UONGOZE MOYO WANGU (21)

Ilipoishia

BAADAYE akili fulani ilimjia na kuwakumbuka marafiki zake Mwita Benard na Betty. Moja kwa moja alijua kuwa wao ndio waliokuwa wamekichukua kitabu hicho.

 “Mungu wangu!” alijisemea Albat baada ya kushtuka.

Upesi bila kuvaa viatu huku shati lake likiwa wazi, alitoka ndani anakimbia na kwenda kwenye gari, aliliwasha na kuondoka nyumbani kwa kasi. Alishika njia ya kuelekea nyumbani kwa Mwita akiwa amekasirika sana.

SASA ENDELEA

Kila mmoja alirudi nyuma hatua mbili, wakikiacha kitabu mezani wasitake tena kukishika, miili yao ilianza kutetemeka, hofu iliwatawala waliogopa sana.

Kwa macho yao walishuhudia kitabu kikijifunga chenyewe, kitendo hicho  kiliwaacha mdomo wazi maana hawakuwa nje ambako kuna upepo bali walikuwa ndani huku kukiwa hakuna feni karibu.

Si Mwita si Benard wala Betty wote waliogopa  kukikaribia tena kitabu cha Leo Pordina, kitabu ambacho miujiza yake ilianza kujionesha kwenye picha ya Leo Pordina baada ya picha hiyo kubadilika badilika.

Kila mmoja wao sasa aliamini kuwa Albat hakuwa amechanganyikiwa bali alikuwa sahihi. Maana macho yao wenyewe yalikuwa yameshuhudia matukio hayo ya ajabu ambayo hawajawahi kuyaona wala kuyasikia katika maisha yao.

Kila mmoja alibaki kimya ashindwe la kuongea wala la kufanya walibaki wakitazamana kama watu wenye siri moja iliyowekwa hadharani. Kila mmoja hakuwa na hamu tena ya kuongea kuhusu kitabu hicho.

Wakiwa katika sintofahamu hiyo, walishangaa kuona Albat akiegesha gari nje ya nyumba, upesi Mwita aliingiwa na ujasiri akakichukua kitabu na kukificha kwenye kona ya kochi na kukifunika na mto. Wote walipeana ishara fulani, Benard aliwasha televisheni haraka kisha Betty akaelekea bafuni.

Punde tu Albat aliingia na kuwakuta Mwita na Benard sebuleni, hakuwapa salamu zaidi aliwaambia.

“Nipeni kitabu.”

Walitazamana wao kwa wao, walishindwa kufanya walichoambiwa wala kujitetea. Maana kila mtu alijua kuwa Albat alishajua kuwa kitabu walikuwa nacho wao.

“Albat best hata salamu hakuna,” aliongea Mwita.

“Salamu haina umuhimu kwa sasa, cha muhimu nipeni kitabu mimi niondoke,” alijibu Albat akiwa na ndita nyingi usoni.

“Karibu kwanza ukae Albat,” Benard alidakia.

“Sihitaji kukaa naombeni kitabu, kwanza mmenikosea sana, mtachukuaje kitabu bila kuniambia?”

“Albat sisi ni wenye makosa kwa mara ya pili tunakutenda tunaomba utusamehe na tuhitaji kukaa na wewe kuzungumza mambo yote yanayokuhusu.”

“Tumeshautambua ukweli sasa tumeamini kuwa hujachanganyikiwa wala hujaathirika kisaikolojia,” aliongea Mwita.

“Sawa pamoja na kutambua hayo, kiko wapi kitabu nipeni sasa hivi.”

Mwita alisogea kwenye kona ya kochi aliufunua mto, alikichukua kitabu kwa uwoga mwingi na kumpa Albat. Albat alikipokea haraka na kuanza kuondoka pale sebuleni.

“Kwanini unatufanyia hivi wenzako? Hebu njoo kwanza tuyajenge besti,” aliongea Benard.

Albat alisimama mlangoni akageuka na kuwatazama kwa sekunde kadhaa kisha akasema.

“Mlikuwa na nafasi ya kunisaidia hapo mwanzo, lakini kwa sasa nafasi hiyo si yenu tena. Sasa mimi ni mwenye nguvu na ninaweza kusimama mwenyewe. Endeleeni na masomo wala msiwaze kuhusu mimi.”

Aliposema hayo alifungua mlango na kutoka, Mwita alimfuata kabla hata hajaiwasha injini ya gari.

“Albat hebu nisikilize, punguza kinyongo, najua ni jinsi gani ulivyoumia baada ya kukupinga, lakini wakati huu sahau dhambi yangu, nipe nafasi ya kukusaidia,” aliongea Mwita.

“Mimi sina kinyongo na wewe najua ilikuwa ngumu kuamini. Hata angekuwa mtu mwingine tofauti na wewe, asingekubaliana na yale yote niliyokuwa nikiongea kuhusu Leo Pordina,” aliongea Albat huku akinyonga ufunguo.

Baada ya gari kuwaka, aliongeza kwa kusema.

“Usijali Mwita, hata hivyo kesho nasafiri.”

“Unasafiri?”

“Ndio.”

“Unakwenda nyumbani?”

“Hapana siendi Tanzania, nakwenda Ujerumani.”

“Kufanya nini tena?” aliuliza Mwita kwa mshangao mkubwa.

“Yote ni kwa ajili ya Leo Pordina.”

“Kivipi tena Albat?”

“Bado hautanielewa na utahitaji maneno mengi ili upate kunielewa,” alijibu Albat huku akikanyaga krachi.

