UONGOZE MOYO WANGU

Ilipoishia

“Mama nimefurahi kukuona, nimesafiri kutoka Afrika Kusini kwa ajili yako, natamani kuongea na wewe,” aliongea Albat kwa tabasamu akiwa amemshika mama Leo Pordina mgongoni.

 “Nami nimefurahi kukuona,” alijibu mama Leo Pordina.

Hakika wote walibaki midomo wazi kwa mshangao wa aina yake.

SASA ENDELEA

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Tayana Leo, aliweza kuzungumza. Kitendo hicho kilikuwa ni muujiza mkubwa sana machoni kwa Lenardo, Matrida pamoja na muuguzi wa hospitali.

Walihitaji masikio maaminifu kusikia ili kuamini kama ni kweli mama Leo Pordina alikuwa ameongea. Lenardo alimsogelea mkewe, alimtazama kwa sura isiyoamini na kumuita.

“Tayana Leo.”

Mama Leo Pordina aliacha kumtazama Albat na kumgeukia mumewe.

“Lenardo,” aliitika kwa kutaja jina la mumewe.

“Mke wangu.”

“Naam mume wangu.”

Upesi Lenardo alimkumbatia mkewe huku machozi mengi yakimtoka. Tayana Leo naye alimlaki mumewe kwa shauku kubwa. Hata hivyo, bado kilikuwa ni kitendawili kisichoteguliwa kutokana na namna mama Leo Pordina alivyoamka.

Albat pekee ndiye aliyekuwa akijua kuwa nguvu ya Leo Pordina iliyokuwa ndani ya moyo wake, ndiyo iliyokuwa imemfanya mama yake aamke na kuzungumza. Hata hivyo, pamoja na hayo, Albat naye alishangazwa na jambo hilo la ajabu.

Baada ya kukumbatiana Lenardo alichukua supu ya samaki na kumnywesha mkewe, Tayana Leo alikunywa taratibu huku akigeuka mara kwa mara kumtazama Albat. Baba Leo Pordina alizidi kujiuliza nini hasa kilikuwa kwa Albat hadi kupelekea mkewe kumtazama sana kijana huyo ukiachia mbali tukio la kunyanyuka kitandani na kuongea.

Wakati huo Matrida alizidi kumtazama Albat asimmalize, alijiuliza kwanini ilikuwa vile, nini kilikuwa kwa Albat hadi kupelekea mtu aliyelala kitandani akiwa hajiwezi kwa mwezi mmoja na nusu kuinuka haraka kiasi kile, kwa sababu ilikuwa ni ngumu kueleweka kwa jambo hilo.

Matrida aliamini kuna kitu kipo kwa kijana huyo wa Kiafrika. Muda mfupi baadaye waliingia madaktari watatu akiwamo daktari mkuu wa hospitali hiyo, hii ilikuwa ni baada ya kupewa taarifa na muuguzi aliyepewa jukumu la kumhudumia bibi Tayana Leo.

Madaktari nao walishangazwa na kuamka na kuketi kwa mama Leo Pordina, walimsogelea karibu wakati akinyweshwa supu ya samaki na mumewe.

“Bibi Tayana Leo habari yako?” daktari mkuu alimsalimia huku akiwa amemshika bega.

“Njema namshukuru Mungu nahisi nimepona,” alijibu mama Leo Pordina.

“Unahisi nini kwenye mwili wako?”

“Nahisi mwili mwepesi ila miguu bado mizito.”

Madaktari hawakutaka kuzungumza mengi kwa kuwa mgonjwa wao alikuwa ameamka muda si mrefu, hivyo walihitaji kumuacha kwanza ili kujiridhisha na hali ile.

“Bwana Lenardo, tutarudi wakati mwingine,” aliongea daktari mkuu.

“Sawa Dk.” alijibu Lenardo.

Matrida aliendelea kumtazama Albat akimtafakari kwa maswali mengi kichwani kwake. Alijikuta anatamani kumfahamu na kujua kile kitu kutoka kwake. Baadaye mama Leo Pordina alihitaji kuzungumza na Albat, Albat aliona ndio muda pekee wa kuijua historia ya binti yake. Albat aliomba kuzungumza naye wakiwa peke yao.

Bwana Lenardo na Matrida walitoka mle ndani na kuwaacha Albat na mama Leo Pordina peke yao. Albat alisogeza kiti karibu na kitanda na kumshika mkono mama Leo Pordina aliyezidi kuonyesha tabasamu.

“Umefanana sana na mwanao,” aliongea Albat kwa sauti ya upole na tabasamu zuri.

Tayana Leo aliinama chini kwa aibu, alitabasamu na kucheka, kisha alijibu.

“Mwanangu ni pacha wangu.”

“Nashukuru kukuona umeinuka tena hakika ni muujiza,” aliongea Albat.

“Nina maswali mengi sana kijana wangu, sijajua nini hasa kipo kwako maana kukuona tu nahisi kama nimemwona mwanangu.”

“Labda kwa kuwa mimi ni rafiki yake mkubwa.”

“Hiyo pekee haitoshi, niliamini siwezi kunyanyuka bila kumwona mwanangu na ilikuwa hivyo siku zote. Nini zaidi kipo kwako kijana wangu? Nieleze ukweli, maana moyo wangu umefarijika sana kukuona hata sijui nguvu za kuinuka kitandani zimetoka wapi.”

“Nami nina maswali mengi sana kuhusu mwanao, ndio maana niko mbele zako. Kwa kuwa si wewe pekee unayeshangazwa na hali hii hata mimi pia inanishangaza.”

“Najua mwanangu amekwishakufa lakini kwanini nipate nguvu bila kumwona yeye. Nampenda sana mwanangu Leo Pordina, kwa mara ya kwanza niliposikia taarifa ya ajali ya ndege, nilihisi maumivu makali zaidi ya ule uchungu nilipokuwa nikijifungua, akili yangu ilishindwa kufanya kazi ghafla. Lakini leo nashangaa kupata nguvu hizi baada ya kukuona wewe, niambie nini kipo kwako kinachohusiana na binti yangu?” aliuliza mama Leo Pordina, bibi Tayana Leo kwa machozi.

Nini kitafuatia? Usikose kesho Jumatatu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*