UCHAGUZI SIMBA UMEPITA SASA NI KAZI

HATIMAYE Simba imefanya uchaguzi wake mkuu uliotawaliwa na utulivu wa hali ya juu na kushuhudia wanachama wakiwaweka madarakani viongozi wanaoamini wataendana na mfumo mpya wa uongozi.

BINGWA tunatoa pongezi zetu za dhati kwa wanachama wa Simba kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaoamini wataifanya klabu yao isijulikane kama kongwe tu bali kubwa ili iweze kushindana na miamba ya Afrika kama vile TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Al Ahly ya Misri na Esperance ya Tunisia.

Aidha, tunatoa pongezi za dhati kwa uongozi mpya uliochaguliwa na kuwakumbusha kwamba wanalo deni kubwa kwa wanachama ambao wanataka kuona mafanikio ndani na nje ya uwanjani na si malumbano au uongozi unaokumbatia rushwa.

Pongezi nyingine ni kwa wagombea waliojaribu lakini kura hazikutosha kwa sababu tunaamini waliochaguliwa ni Simba na ahadi walizozitoa wakati wa kampeni zitafanyiwa kazi na uongozi mpya ili Simba iwe tishio Afrika.

Uchaguzi mkuu wa Simba uliofanyika Jumapili na matokeo kutangazwa alfajiri ya jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, ulishuhudia Swedi Nkwabi, akichaguliwa mwenyekiti wa bodi ya ukurugenzi kupitia wanachama.

Nkwabi alikuwa mgombea pekee na alichaguliwa kwa kura nyingi baada ya gwiji wa klabu hiyo aliyeichezea Simba kwa mafanikio, Mtemi Ramadhani, kujitoa dakika za mwishoni. Ni uchaguzi ulioshuhudia viongozi wote waliomaliza muda wao; Iddi Kajuna, Said Tully, Ally Suru na Jasmine Costa, wakiangushwa.

Wajumbe waliochaguliwa kuingia katika nafasi ya ukurugenzi ni Hussein Kitta Mlinga, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Suleiman Haroub Said, Mwina Mohammed Kaduguda na Asha Ramadhani Baraka.

Kilichopelekea Simba kufanya uchaguzi ni uongozi uliochaguliwa Juni 30 mwaka 2014 chini ya Rais Evans Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na wajumbe waliotajwa hapo juu kumaliza muda wao.

Uongozi uliomaliza muda wake umeshuhudia viongozi wake wawili; Aveva na Kaburu, wakiwa rumande tangu Juni 29 mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

BINGWA tunatoa pongezi za kipekee kwa Kaimu Rais, Salum Abdallah ‘Try Again’, aliyeteuliwa na kamati ya utendaji Julai 1 mwaka jana kwa namna alivyosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu hadi kufanyika uchaguzi huo kwa hali ya utulivu.

Tunaamini Nkwabi amechaguliwa na wanachama kwa sababu amekidhi matakwa ya katiba mpya ya Simba ambayo inataka mwenyekiti atakayeongoza bodi ya wakurugenzi itakayokuwa na wajumbe wanane huku pia akiwa na mamlaka ya kuteua wajumbe wengine wanne awe na elimu ya shahada.

BINGWA pia tunatoa pongezi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Friends of Simba, Crescentius Magori, kuteuliwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) tukiamini yeye ni mtu sahihi kwa kushirikiana na uongozi mpya kuifanya Simba kuwa tishio Afrika.

 

 

 

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*