UBABAISHAJI TTA UNAUA TENISI

KATIKA ukurasa wa 12 wa gazeti hili, kuna makala ambayo inaeleza jinsi gani ubabaishaji wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA) unavyozidi kuupoteza mchezo huo wenye mashabiki lukuki nchini.

Makala hiyo imeeleza jinsi gani ubabaishaji katika chama hicho umechangia kujiuzulu kwa nyakati tofauti viongozi wa juu wa TTA, ambapo alianza kujiuzulu Rais wa chama hicho, Methusela Mbajo na baadaye Makamu wake, Fina Mango.

Imeelezwa kuwa tangu wawili hao wajiuzulu, chama kimekuwa chini ya Katibu Mkuu, William Kallage na Msaidizi wake, Joshua Mutale ambao kwa namna moja au nyingine wanaonekana kushindwa kukiendesha chama hicho.

Licha ya kutakiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kufanya mabadiliko ya Katiba na kuitisha Uchaguzi Mkuu, wawili hao wameshindwa kutimiza agizo hilo na kuendelea kuendesha chama hicho bila kuitisha uchaguzi.

Makala hiyo imeeleza wazi kuwa ni mwaka mmoja sasa umepita tangu uongozi wa muda wa chama hicho ulipoitwa mbele ya Kamati ya Nidhamu, Usuluhishi na Rufaa ya BMT na kutakiwa kuyafanyia kazi mapungufu yaliyopo kabla ya kuitisha uchaguzi wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi.

Licha ya hayo yote, hali bado ni tete ndani ya chama hicho na mchezo wa tenisi kwa ujumla unazidi kudidimia nchini, hasa katika kipindi hiki kutokana na kukosekana kwa mashindano yoyote ya taifa, huku vipaji vya vijana wenye uwezo wa kucheza mchezo huo vikizidi kumpotea.

Kutokana na hali hiyo, BINGWA tunasikitishwa na hali ya mambo ilivyo ndani ya TTA, maana tunafahamu katika mazingira haya ya ubabaishaji itakuwa ngumu sana kuuendeleza mchezo huo unaokubalika sana nchini.

Tunasema kama viongozi wa mpito wa chama hicho wameshindwa kukisimamia, basi nao waachie ngazi kama wenzao ili kutoa nafasi kwa watu wenye nia ya dhati ya kuendeleza mchezo huo wakiongoze.

Tunaamini ili mchezo wa tenisi uendelee nchini, basi ni lazima Katiba ya TTA irekebishwe na uitishwe uchaguzi mkuu ambao utachagua watu wa kuingia kuendeleza chama hicho, kwa sababu ubabaishaji wa sasa unaua tenisi nchini.

Tunaitaka BMT kuchukua uamuzi mgumu dhidi ya TTA na uongozi wake ili kuhakikisha uchaguzi unaitishwa haraka iwezekanavyo na kupatikana uongozi mpya wa kuendeleza mchezo huo.

Tunaamini kama BMT ikilivalia njuga suala la uchaguzi wa TTA kama ambavyo imekuwa ikifanya kwenye mchakato wa mabadiliko kwenye klabu za Simba na Yanga, utafanyika mapema zaidi ya watu wanavyodhani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*