Uchaguzi Yanga wasitishwa

NA HUSSEIN OMAR

MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), , ametangaza kusogeza mbele uchaguzi wa klabu ya Yanga hadi hapo watakapotoa taarifa.

Uchaguzi wa Yanga ulipangwa kufanyika kesho ili kujaza nafasi ambazo zipo wazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, uchaguzi huo umesogezwa mbele na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa Jumatatu.

Akizungumza na BINGWA jana, Mchungahela alisema wameamua kuusimamisha kwa sasa kutokana na baadhi ya wanachama kuweka pingamizi mahakamani.

“Wakati tupo kwenye kikao tulipata taarifa kuwa kuna baadhi ya wanachama kutoka Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Morogoro wamefungua kesi ya kuusimamisha,” alisema Mchungahela.

“Sisi kama kamati hatutaki kugongana na mhimili wa mahakama, tumesikia wameanza kusikiliza mashauri, hivyo  tumeamua kusimamisha uchaguzi kufanyika siku ya Jumapili hadi  tupate ruhusa ya mahakama,” alisema.

Alisema ifikapo Jumatatu watatoa taarifa, huku akiwataka hata wale wagombea  ambao wanaendelea na kampeni wasitishe kwa sasa, ikiwamo mdahalo uliopangwa kufanyika jana na kurushwa live na kituo cha televisheni cha Azam TV.

Wagombea watatu waliopitishwa kuwania nafasi ya uenyekiti ni Dk. Jonas Benedict Tiboroha, Mbaraka Hussein Igangula na Erick Ninga, huku Yono Kevela, Titus Eliakim Osoro na Salum Magege Chota wakiwania umakamu mwenyekiti.

Wagombea 16 wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji Yanga ni Hamad Ally Islam, Benjamin Jackson Mwakasonda, Sylvester Haule, Salim Seif, Shafil Amri na Said Kambi.

Wengine ni Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Ally Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Peter Kazige.

Uchaguzi huu ni maalumu kuziba nafasi za wagombea waliojiuzulu kwa nyakati tofauti baada ya uchaguzi wa Juni 11, mwaka 2016.

Waliojiuzulu ni aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.

Wajumbe waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni wane tu ambao ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*