UONGOZE MOYO WANGU

lipIoishia

Toka jana walipokuwa wakikitazama kitabu hicho, picha ya Leo Pordina ilikuwa ikiangalia kushoto, lakini asubuhi hiyo picha iligeuka na kuangalia kulia. Halafu tabasamu la Leo Pordina katika picha hiyo lilikuwa limepotea, wakati huo alionekana amenuna.

SASA ENDELEA…

Jambo hilo la ajabu alikuwa ameliona Mwita aliyekuwa amekishika kitabu. Alitoa macho vema kulitazama tukio hilo la kuogofya.

Hakutaka kuwaambia kwanza wenzake wala kuwauliza lolote, alibaki kuitazama picha ya Leo Pordina ili aendelee kuhakikisha uzima wa macho yake. Bado picha ya Leo Pordina ilikuwa imegeukia kulia badala ya kushoto.

Alikifunga kitabu haraka na kuwatazama wenzake waliokuwa wakiendelea kuongea kuhusu Albat kuchanganyikiwa. Baadaye kidogo alikifungua tena, tukio lingine la ajabu alilishuhudia baada ya kuona Leo Pordina ametabasamu katika picha ile wakati mwanzo alikuwa amenuna, huku akimtazama sana yeye.

Mwita alianza kuhema taratibu akiogopa kukishika tena kitabu. Upesi alikiweka mezani, sasa akiamini moja kwa moja kuwa Albat alikuwa sahihi. Benard na Betty walimtazama na kumwona katika hali ya tofauti.

“Vipi Mwita kuna tatizo?” aliuliza Betty.

“Tatizo lipo ndio,” alijibu Mwita.

“Nini tena?” aliuliza Benard.

“Hebu fungueni ukurasa wa pili wa kitabu,” aliongea Mwita.

Upesi Benard alikifungua, akakitazama na kuuliza.

“Kuna nini?”

“Itazame vizuri picha ya Leo Pordina,” aliongea Mwita.

Benard aliitazama kwa makini huku Betty naye akisogea kuitazama.

“Mmmmh!” Benard aliguna.

“Mmeona nini?” Mwita aliwauliza.

“Hii picha jana mbona kama ilikuwa ikiangalia kushoto?” aliuliza Betty.

“Kweli hata mimi nakumbuka ilikuwa hivyo,” alijibu Benard.

“Macho yenu hayajawadanganya mnachokiona ni sahihi, hiyo picha jana ilikuwa ikiangalia kushoto lakini leo inaangalia kulia, ina maana kuwa imegeuka,” aliongea Mwita.

Benard na Betty walitazamana huku hofu fulani ikianza kujengeka kwao.

“Na nilipokifungua kwa mara ya kwanza baada ya kuona imegeuka nilikuta Leo Pordina akiwa amenuna lakini sasa anatabasamu,” aliongeza Mwita.

“Mbona amenuna?” aliuliza Benard.

“Nini?” Mwita alishtuka.

“Ndio kanuna si unamuona?” alijibu Betty huku akimwonesha Mwita.

“Basi picha imebadilika tena,” alijibu Mwita.

Wote walichanganyikiwa, walijiuliza mara mbilimbili kuhusu tukio hilo la ajabu, sasa wote waliamini kuwa kitabu hicho kilikuwa na miujiza. Upesi walikiweka mezani wakikiogopa tena kukishika.

Walikuwa wamekiweka mezani bila kukifunga, lakini walishangaa kuona kikijifunga chenyewe, hapo ndipo walitamani kutafutana.

NYUMBANI KWA ALBAT

Baada ya Albat kumaliza kuongea na wahudumu wa shirika la ndege, shirika  la Bayerkeni airways, ili kupata tiketi ya ndege ya kuelekea Ujerumani, aliingia chumbani ili kuanza kupanga nguo zake mapema kabla ya kesho kutwa kuianza safari.

Akiwa kabatini alishangaa kuona anatokwa na machozi, alijishika kwenye macho akijiuliza kwanini alikuwa akitokwa na machozi, wakati hakuwa amepiga mwayo wala kukumbuka jambo lolote la huzuni.

Maana kwa wakati huo alikuwa ni mwenye furaha baada ya mchungaji kumpa mwongozo juu ya jambo linalomkabili.

Akiwa katika kushangaa huko, alisikia sauti ya mtu akilia, moja kwa moja alijua kuwa aliyekuwa akilia alikuwa ni Leo Pordina. Lakini alijiuliza kwanini atokwe yeye na machozi.

Alianza kuogopa huku akizungusha kichwa kutazama pande zote mle chumbani. Baadaye wazo lilimjia, alipotazama kitandani hakukiona kitabu cha Leo Pordina, wala hakikuwemo mle chumbani, tukio lililokuwa la ajabu kwake na la mara ya kwanza kuona kitabu kimetoweka kitandani.

Aliendelea kusikia sauti ya Leo Pordina akilia, huku yeye akiendelea kutokwa na machozi, ina maana kuwa machozi yaliyokuwa yakimtoka ni kwa sababu ya  kilio cha Leo Pordina. Lilikuwa ni jambo lingine la ajabu zaidi kuwahi kulishuhudia.

Hakujua nini kilikuwa kikimliza mpenzi wake, wala hakujua kitabu kilikuwa kimekwenda wapi. Lakini baadaye alijisemea kuwa  huenda alikuwa amemuudhi Leo Pordina kiasi cha  Leo Pordina kuamua kukichukua kitabu chake.

“Leo Pordina mpenzi wangu unalia nini ni kipi nimekukosea?” aliuliza Albat akiongea peke yake akiamini Leo Pordina alikuwa akimsikia.

Hakujibiwa lolote zaidi alisikia sauti ile ya kulia ikisikika kutokea sebuleni. Upesi alitoka chumbani na kwenda sebuleni ambapo hakumwona Leo Pordina. Ila jambo la ajabu alipotazama mezani aliiona karatasi yenye maandishi.

Aliisogelea na kuishika, alikutana na mwandiko wa Leo Pordina, maandishi yakiwa yanasomeka hivi.

“Sikuwahi kumpa mtu yeyote kitabu changu, leo natokwa na machozi kwa sababu, mtu mwingine tofauti na wewe amekishika na kukifungua, nimekosewa sana.”

Albat alishtuka na kutazama huku na kule, hakuelewa kwanini Leo Pordina alikuwa amesema vile, baadaye alijisemea kuwa ni nani mwingine alikuwa amekishika kitabu hicho.

Baadaye akili fulani ilimjia na kuwakumbuka marafiki zake Mwita Benard na Betty. Moja kwa moja alijua kuwa wao ndio waliokuwa wamekichukua kitabu hicho.

“Mungu wangu!” alijisemea Albat baada ya kushtuka.

Upesi bila kuvaa viatu huku shati lake likiwa wazi, alitoka ndani anakimbia na kwenda kwenye gari, aliliwasha na kuondoka nyumbani kwa kasi. Alishika njia ya kuelekea nyumbani kwa Mwita akiwa amekasirika sana.

Nini kitafuatia? Usikose Alhamisi.    

Previous Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*