UNAKUMBUKA Simba ilivyoikung’uta Al-Ahly 2-1, Kirumba 1985

NA HENRY PAUL

KESHO Simba wanatarajiwa kucheza na Al Ahly wa Misri katika mchezo wa marudiano wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Ikumbukwe, Simba iliwahi kuifunga mabao 2-1 Al Ahly katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika kabla ya kuitwa Ligi ya Mabingwa uliochezwa mwaka 1985, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Mchezo huo ambao ulikuwa ni mkali na wa kusisimua kwa muda wote wa dakika 90 na kuvuta hisia za wapenzi, ulikuwa ni wa kwanza wa raundi ya pili ya michuano hiyo.

Kabla ya mchezo huo, Simba walikuwa wamejiandaa vizuri kwa kuweka kambi ya mwezi mmoja mjini Mwanza katika Hoteli ya Victoria chini ya kocha wao mkuu, Abdallah Kibadeni ambaye alikuwa akisaidiana na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Mohamed Kajole (kwa sasa ni marehemu).

Katika mazoezi yao, Simba walikuwa wanajifua asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa Mabatini, wakiwa na lengo la kushinda mchezo huo na kuondoa ile dhana iliyojengeka kuwa timu za Tanzania haziwezi kufunga timu za Misri.

Siku ya mchezo huo, Uwanja wa CCM Kirumba ulifurika mno mashabiki kutoka nchi za jirani Uganda na Kenya.

Baadhi ya wapenzi na mashabiki hao waliokuwa wamefurika uwanjani hapo walisikika wakisema kuwa ni mara chache sana uwanja huo kujaa watu namna ile.

Mchezo ulianza kwa kasi, Al-Ahly wakiwashambulia Simba kutoka dakika ya kwanza kwa mashambulizi ya mfululizo kwa takribani dakika 15 za kipindi hicho cha kwanza.

Mashambulizi yao hayo ya mfululizo yalizaa matunda, kwani ndani ya dakika 15 za kipindi hicho cha kwanza walifanikiwa kupata bao la kuongoza.

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wao mahiri, Mohamood El Khatib ‘Bibo’.

Baada ya Al Ahly kupata bao hilo, hawakuishia hapo, kwani waliendelea kupeleka mashambulizi makali langoni mwa timu ya Simba, huku mabeki wakiwa na kazi moja tu ya kujitahidi kudhibiti mashambulizi hayo.

Katikati ya kipindi hicho cha kwanza, Simba walizinduka na kuanza kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza langoni mwa wapinzani wao, Al-Ahly wakiwa na lengo la kutaka kusawazisha.

Dakika 10 kabla ya mapumziko, Simba walifanya shambulio moja la nguvu langoni mwa timu ya Al Ahly na kufanikiwa kusawazisha.

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji mahiri, Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’, aliyepokea pasi kutoka kwa Malota Soma ‘Ball Juggler’.

Baada ya Simba kusawazisha bao hilo, mchezo ulibadilika na kuwa wa kushambuliana kwa zamu.

Kipindi cha pili kilipoanza, mchezo kwa kiasi kikubwa ulionekana kulingana, kwani mashambulizi sasa yakawa yanafanywa kwa zamu. Simba walikuwa wakishambulia na Al Ahly pindi walipokuwa wanapata nafasi walikuwa wanashambulia pia.

Pamoja na mashambulizi kufanywa kwa zamu, lakini walikuwa ni Simba ambao walikuwa wanafanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wao, kutokana na kwamba walikuwa wanashangiliwa mno na umati mkubwa uliokuwa umefurika uwanjani hapo.

Dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika, mashambulizi hayo ya Simba yalizaa matunda, kwani walifanya shambulio moja la nguvu langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kupata bao la pili.

Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Mtemi Ramadhani aliyepokea pasi kutoka kwa Mogela.

Baada ya Al Ahly kufungwa bao hilo walichachamaa na kuanza kulisakama lango la Simba kwa mashambulizi makali wakiwa na lengo la kutaka kusawazisha, lakini ngome ya Simba iliyokuwa ikiongozwa na Twalib Hilal ilikaa imara na kuzuia mashambulizi yote ya hatari yaliyokuwa yakielekezwa langoni mwao.

Pamoja na mabeki kufanya kazi ya ziada ya kuwazuia washambuliaji wa Al Ahly ambao walikuwa wana uchu wa kusawazisha bao, lakini pia kipa wa Simba, Moses Mkandawile, katika dakika hizo za mwisho aliokoa michomo mitatu ambayo ilikuwa inaelekea kutinga wavuni.

Simba; Moses Mkandawile, Kiwhelo Mussa (marehemu), Athumani Maulid (marehemu), Thobias Nkoma (marehemu), Twalib Hilal, Ramadhani Lenny (marehemu), Malota Soma ‘Ball Juggler’, Mtemi Ramadhani, Zuberi Magowa (marehemu), Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’ na Sunday Juma.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*