UNAPOMTAJA GUARDIOLA UMKUMBUKE NA CONTE

PEP Guardiola ni kama ameshamaliza kazi aliyopanga kuifanya pale Manchester City. Na kizuri zaidi ameifanya Man City icheze kama wale wamiliki wa Kiarabu walivyotamani kwa miaka kadhaa sasa.

Nani anayeweza kukaa bila kumuwaza Guardiola kwa sasa?

Katika wakati huu unaosoma andiko hili, nikukumbushe vitu viwili ambavyo vina kiki sana; ‘Nanihii kukaza’ pamoja na Simba kuendelea kushikilia usukani wa VPL. Halafu cha tatu ambacho kipo mawazoni mwa wadau wengi wa soka nchini hasa wale wanaofuatilia soka la majuu ni Pep Guardiola.

Guardiola anatajwa sana, halafu anayefuata kwa karibu ni Jose Mourinho na Man United yake kwa ujumla.

Antonio Conte yeye amepotea kabisa kwenye fikra na midomo ya wengi. Si mbaya sana, kwa sasa angalau anapumua kwa amani. Ni mwanamume pekee aliyefanikiwa kupata utulivu wa nafsi na akili wakati muhimu katikati ya mawimbi mazito pale Chelsea.

Kazi anayoifanya pale Stamford Bridge kwa sasa inaridhisha, nazungumzia katika msimu wa pili baada ya kuchukua ubingwa wa Premier League. Ni tofauti na ilivyokuwa kwa kocha aliyemtangulia darajani, Mourinho.

Mourinho kwa sasa anahangaika kuirudisha Manchester United kwenye reli, Conte amefanikiwa kutulia na kuifanya Chelsea ikae sawa kwenye reli ambayo Mourinho aliwahi kupita kwa misukosuko miaka miwili iliyopita.

Nani amesahau kilichomuondoa Mourinho pale Chelsea? Si kitu kigeni sana na ambacho kilikaribia kumfukuzisha kazi Conte darajani msimu huu.

Mourinho aliondoka kwa aibu Chelsea baada ya kuipa ubingwa msimu mmoja kabla, kilichomtoa pale ni baada ya kuifanya timu hiyo kumaliza katika nafasi mbovu mno ikiwa kama bingwa mtetezi.

Miezi saba tu baada ya kuchukua ubingwa wa Premier, Mourinho alisimamishwa kazi huku Chelsea akiiacha katika nafasi ya 16, tena ikiwa kwenye hatari kubwa mno ya kushuka daraja kuliko kutetea ubingwa.

Hiyo ikaongezwa kwenye historia ya makocha waliotimuliwa Chelsea halafu jina la Conte nalo likaandaliwa kuingizwa humo hasa baada ya kulumbana na mshambuliaji mahiri aliyeisaidia sana Chelsea, Diego Costa, kumkosa Romelu Lukaku katika vita ya kumwania dhidi ya Manchester United.

Na kingine kikubwa zaidi ni kumuuza kiungo mkabaji, Nemanja Matic kwenda Man United.

Kitendo cha nyota hao wawili, Lukaku na Matic, kuanza vizuri United kilisababisha maisha ya Conte yawe magumu Chelsea.

Kwanini? Sababu ni licha ya kubakiwa na akina Eden Hazard, Pedro, Willian sambamba na kusajili watu kama Tiemoue Bakayoko na Danny Drinkwater ambao waliangaziwa kama jeshi litakalomsaidia Conte kutetea ubingwa, bado alionekana kama kocha mwingine atakayefeli tu katika msimu wa pili.

Maneno mengi yalisemwa, wengi walimcheka na kumtabiria anguko msimu huu.

Presha ikawa kubwa, hata yeye mwenyewe alikaribia kuanguka kwenye kibarua chake, kazi ilitaka kumshinda.

Nimeamini, soka ni mchezo wa wazi na kila kinachotokea kwenye mchezo huu si maigizo. Sikuamini kama Chelsea itatulia hivi baada ya kuchukua ubingwa msimu uliopita baada ya changamoto za usajili.

Sikuamini kama Conte angefika mbali na Chelsea hii hasa kutokana na kutoelewana na watu kama Michael Emenalo ambaye alikuwa Mkurugenzi wa ufundi akisimamia sajili za wachezaji na mwanamama, Mkurugenzi mwingine wa klabu, Maria Granovska.

Lakini baada ya kutokea hayo yote, hadi kupelekea Emenalo kuondoka Chelsea, Conte aliamua kubaki na kutuliza akili yake kwenye mawimbi mazito ili kuilinda heshima yake kama kocha mwenye mafanikio Italia na England pamoja na kuilinda hadhi ya Chelsea kwa ujumla.

Ukizitaja timu zenye presha sana England, Man United inaongoza, ikifuatiwa na Chelsea. Inahitaji kocha mwenye busara sana kuzisimamia hizi timu. Conte amedhihirisha kuwa yeye ni jabali, mwamba, jembe anayeweza kuishi katika vipindi tofauti vya soka.

Guardiola kazi yake ishamalizika, ana nini kipya cha kuzungumziwa zaidi ya rekodi atakazoendelea kuzivunja?

Kwa sasa hebu tumwangalie Conte na jeshi lake la Chelsea, jeshi lililotulia na linaloelekea katika njia sahihi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*