UNAHITAJI ‘ROHO YA PAKA’ KUWA KIONGOZI YANGA YA SASA

NA MICHAEL MAURUS


JUMAPILI iliyopita Yanga ilicheza na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wao wa nne wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Yanga ilipokea kipigo cha mabao 3-2 na kuzima ndoto za Wanajangwani hao kusonga mbele kwenye michuano hiyo, tayari kuwania Dola za Marekani 1,250,000 (Sh bilioni 2.8) zinazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa mshindi.

Mshindi wa pili anaondoka na kitita cha Dola za Marekani 625,000 (Sh bilioni 1.4), huku timu zitakazofika nusu fainali zikipata Dola 450,000 (zaidi ya Sh milioni 1), wakati zile zitakazoishia robo fainali zikizawadiwa Dola 350,000 sawa na zaidi ya shilingi milioni 700.

Hivyo, hadi sasa Yanga wana uhakika wa kupata Dola za Marekani 275,000, sawa na zaidi ya shilingi milioni 600 kwa kushika mkia katika Kundi D au hata kama itakamata nafasi ya tatu.

Ikumbukwe kuwa katika Kundi D, USM Alger ya Algeria ndiyo inayoongoza ikiwa na pointi nane sawa na Gor Mahia inayofuatia, huku Rayon Sports ya Rwanda, ikiwa na pointi tatu, Yanga ikijikusanyia moja tu.

Mbaya zaidi, katika makundi yote manne ya michuano hiyo, Yanga ndiyo iliyofungwa mabao mengi zaidi hadi raundi ya nne, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11, huku pia ikiwa ndiyo timu yenye pointi chache zaidi yaani moja.

Kwa kifupi, hadi kufikia raundi ya nne ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho, Yanga ndiyo timu dhaifu zaidi.

Ukiachana na hayo, juzi kwenye Uwanja wa Taifa, kikosi cha Yanga kilicheza kwa kiwango cha chini mno kiasi cha mashabiki kujikuta wakichanganyikiwa na kuanza kuwatupia lawama viongozi wao waliokuwa wamekaa jukwaa kuu, yaani VIP A wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Wanajangwani hao, George Mkuchika.

Binafsi bao la kwanza la Gor Mahia wakati linafungwa, nilikuwa ndio ninaingia uwanjani hapo nikiwa na wanahabari wenzangu waliokuwa na shauku kuona iwapo Yanga ‘wangepindua meza kibabe’ kama alivyotamba Msemaji wa klabu hiyo, Dismas Ten.

Baada ya kuingia uwanjani, nilishuhudia dakika takribani 85 za mchezo huo ambapo Yanga walionekana kama timu ya Umitashumta mbele ya Gor Mahia, wakizidiwa katika kila idara na hatimaye kupewa kipigo hicho.

Japo Yanga walipata mabao mawili, lakini yalionekana kuwa ya ‘kuungaunga’ tofauti na yale ya wapinzani wao ambao ni mabingwa wa Kenya na michuano ya SportPesa Super Cup iliyofanyika nchini kwao hivi karibuni.

Japo wapo baadhi ya watu wa Yanga waliokuwa wakitamba kuwa walifungwa kwa kuwa waliwakosa wachezaji wao wapya, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Heritier Makambo kutoka DR Congo, lakini ukweli ni kwamba bado hawastahili kuongea wanapokutana na watani wao wa jadi, Simba.

Kimsingi, kikosi cha Yanga cha msimu huu hakitoi mwanga wowote wa kutoa upinzani mbele ya Simba iliyosajili vifaa vitupu, Azam, Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons, Kagera Sugar na nyinginezo.

Hakuna majina ya kutisha katika usajili wa Yanga, ni wachezaji wa kawaida tu ambao hata kidato cha kwanza hawezi kuwa na hofu kukabana nao.

Ukiwaondoa Papy Tshishimbi na Ibrahim Ajib mwenye kipaji cha kipekee kilichokosa matumizi, wachezaji wengine wote waliobaki ni wa kawaida tu ambao hata Majuto Omary wa timu ya Taswa FC, anaweza kukabiliana nao pamoja na kitambi chake.

Unapokilinganisha kikosi cha Yanga cha safari hii na kile cha Simba kilichojichimbia nchini Uturuki, kuna tofauti kubwa sana. Kuna wachezaji wenye majina ya kuogopesha na viwango vya juu kuanzia safu ya ulinzi, kiungo hadi ushambuliaji.

Nani wa kulaumiwa kutokana na kikosi hiki cha Yanga? Binafsi naamini ni viongozi waliopo madarakani.

