ya Albat huku wakipiganaji wote wakimtazama. Yalizamia kwenye kona moja ya jengo na kuondoka kabisa eneo lile.

Albat alishusha pumzi moyo wa woga ukapungua kudunda. Alimtazama Shania na kumwambia.

“Twende!”

Waliendelea na safari ya kusogea katikati ya mji. Njiani walikuwa wakiwauliza watu wachache waliokuwa barabarani kuhusu msichana Leo Pordina. Albat alikuwa akitoa simu yake na kuwaonesha watu picha ya Leo Pordina.

Lakini matumaini ya kupata habari yoyote, yalizidi kupotea, hakukuwa na hata mtu mmoja aliyeeleza habari ya matumaini. Wengi walisema kuwa wanafahamu kuwa watu wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo walikufa na kuzikwa kwenye kaburi la pamoja.

Siku hiyo Albat alitumia saa nyingi kuzunguka sehemu mbalimbali. Baadhi ya watu walikuwa wakimkimbia, kwani hawakutaka kuhusika katika habari yoyote ile wakiogopa mkono wa Alkujar. Wengine walijua kuwa Albat alikuwa mwandishi wa Serikali ya Marekani, wengine walijua kuwa ni mpelelezi wa Serikali ya Syria.

Siku ya pili iliingia bila matumaini yoyote, chakula kilishaanza kumuishia Albat, hakukuwa na dalili yoyote ya kwamba Leo Pordina anaishi katika mji huo.

Wakiwa wanapita pembeni ya jengo moja, ndege ya kivita ilipita juu na kuangusha bomu, bahati nzuri Albat aliliona mapema, alimshika Shania na kulala naye chini. Mlipuko mkubwa ulisikika vipande vya matofali viliruka huku na kule, jengo lilikuwa limeharibiwa vibaya.

Ilikuwa ni ndege ya Serikali iliyokuwa imefanya shambulio hilo, hii ilitokana na mji huo kukaliwa na waasi. Baada ya dakika 10, Albat aliinuka, alimshika Shania na kumwinua. Alipotazama eneo la jengo lile aliwaona watu wakiwa wamefukiwa na vifusi huku baadhi yao wakiwa wamekatika viungo vyao.

Vilio vilisikika, watu walianza kusogea eneo hilo. Waliokuwa wamekufa walikuwa ni watu waliokuwa karibu na jengo hilo.

Ilikuwa ni kawaida ndege za jeshi la Serikali kupita mara kwa mara katikati ya mji huo na kuangusha mabomu, kama mashambulizi ya kushtukiza, endapo itahisi kuwa jengo fulani lina waasi ndani.

Nini kitafuatia? Usikose kesho.   


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*