googleAds

UONGOZE MOYO WANGU-31 (GUIDE MY HEART)

Ilipoishia

 “Lukas alimkabidhi mwanangu kitabu ambacho alikubali kuhatarisha maisha yake ili kisipotee katika mikono yao. Mwanangu alikipokea kwa kilio kikubwa baada ya kukipokea, Lukas alimwambia.

 SASA ENDELEA

“Mpenzi wangu mwenye thamani kubwa ndani ya maisha yangu, nakukabidhi kitabu hiki chenye  nguvu kubwa ya mapenzi yetu. Nisamehe sana maana nimeshindwa kupigania uhai wangu ambao ni mali yako, lakini naamini nitarudi kwa namna nyingine. Pia usije kuwashtaki wale vijana, usifanye hivyo wewe wasamehe tu na hakikisha hawafungwi jela. Nakutakia maisha mema nakupenda sana Leo Pordina.”

Yalikuwa ni maneno yaliyorarua moyo wa mwanangu, alilia sana, alimwomba abaki pamoja naye lakini Lukas hakuweza kupigania maisha yake, hatimaye alifia kwenye kifua cha mwanangu ndani ya kanisa.

Mwanangu alilala pale pale akilia kilio kikuu, hakuamini kama mpenzi wake amepoteza maisha kirahisi namna ile.

Kulipokucha kiongozi wa kanisa alifika  kanisani na kumkuta binti yangu akiendelea kulia huku akiwa amemlalia Lukas juu. Upesi alipiga simu polisi, polisi walifika pale na kuichukua maiti.  Walimchukua pia na yeye ili akajieleze kituoni.”

Mama Leo Pordina aliendelea kumsimulia Alabt mkasa huo wa kutisha uliowahi kumpata mwanawe.

“Alieleza kwa tabu maaana hakuwa na nguvu ya kusema kila kitu. Polisi waliamua kumrudisha nyumbani maana akili na afya yake vilianza kubadilika. Kilio kilitawala kwa familia zote mbili, ulikuwa ni msiba mkubwa kuwahi kutokea kwenye koo zetu. Shuleni kwao nako hali ilikuwa si nzuri, wanafunzi walilia sana wakimlilia kijana Lukas.

Mwanangu alishindwa kula, tulitumia ushawishi mkubwa na kumfariji kwa nguvu zote ili apate kula chakula. Baada ya siku mbili polisi wafanikiwa kuwakamata vijana waliosababisha kifo cha kijana Lukas.

Vijana hao watatu walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili. Kesi hiyo iliendeshwa mjini Makia, mhusika mkuu ambaye ni mwanangu, naye alifikishwa mahakamani kutoa ushahidi. Mahakama iliwakuta na hatia ya kuua, hivyo iliwahukumu vijana hao kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Lakini pale pale mhakamani, mara baada ya kutoka hukumu hiyo, mwanangu aliongea jambo la ajabu ambalo liliwafanya watu wote wamshangae na kuhoji vikali. Wazazi wa Lukas pia hawakupenda kusikia neno hilo la kuudhi.

Binti yangu aliomba mahakama iwasamehe na kuwaacha huru vijana hao. Hata vijana wenyewe walishangaa sana kusikia hivyo. Mahakama haikuwa tayari kukubali suala hilo, kwa kuwa yenyewe ndiyo iliyokuwa imewashtaki vijana hao.

Lakini Leo Pordina hakutaka kuona vijana hao wakifungwa jela kwa kosa la kumuua mpenzi wake. Ingawa ilimuuma sana lakini alihitaji kutimiza kile mpenzi wake alichomwambia. Kumbuka wakati Lukas akifa katika mikono yake alimtaka mwanangu kuwasamehe vijana waliopelekea kifo chake.

Mahakama ilisema kuwasamehe vijana hao ni juu yake, wala hakatazwi ila mkono wa sheria lazima ufuatwe kwa kuhakikisha vijana hao wanatumikia adhabu hiyo. Lakini Leo Pordina aliendelea kusisitiza kuwa anahitaji mahakama hiyo iwaache huru.

Mahakama ilianza upya kujadili suala hilo, wazazi wa Lukas walichukizwa na maneno ya Leo Pordina na kudai kuwa kumbe mwanangu alifurahia kifo cha mtoto wao, walihoji vikali kwanini aanze kuwatetea vijana waliomuua mtoto wao.

Mahakama ilisema haimzuii mwanangu kuwasamehe wale vijana ila suala la kutumikia adhabu liko pale pale kwani ni jambo lingine katika mkono wa sheria.

Lakini mwanangu Leo Pordina alisimama mahakamani na kuwaeleza jambo lilionekana la msingi kwa mujibu wa msamaha huo. Alisema kuwa pindi Lukas alipokuwa anakufa kwenye mikono yake, aliwasamehe vijana hao na kumtaka yeye pia kuwasamehe. Alisema hivyo alikuwa anatimiza ahadi ya mpenzi wake, maana alisema asingefanya hivyo, angekuwa amevunja agano lake na Lukas.

Mahakama ilihoji kuwa kama alikuwa hapendi kuona vijana hao wakifungwa, kwanini alitoa ushahidi wa kutosha wa kuonyesha vijana hao wamehusika na mauaji ya Lukas. Ilitakiwa akatae kuwa hawahusiki ili wasifikishwe mahakamani.