Kuna ‘komandoo’ mmoja wa Yanga wakati mchezo wa Jumapili ukiendelea aliniomba tuzungumze na kuwatetea viongozi wa klabu hiyo kwamba wao si tatizo, bali yote hayo yametokana na ukosefu wa fedha kiasi cha kuwakwamisha viongozi kushindwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu.

Nilimwambia kuwa kitendo cha kushindwa kupata fedha za kusajili wachezaji, kulipa mishahara na posho nyinginezo, ni udhaifu mkubwa unaoondoa sifa ya mtu kuwa kiongozi, hasa wa klabu ya soka.

Nilimwambia kuwa Yanga ina watu kama Salim Abdallah ‘Try Again’ zaidi ya 100, watu wa aina ya Mohammed Dewji ‘Mo’, zaidi ya 50 na matajiri wengine wengi tu, lakini tatizo ni nani wamkabidhi fedha zao.

Ili mtu akukabidhi fedha uiendeshe timu, lazima akupime ulivyo (image), hakuna tajiri anayeweza kuingiza fedha zake sehemu ambayo hana uhakika na usalama wa fedha hizo au hana uhakika kama zitatumika kama ilivyokusudiwa.

Tunaona katika uongozi wa sasa wa Simba, fedha si tatizo, klabu hiyo ina uwezo wa kusamjili mchezaji yeyote yule. Wekundu wa Msimbazi hao chini ya Try Again, wana uwezo wa kumsajili hata Yaya Toure raia wa Ivory Coast.

Matajiri wa Simba hawana shaka na fedha zao linapokuja suala la kuichangia timu yao kwa kuwa wanaamini Try Again hawezi kuwaangusha hata kidogo.

Ndiyo. Hata ndani ya Yanga, iwapo kungekuwa na viongozi wa aina ya Try Again, sidhani kama leo hii klabu hiyo ingekuwa ikilialia njaa kiasi cha kushindwa kuwaongezea mikataba wachezaji wao walioitumikia timu kwa ‘jasho na damu’ kama Hassan Kessy au Kelvin Yondani.

Ni Kessy na Yondani hawakuifanyia Yanga msimu uliopita? Pamoja na matatizo ya kifedha, bado waliitumikia timu yao kwa uwezo na nguvu zao zote kiasi cha kujikuta wakati mwingine wakipandwa na jazba na kucheza rafu zisizo na lazima kutokana na uzembe wa baadhi ya wenzao.

Lakini mwisho wa siku, Yondani alisaini mkataba mpya saa chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa kisa ni shilingi milioni 80 alizotaka akifahamu kuwa dau hilo linaweza kuwa la mwisho kwake wakati huu umri unavyozidi kumpa mkono.

Kwa upande wake, Kessy ataukosa msimu huu na hivyo kuwanyima uhondo mashabiki wa Yanga kutokana na udhaifu wa viongozi wa timu hiyo walioshindwa kumalizana naye.

Kuna mashabiki lukuki wa Yanga wanaonipigia simu kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakiniuliza nini suluhisho la kuitoa Yanga hapa ilipo?

Mara zote jibu langu limekuwa ni moja tu, viongozi wote wa Yanga kujiuzulu kama alivyofanya Mwenyekiti wao, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na baadhi ya wajumbe.

Hapa ninamaanisha wajumbe wa kada zote, kuanzia ya usafi kama ipo hadi ya utendaji. Kwa hali ilivyo, kunatakiwa sura mpya kabisa ndani ya Yanga kwa sasa.

Nimekuwa nikijiuliza iwapo viongozi waliobaki madarakani Yanga hadi sasa wanawaonea huruma ndugu na jamaa zao. Hivi kuna mtoto, kaka, dada, mzazi, mke, mume, rafiki au jirani ambaye anaweza kujivunia kuwa ana ndugu ambaye ni kiongozi wa Yanga ya sasa?

Kwa lipi hasa? Kumsajili Fei Toto na Deus Kaseke, huku Simba wakiwa wamemnasa Adam Salamba, Cletous Chama na Meddie Kagere? Au kuna mtu anaweza kujitambulisha mbele za watu kuwa yeye ni kiongozi wa Yanga wakati ameshindwa japo kumbakiza Kessy Jangwani?

Ama kwa hakika, unahitaji kuwa na roho ya paka kuendelea kung’ang’ania uongozi wa Yanga hii ambayo inakubali kufungwa mabao saba na Gor Mahia, ikiwa ni timu nyanya zaidi kati ya zote zilizotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika hadi mechi za raundi ya nne.

Usikose nakala yako ya BINGWA la Jumamosi ambapo nitakuletea kigongo kuhusiana na Yanga hii ya sasa ambayo iwapo hakutafanyika jitihada za makusudi kabisa, watu watapoteza maisha Septemba 30, mwaka huu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*