UONGOZE MOYO WANGU

Ilipoishia

Aligeuka na kurudi aliko kaa bila kumjibu lolote. Yule msichana alishangazwa na kitendo cha mwanaume kuja mbele yake na  kumwita jina lisilo lake.

Albat alikaa kwenye kiti chake aliwatazama baadhi ya abiria wa pembeni yake na kutazama dirishani. Akili yake iliamini Leo Pordina alikuwa pamoja naye.

SASA ENDELEA

SAA 2:00 mshale wa dakika ukiwa unaelekea kwenye eneo la dakika mbili, ndege ya shirika la Bayerkeni ilitua uwanja wa kimataifa wa Borusia jijini Berlin.

Hali ya hewa ya Ujerumani ilikuwa ni ya baridi kiasi na matone madogo ya mvua na barafu. Baada ya kutoka airport, Albat alielekea eneo la tax akiwa na mizigo michache. Alipokelewa na dereva mmoja, mzee wa makamo.

Albat alimwomba dereva huyo ampeleke hoteli ya nyota tatu iliyokuwa karibu na chuo kikuu cha Maxfuture. Albat alipelekwa hadi kwenye hoteli moja iliyoitwa Flower iliyokuwa umbali wa kilomita 11 kutokea Chuo Kikuu cha Maxfuture. Albat alipokelewa kwenye hoteli hiyo ambayo kwa nchi za Kiafrika, ingeweza kulinganishwa na hoteli ya nyota nne.

Albat aliamini angeweza kumudu gharama kwenye hoteli hiyo kwa siku atakazokaa nchini Ujerumani. Alipelekwa kwenye chumba kilichokuwa ghorofa ya tatu ya jengo hilo. Jambo la kwanza kwake baada ya kuingia katika chumba hicho, lilikuwa ni kutoa kitabu cha Romeo and Juliet kitabu cha Leo Pordina na kukiweka kitandani.

Ikiwa ni saa nne usiku, Albat alipata chakula, hakuwa amechoka sana ingawa safari ilikuwa ni ya zaidi ya saa 22. Jambo la kwanza kwake alilokuwa akilifikiria, endapo ataamka asubuhi, lilikuwa ni kwenda chuo cha Maxfuture, chuo alichokuwa akisoma Leo Pordina na wenzake watatu ambao nao walipoteza maisha kwenye ajali ya ndege.

Leo Pordina na wenzake watatu walikwenda kusoma chuo cha Zululand Afrika Kusini, baada ya majina yao kutajwa kwenye orodha ya wanafunzi wanaokwenda kukiwakilisha chuo chao cha Maxfuture katika nchini nyingine.

Chuo cha Maxfuture kilikuwa kikiendesha mpango wake kila mwaka wa kubadilishana wanafunzi kutoka kwenye mataifa mbalimbali. Chuo kilikuwa kikiwachagua wanafunzi wanne kwenda kwenye nchi zilizokuwa kwenye mapendekezo.

Leo Pordina na wenzake watatu walichaguliwa kwenda barani Afrika katika chuo kikuu cha Zululand cha nchini Afrika Kusini.

Kesho yake ilifika Albat aliamka salama, baada ya kupata kifungua kinywa, alikwenda kupanda basi la jiji la Berlin lililokuwa likielekea chuo kikuu cha Maxfuture. Jambo lake kuu kwake lilikuwa ni kwanza kukutana na wazazi wa Leo Pordina kama alivyoelekezwa na Mchungaji Luke Morgan.

Lakini alijua hawezi kuwapata wazazi wake kirahisi bila kwenda kwanza kwenye chuo alichokuwa akisoma kipenzi chake. Maana hakuwa akijua Leo Pordina alikuwa akiishi sehemu gani ndani ya jiji hilo kubwa duniani.

Baada ya dakika 35, Albat alishuka eneo la Kansil eneo lililoitwa kituo kikuu cha chuo, Albat alistaajabu uzuri wa chuo cha Maxfuture, eneo lililokuwa limetawaliwa na uoto wa kijani na maua mekundu, majengo ya kifalme yalikuwa yamezunguka pande zote.

Alitembea taratibu akishangaa uzuri wa chuo hicho, kilichokuwa cha tatu kwa ukubwa nchini Ujerumani. Hakika alitamani siku moja kuja kusoma katika chuo hicho.

Moja kwa moja aliingia geti kuu la chuo hicho na kuonana na wana usalama wa chuo, ambao walimpa kitambulisho kama mgeni. Akiwa anatembea kuelekea kwenye majengo makuu ya chuo, alikuwa akipishana na wanafunzi wengine waliokuwa wakimtazama wakijua kuwa alikuwa ni mgeni.

Alifika eneo moja lililokuwa na maua mengi pamoja na mnara mfupi. Macho yalimtoka baada ya               kuona picha ya Leo Pordina pamoja na wale wenzake waliopata ajali ya ndege, zikiwa mbele ya mnara huo. Ilishangaza kwa kuwa ni mwezi mmoja ulikuwa umepita tokea ajali ya ndege itokee, lakini bado waliendelea kukumbukwa.