Lakini mwanangu aliwajibu jibu lililomfanya aonekane mtu wa tofauti na mwenye hekima. Wazazi wa Lukas walianza kumwelewa mtoto wangu. Alisema  kwanza uongo ni dhambi, hivyo hakuwa na haja ya kuongopa kwamba vijana hao hawahusiki ili wasikutwe na hatia, alitoa ushahidi wa kutosha mahakamani ili sheria na jamii iwakute na hatia.

Maana alihitaji jamii ijue kuwa vijana hao wanahusika na kifo cha Lukas ili wao wenyewe watambue kuwa wamefanya kosa kwa kuwa msamaha wenye nguvu ni ule unaokuja wakati binadamu anakosa tumaini.

Alisema kulikuwa hakuna maana ya msamaha ikiwa vijana hao wataendelea kusota jela. Hawatatambua nini maana ya msamaha kwa kuwa tayari watakuwa wamehukumiwa. Ili msamaha uwe na nguvu alisema ni vema vijana hao wakatafakari kuachiwa kwao huru ingawa walikuwa wamefanya jambo linalostahili hukumu hiyo.

Alisema kuwasamehe vijana hao, kutamfanya awe huru na maisha kwa kuwa atakuwa ametimiza ahadi ya mpenzi wake. Alisema hata yeye pia anaona vema akiwasamehe.

Watu wote mahakamani walistaajabu maneno hayo yenye nguvu, yule kiongozi wa kanisa ambalo kijana Lukas alifia, naye alishangazwa sana  na maelezo ya mwanangu. Hata yeye alisimama mahakamani kumuunga mkono binti yangu. Ilibidi wazazi wa Lukas nao wakubali shauri hilo maana nao hawakutaka kupinga, kwa kuwa wangeonekana wanampinga mtoto wao aliyekuwa ametoa msamaha kwa vijana waliomuua.

Kesi hiyo pia ilikuwa ikirushwa kwenye vyombo vya habari, watu wote nchini Ujerumani waliisikia na kuitolea maoni.

Mahakama haikuwa na namna nyingine, iliwaachia huru vijana hao kwa sharti la kifungo cha nje cha miaka mitano. Vijana hao hawakuamini kama wameachiwa huru, lilikuwa ni jambo la ndoto kwao, walimwona mwanangu ni binadamu wa kipekee sana hasa katika maisha yao.

Vijana hao waliokuwa wahuni wa mtaani na watumiaji wa dawa za kulevya, waliacha kufanya mambo yote mabaya na kuamua kuishi maisha mapya yenye kupendezwa na watu.

Walianza kumtumikia Mungu katika kanisa ambalo Lukas alifia. Msamaha ule ulileta nguvu hata kwa mwanangu Leo Pordina kwani vijana hao walikuwa marafiki zake.

Mwanangu alikuwa katika hali mbaya ya upweke kiasi cha kutaka kumletea ugonjwa kama huu unaonisumbua mimi. Vijana hao walikuwa wakimtembelea na kumfariji, walikuwa ni marafiki zake wakubwa.

Lilikuwa ni tukio kubwa sana lililojenga kitu cha ajabu kwenye maisha ya binti yangu. Wazazi wa wale vijana walimshukuru sana mwanangu kwani alikuwa amewaokoa vijana wao maana wao kama wazazi walikuwa wameshindwa kuwaonya vijana hao waliokuwa sugu katika maovu.”

Alisimulia bibi Tayana Leo kwa machozi mengi maana kumbukumbu hiyo ilikuwa ikipenya hadi kwenye kiini cha moyo wake. Albat alishangazwa sana na simulizi hiyo ya maisha ya Leo Pordina, safari hii hakutokwa na machozi ya Leo Pordina pekee hata ya kwake pia yalimtoka.

Pia ilikuwa ni simulizi ya ajabu na yenye kuogofya kwani ilionekana kuingia moja kwa moja kwenye maisha ya Albat.

Mama Leo Pordina alipokunywa tena juisi aliendelea kusimulia.

“Baada ya siku kadhaa mwanangu alipata afya njema, Jumapili saa moja jioni alikwenda kwenye lile kanisa akiwa na kile kitabu cha simulizi ya Romeo and Juliet. Alipiga magoti kanisani na kumwomba Mungu akilia sana.

Alimwomba Mungu amrudishe Lukas duniani na kama hatafanya hivyo, basi amletee mtu mwingine atakayebadili nafasi ya Lukas, atakayekuwa na tabia ya Lukas kwa kila kitu asipungukiwe hata na tabia moja. Aliahidi kutompa kitabu mtu yeyote asiyefanana na Lukas.

Toka siku hiyo mwanangu aliishi maisha ya amani akitegemea Mungu kutenda jambo alilomwomba.”

Mama Leo Pordina alimalizia kusimulia historia fupi ya binti yake iliyokuwa na tukio la jabu ndani yake. Albat alishaanza kupata majibu ya maswali yake ingawa bado alisumbuliwa na suala moja tu la Leo Pordina kumtokea katika hali ya kimiujiza, maana ilikuwa ikiaminika kuwa alikuwa amekwisha poteza maisha nchini Syria.

Lakini Albat alimuuliza mama Leo Pordina swali gumu lenye kuleta maana ya ajabu.

“Mama unadhani mimi naweza kuwa Lukas yule aliyekufa miaka sita iliyopita?”

Nini kitafuatia? Usikose kesho.

Najua ni hadithi itakayofunza mengi, ingawa bado inakupa maswali yasiyo na majibu endelea kuifuatilia. Toa maoni yako. Like page ya Hadithi za Eman Fisima Facebook usome hadithi kali ya Nilishakufa,  Mungu akubariki.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*