googleAds

UAMUZI MGUMU YANGA

NA WINFRIDA MTOI

PAMOJA na kupata ushindi wake wa kwanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Coastal Union juzi, uongozi wa Yanga umepanga kufanya uamuzi mgumu ili kuwapa raha wapenzi mashabiki wao.

Yanga ilianza Ligi Kuu Bara kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting, kabla ya kubanwa mbavu na Polisi Tanzania kwa sare ya mabao 3-3, mechi zote hizo zikipigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo wao wa tatu wa juzi dhidi ya Coastal Union, Yanga walishinda bao 1-0, shujaa wao akiwa ni kiungo Abdulaziz Makame.

Hata hivyo, wapenzi wa timu hiyo wameonekana kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi chao, wakiamini matokeo wanayopata, hayalingani na fedha walizotumia kuisuka upya timu yao.

Baada ya mechi hizo chache za ligi na kuondolewa kwao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wapenzi wa Yanga wanajiona kama ‘wameuziwa mbuzi kwenye gunia’.

Kati ya vitu vinavyowaumiza Wanajangwani hao, ni matokeo ya watani wao Simba, kwani hawajapoteza hata pointi moja Ligi Kuu Bara, licha ya kukutana na timu ngumu kama Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Na kati ya vitu vinavyowaumiza zaidi watu wa Yanga, ni kuona safu yao ya ushambuliaji ikishindwa kuwapa raha, pamoja na kusajili wachezaji wa kigeni kwa gharama kubwa.

Wachezaji wa kigeni wanaounda safu ya ushambuliaji ya Yanga ni Juma Balinya, Sadney Urikhob, Issa Bigirimana, Maybin Kalengo, David Molinga na Patrick Sibomana ambao wote ni wapya.

Japo ilielezwa kuwa wachezaji hao ni ‘vifaa’, lakini hadi sasa bado hawajawakuna wapenzi wa Yanga, wakionekana kuwa mizigo kutokana na viwango wanavyovionyesha ambavyo ni vya kawaida sana.

Pamoja na hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera anayeelezwa kuwa ndiye aliyependekeza kusajiliwa kwa wachezaji hao, amekuwa akisisitiza kupewa muda wa kujenga muunganiko wa vijana wake hao.

Lakini kwa kuwa soka ni mchezo wa wazi, watu wa Yanga wanaonekana tayari wameshapata majibu juu ya viwango vya wachezaji hao na sasa wanaushinikiza uongozi kusaka wengine watakaowapa raha.

Mbaya zaidi, presha ya mashabiki dhidi ya viongozi wao, imekuwa kubwa kwa sababu walichangia fedha za usajili kupitia kampeni ya Kubwa Kuliko iliyozalisha mamilioni ya fedha.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa tayari uongozi wa klabu hiyo, umekubali matokeo na muda wowote kutafanyika uamuzi mgumu utakaoligusa benchi la ufundi pamoja na wachezaji, hasa wa kigeni.

“Kuna panga kubwa linakuja, sidhani kama litamwacha mtu salama, hata mwalimu Zahera anaweza kujikuta akipoteza nafasi yake. Kuna uwezekano wakabaki wachezaji wanne tu wa kigeni, wengine wote wakatemwa,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakupenda jina lake liwekwe wazi.

Juu ya kilio hicho cha wapenzi wa Yanga, Mwenyekiti wao, Dkt. Mshindo Msolla, aliwataka kutulia akisema uongozi wake umesikia kilio chao, hivyo kuwa katika mchakato wa kukifanyia kazi.

Alisema ndani ya muda mfupi ujao, mambo yatakuwa mazuri ndani ya klabu hiyo na kikosi chao kitakuwa moto wa kuotea mbali.

“Tumesikia malalamiko yenu, tunayafanyia kazi. Tunafahamu Yanga wanataka furaha, uongozi unapambana kuona kila kitu kinakaa sawa,” alisema.

Aliwataka kutosikiliza maneno ya watu kuwa kuna mgogoro ndani ya klabu hiyo, ikidaiwa haelewani na makamu wake, Frederick Mwakalebela jambo lisilokuwa na ukweli wowote.

“Yanga hakuna mgogoro wowote, viongozi tunafanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri, watu wanaosema maneno hayo ni wale wenye nia mbaya na klabu yetu.

“Niwaondoe hofu, viongozi wetu tupo makini, tunapambana na msimu huu ubingwa utakuwa wetu, hakuna kusikiliza maneno ya watu tunaona na tunafanyia kazi kila kitu, lengo ni moja Wanayanga wawe na furaha,” alisema Msolla.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*