UDHAMINI LIGI YA WANAWAKE USIWE KAMA WA FDL

NA ZAINAB IDDY

WADAU wa soka nchini walikuwa na kilio cha muda mrefu juu ya uwekezaji kwenye Ligi Kuu ya Wanawake kwa lengo la kuiboresha na kuongeza ushindani kwa timu shiriki.

Alhamisi iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kusaini mkataba wa miaka mitatu wa kuidhamini ligi hiyo kupitia Bia ya Serengeti Lite.

Mkataba huo uliosainiwa na Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura mbele ya kiongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), una thamani ya Sh milioni 450 na pia ni udhamini wa kwanza tangu ligi hiyo ilipoanzishwa.

Hili ni jambo la kupongezwa hasa kwa TFF ambao wamehangaika huku na kule kutafuta mdhamini wa kuongeza nguvu katika ligi ya wanawake ambayo sasa imeanza kuwa na msisimko wa aina yake kutokana na ushindani uliopo kati ya timu shiriki.

Kupatikana kwa mdhamini huyo kutasaidia kuinua viwango vya wachezaji kwa kuwa klabu zao zitakuwa na fedha ambazo zitatumika kuwalipa mishahara.

Lakini pia itasaidia kuimarisha ligi hiyo kwa sababu klabu zitakuwa na fedha za kutosha kumudu gharama mbalimbali za kuendeleza timu zao hususan kwenye masuala ya usafiri, huduma za malazi na mambo mengine muhimu.

Ni dhahiri kuwa Ligi Kuu ya Wanawake tayari imeanza kuwateka wapenzi wengi wa soka kwani baadhi yao wamekuwa wakiifuatilia kwa karibu hasa ilipoanza katika mzunguko wa kwanza.

Hatua hiyo ni ishara kuwa hata kampuni ambazo zitajitokeza kujitangaza kupitia ligi hiyo zitakuwa zimejiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kukuza biashara zao.

Kama uwekezaji utafanywa kikamilifu katika soka la wanawake, ni wazi Tanzania itakuwa na ligi bora kuanzia ngazi za wilaya hadi Ligi Kuu, lakini pia kikosi bora cha timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ kinaweza kupatikana kwa urahisi.

Waswahili wanasema: “Penye neema hapakosi fitina,” mara nyingi vyama vya michezo hapa nchini vimekuwa vikichangia kuibuka kwa matatizo hasa baada ya kupatikana wadhamini wanaotaka kusapoti mashindano, kwani baadhi ya viongozi hutumia mamlaka waliyonayo kuzinyonya timu husika.

Hili ni jambo lisilo na kificho kwani tumeshuhudia katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), baadhi ya timu shiriki zikihangaika kutokana na kutopata mgawo unaostahili ambao unatolewa na wadhamini au kushindwa kupata kwa wakati mwafaka wa kuandaa timu.

Mbali na FDL, tatizo hilo pia lilijitokeza katika ligi ya vijana chini ya miaka 20 iliyofanyika mwaka jana, wachezaji hawapati haki wanazostahili kwa wakati jambo linalosababisha kupunguza ubora wa ligi husika.

Sasa ni wakati wa TFF ambao ndio wenye dhamana ya kusimamia soka hapa nchini kutumia nafasi zao kutenda haki katika suala zima la utoaji mgawo unaotoka kwa mdhamini aliyejitosa kusaidia soka la wanawake kwa wakati.

Usimamizi mzuri utasaidia kuongeza morali na hamasa kwa timu shiriki kufanya maandalizi kikamilifu na kuifanya ligi kuwa yenye ushindani wa kweli.

Kwa upande wa timu shiriki zinapaswa kutambua kuwa upatikanaji wa kampuni zinazotaka kudhamini ligi ni suala ambalo halitokei mara kwa mara, hivyo ni vema kuyatimiza malengo yaliyotarajiwa kwa hao waliopatikana.

Jambo muhimu ni kuwepo kwa uwazi wa kutosha ili mdhamini afahamu matumizi sahihi ya kile anachokitoa kuliko kusikia malumbano yasiyo na tija kila mara ambayo mwisho wa siku yanaweza kumkimbiza na kuwakatisha tamaa wengine wenye nia ya kusaidia soka la wanawake.

Hata hivyo, kuna haja ya TFF kuomba udhamini uwe mkubwa zaidi kwa sababu kampuni inapata fursa kubwa ya kujitangaza kupitia timu hizo.

Pia wachezaji waliopo katika klabu za wanawake wanatakiwa kutambua thamani yao kwenye ligi wanazoshiriki ambazo kwa kiasi kikubwa ndizo zinachangia kuibua vipaji na viwango vyao kuonekana ndani na nje ya nchi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*