Wanafunzi wa chuo hicho bado waliendelea kuwa kwenye maumivu makubwa ya kuwapoteza wanafunzi hao. Albat alifarijika sana kuona vile, ingawa nafsi yake iliendelea kuumia. Wakati mwingine hata yeye pia alikuwa haisikii  ile sauti ya Leo Pordina iliyokuwa ikimwaminisha kuwa yeye ni mzima.

Alisimama pale kwa muda mrefu, eneo hilo lilikuwa ni tulivu lisilo na watu wengi, baadhi ya wanafunzi waliokuwa karibu, walianza kumtazama wakijiuliza alikuwa ni nani.

Baadaye alikwenda mapokezi ya chuo na kukutana na wafanyakazi saba, aliongea kuhusu jambo lililokuwa limemleta chuoni hapo, walimwelewa haraka na kumpigia simu mkuu wa chuo, mkuu wa chuo alimkaribisha Albat ofisini kwake.

Albat alipelekwa kwa gari hadi kwenye jengo kuu lililokuwa umbali wa kilomita tatu tokea eneo kuu la mapokezi. Alipofika alikaribishwa kwa ukarimu baada ya kutambulishwa kwa baadhi ya maprofesa wa chuo waliokuwa chuoni muda huo.

Walimu wa chuo hicho waliokuwepo walistaajabu na kufurahi kumwona  mwanafunzi wa chuo cha Zululand amefika katika chuo chao maana toka ajali ya ndege itokee hakuna mwanafunzi yeyote wala profesa wa chuo cha Zululand aliyefika katika chuo cha Maxfuture.

Wanafunzi, maprofesa na watu wa idara ya chuo cha Zululand wao walikuwa wametuma tu salamu za pole kwa chuo cha Maxfuture na si kuja kabisa Ujerumani.

Albat alikaribishwa kwa moyo mmoja ndani ya idara ya chuo, kabla ya kuonana na mkuu wa chuo ambaye kuonana naye ilikuwa ni bahati kwa wanafunzi wa chuo hicho, Albat aliongea mawili matatu na walimu wengine. Aliwapa pole kwa kuwapoteza wanafunzi wao.

Baadaye kidogo alikutana na mkuu wa chuo na kuongea naye, hakutaka kuzungumza ni jambo gani hasa lililokuwa limemleta Maxfuture au Ujerumani, kwa kuwa alijua suala lake lilikuwa zito na linalomhitaji yeye mwenyewe pekee, kwa kuwa hata angemweleza mtu yeyote asingemwelewa zaidi angemwona mwendawazimu.

Profesa mkubwa na mkuu wa chuo hicho aliyeitwa Mackel Yufer alimshukuru sana Albat kwa kuwatembelea na kuwapa pole, kwa kuthamini alichokifanya Albat, alitangaza mkutano mkubwa wa wanafunzi wa chuo na wana idara wote wa chuo hicho.

Taarifa hiyo ilitolewa katika mtandao wa chuo na kwenye vyombo vya habari. Albat alishangaa kuona anaambiwa jambo ambalo hakulifahamu kuhusu Leo Pordina.

“Leo Pordina alikuwa ni makamu wa Serikali ya wanafunzi kwa muda mrefu, wanafunzi hawakutaka aachie madaraka maana walimpenda na kumwona kiongozi bora kwao. Mwaka huu alikuwa kwenye harakati za kugombea urais wa Serikali ya chuo, alikuwa pia mgombea wa uenyekiti wa vyuo vikuu vya Ujerumani. Hivyo chuo na nchi yetu kwa ujumla imempoteza mtu muhimu sana,” aliongea mkuu wa chuo hicho.

Albat alishangazwa na ukubwa wa Leo Pordina ndani ya Serikali za wanafunzi nchini Ujerumani. Hakuwa akijua lolote kuhusu masuala hayo kwani Leo Pordina hakuwahi kumwambia kuwa yeye ni makamu wa chuo cha Maxfuture wala kujitambulisha kwa wanafunzi wa chuo cha Zululand.

Baada ya maongezi hayo, Albat alimuaga mkuu wa chuo, profesa alimtaka kufika kesho mapema kwenye mkutano wa wanafunzi uliopangwa kufanyika saa kumi jioni, mkutano ulioandaliwa kwa ajili yake.

Ilipofika kesho Albat alifika tena chuoni hapo, ndani ya ukumbi wa chuo zaidi ya wanafunzi 10,000 walikuwa wamehudhuria mkutano huo. Albat alikaribishwa kama msemaji mkuu wa mkutano huo, akikiwakilisha chuo kikuu cha Zululand yote hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya Leo Pordina na wenzake.

Albat alisimama mbele ya umati wa wanafunzi na kuongea kwa lugha ya Kijerumani.

“Asanteni kwa kunikaribisha katika chuo chenu. Jina langu naitwa Albat Zimbe, ni mwanafunzi wa chuo cha Zululand cha Afrika Kusini, nilikuwa ni rafiki mkubwa sana wa Leo Pordina.”

Wakati Albat akiongea hayo, msichana mmoja mzuri mwembamba aliyekuwa amevaa miwani, alikuwa akimsikiliza kwa makini Albat. Ilionyesha ameguswa sana na ujio wa Albat.

Nini kitafuatia? Usikose kesho.

 Kama Leo Pordina si jini na wala si mzimu, unadhani imekuaje hadi amtokee Albat.

Previous Article
Next Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*