“Albat usiondoke kwanza hebu tuongee,” aliongea Mwita huku mikono yake ikiwa kama inataka kuzuia gari.

Lakini Albat aliweka gia namba moja na kuondoa gari. Alimuacha Mwita  amesimama akiwa ameshindwa kulizuia gari, alimuacha mwenye sura ya huzuni.

Albat alifika nyumbani saa 6:45 mchana, aliingia chumbani na kitabu cha Leo Pordina, alikitazama na kukifungua ukurasa wa pili wenye picha ya Leo Pordina, aliibusu picha na kukiweka kitandani.

Mchana ulipita na usiku uliingia, tayari alishakuwa amefanya maandalizi yote ya safari, alikuwa akiogopa kuwapigia simu wazazi wake kuwaeleza kuhusu safari yake ya kuelekea Ujerumani. Alijua endapo atawapasha habari kuhusu safari hiyo, huenda wazazi wake wasimruhusu kwenda, jambo ambalo lingekuwa ngumu kukubali uamuzi wao.

Aliona afanye siri wasipate kujua kama watajua, basi atakayekuwa amewajulisha awe ni rafiki yake Mtanzania mwenzake Mwita na si yeye. Ingawa alijua ni kosa kubwa analolifanya lakini alijisemea kuwa wakati mwingine kufanya makosa ni kutengeneza njia iliyosahihi.

Tayari moyo wake ulishakuwa na nguvu ya kufanya lolote kwa ajili ya Leo Pordina, aliuona kabisa kuwa unaongozwa na msichana huyo kisura. Kwa wakati huo fikra zake zilikuwa zimesimama katika pande mbili, aliamini Leo Pordina aliuawa bado anaishi kwenye dunia aliyopo yeye, pia aliamini Leo Pordina alishakufa ila alikuwa akiishi kupitia moyo wake.

Akili yake pia ilikosa jibu moja sahihi kati ya hayo mawili, muda mwingine aliamini kweli Leo Pordina alikuwa akiuongoza moyo wake na fikra zake maana alijikuta anajipa matumaini pasipo kuwa na tumaini, hakuelewa ni kwanini alikuwa hivyo, ubongo wake ulishindwa kufikiria ng’ambo ya pili ya udadisi wake.

Tarehe 12/12/2014 Albat alikuwa uwanja wa ndege, saa mbili asubuhi alipewa tiketi ya ndege ya shirika la Bayerkeni airways, baada ya saa moja abiria wote waliingia kwenye ndege.

Ndege ya Bayerkeni iliuacha uwanja wa Madiba Zululand na kuruka angani tayari kwa kuanza safari ya kuelekea jiji la Berlin lililokuwa mashariki mwa Ujerumani.

Wakati mwingine roho ilikuwa ikumuuma sana Albat, kwani alikuwa akiamini kabisa kuwa alikuwa amemucha Leo Pordina nyumbani kwake. Kwa kuwa wakati anapanda ndege hakuiona ishara yoyote ya Leo Pordina naye kupanda ndege.

Hivyo aliamini kuwa alikuwa amemuacha ndani ya nyumba yake yaani anamuacha Afrika Kusini na yeye anakwenda Ujerumani kitendo alichokiona kuwa ni kama anamuacha Leo Pordina peke yake.

Ndege ikiwa inakaribia kufika katikati ya safari, Albat akiwa anasoma jarida la Lol, alianza kusikia kicheko cha Leo Pordina mle ndani ya ndege. Alishtuka na kuliweka jarida chini alitega sikio ili kukisikia vema maana kilikuwa ni kile kicheko sahihi cha Leo Pordina.

Baadaye aligundua kuwa kicheko hicho kilikuwa kikisikika viti vya tatu nyuma kutokea yeye alipo. Upesi alinyanyuka na kuanza kupiga hatua akiifuata sauti hiyo nzuri iliyokuwa na kicheko cha kipekee. Kadiri alivyozidi kusogea ndivyo alivyokisikia vizuri.

Moyo wake unaoongozwa uliamini kuwa aliyekuwa anacheka mle ndani ya ndege alikuwa ni Leo Pordina na si mtu mwingine. Aliendelea kutembea huku akiwatazama abiria mmoja baada ya mwingine ili kumtafuta anayecheka.

Alipofika viti vya tatu tokea alipokuwa amekaa yeye, hakuamini macho yake baada ya kumuona Leo Pordina akicheka, yaani alimuona kwa macho yake mawili.

“Leo Pordina!” aliita Albat.

Leo Pordina aliacha kucheka na kumtazama Albat. Alimtazama sana na kutabasamu. Lakini ghafla alishangaa kumuona mtu mwingine tofauti na Leo Pordina alikuwa ni msichana wa kizungu aliyebaki kumtazama Albat aliyekuwa ameganda kama sanamu.

“Haloo kaka halooo!” aliita msichana huyo.

Albat alizinduka.

“Vipi mbona unanitazama sana umenifananisha?” aliuliza msichana huyo.

Albat alishindwa cha kujibu, akili yake ilikuwa imesimama ghafla kwa kuwa macho yake, kweli yalikuwa yamemuona  Leo Pordina. Hivyo hakuamini kuona msichana yule si Leo Pordina.

Aligeuka na kurudi aliko kaa bila kumjibu lolote. Yule msichana alishangazwa na kitendo cha mwanaume kuja mbele yake na  kumuita jina lisilo lake.

Albat alikaa kwenye kiti chake aliwatazama baadhi ya abiria wa pembeni yake na kutazama dirishani. Akili yake iliamini Leo Pordina alikuwa pamoja naye.

Nini kitafuatia? usikose kesho 

Previous Article
Next Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*